Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
LIMETOKEA jambo baya katika nchi
yetu linaloweka historia kwa kiongozi wa serikali, ngazi ya uwaziri
kupoteza kazi kwa sababu ya ulevi. Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga amefukuzwa kazi na Rais Dk. John Magufuli kwa sababu ya mteule
wake huyo kuzidisha kilevi kilichomfanya kushindwa kutimiza majukumu
yake sawasawa.
Kuna mambo mengi yanazungumzwa
juu ya hatua iliyochukuliwa, wengi wakimpongeza rais kwa nia yake ya
dhati ya kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa maadili,
uwajibikaji na nidhamu.
Ni kweli kwamba kuna kundi kubwa la watu
wanaokunywa pombe, baadhi yao wakipitiliza na kujikuta wakishindwa
kufanya kazi au kufanya vyema katika majukumu yaliyo mbele yao, lakini
pia wakishindwa kuweka sawa mambo yao.
Lakini ulevi wa pombe una madhara kidogo
sana kwa jamii yetu kuliko ulevi wa madaraka walionao viongozi wengi
katika serikali yetu. Hapa ninazungumzia watu kama wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa idara, wakuu wa mikoa, maofisa wakubwa mikoani,
wakurugenzi walio wizarani, manaibu mawaziri na hata mawaziri wengine.
Ulevi huu wa madaraka upo pia hadi kwa
maofisa watendaji wa ngazi za vijiji na kata, achilia mbali watu
waliopewa dhamana ya kulinda uhai wa watu kama madaktari na polisi.
Kabla ya kuingia madarakani kwa serikali hii ya Magufuli, wananchi walikuwa wakiteswa sana na kauli kama ‘unajua mimi ni nani?’.
Kauli hizi zilitolewa na viongozi hao
wakati wananchi wakiwa wanahitaji huduma zao, lakini wanacheleweshewa au
kunyimwa. Mbaya zaidi, wakati mwingine zinatolewa hata na watoto wao,
vimada wao, wake zao, wajomba zao au wategemezi wengine kwa sababu tu
waziri, mkuu wa mkoa au bosi wa mamlaka ni baba, mjomba, shangazi au
unasaba mwingine.
Ulevi huu upo sana kwa viongozi wa
serikali, wanataka wananchi wawaogope, wakienda kutaka huduma,
wanyenyekewe, wakati ukweli ni kwamba wanaopaswa kunyenyekewa ni
wananchi kwa sababu ndiyo waajiri.
Ni vyema, Rais Magufuli akamulika eneo
hili na wananchi wapo tayari kumsaidia. Kuna mabosi wanafika kazini muda
wanaotaka, wanafanya kazi pale wanapojisikia na wanatoa lugha za kejeli
na masimango bila kujali kana kwamba ni shughuli zao binafsi.
Tunajua jeshi la polisi kwa mfano,
linaendeshwa kwa fedha za walipa kodi, lakini siyo jambo la ajabu kwamba
wananchi wanapokwenda kupeleka matatizo yao, baadhi ya askari waliolewa
madaraka wanawalazimisha kutoa hela ya mafuta ili waende kufuatilia
tatizo lake.
Shida kama hizi wanazipata karibu katika ofisi zote za umma ambazo zimewekwa kwa ajili ya kuwahudumia.
Ni afadhali ya ulevi wa pombe kwa sababu
wanakunywa kwa pesa zao, lakini ulevi huu unawaumiza watu wasiostahili,
tena katika ofisi za umma.
Vyema Rais Magufuli akautazama ulevi
huu. Wananchi wanawajua watumishi wa umma waliolewa kilevi hiki na wako
tayari kuwataja ili nao wawajibishwe kama ilivyotokea kwa Charles
Kitwanga.
Nachochea tu!
0 comments:
Post a Comment