Stori: Gabriel Ng’osha, Wikienda
Dar es Salaam: Kunani bandarini? Kufuatia ziara za kila kukicha za kushtukiza za bandarini za Waziri Mkuu, Cassim Majaliwa, baadhi ya Wabongo wamekiri kwamba, kwa vyovyote kuna kitu waziri mkuu amegundua au anakifahamu juu ya utendaji wa wahusika.
Baadhi ya waliozungumza na Ijumaa Wikienda ndani ya Bandari ya Dar walisema kuwa wana imani kubwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ na waziri mkuu ambaye anaonekana kugundua mianya mingi ya ufisadi bandarini ambayo kama ikidhibitiwa vizuri bandari pekee inaweza kuendesha nchi kama ambavyo aliwahi kusema Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
“Kuna kitu kikubwa ambacho sisi wananchi wa kawaida hatukifahamu ila Serikali ya Magufuli
inafahamu umuhimu wa mahali hapo na ndiyo maana inapakomalia,’’ alisema Baraka Ndege, mkazi wa Sinza, Dar.
Kauli za wananchi hao zinakuja mara baada ya waziri mkuu huyo kushtukiza katika Kitengo cha Upimaji Mafuta Bandarini kilichopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kubaini kuwa mita za kupima mafuta (Oil Flow Meters) zikiwa zimejaa kutu kutokana na kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano.
Waziri Majaliwa anaamini uzembe huo umeligharimu taifa kwa kupoteza mapato ya miaka mitano, jambo lililosababisha kumpa saa nne, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo.
Katika ziara hiyo pia ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini, hali iliyomlazimu waziri mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.Baadhi ya vitengo vilivyotumbuliwa katika bandari hiyo ni Forodha, Bodi ya TPA na WMA.
0 comments:
Post a Comment