Wanafunzi katika shule ya msingi Kivukoni iliyoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wilayani Songea mkoani Ruvuma wanasomea katika vibanda vilivyoezekwa kwa makaratasi ya nailoni na nyasi baada ya majengo ya shule yao zikiwemo ofisi za walimu kuharibiwa na ufa na hivyo walimu wameomba watalaamu wa miamba kuchunguza tukio hilo.
Kufuatia tukio hilo la shule hiyo yenye miaka kumi na nane kuharibiwa kwa ufa uliopasua sakafu na kuta zote za shule hadi nje ya shule walimu wa shule hiyo wameiomba serikali kutuma watalaamu wa miamba kuchunguza tukio hilo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kivukoni Bw. Hakim Kais amesema shule hiyo kuharibiwa na ufa ni maafa na kuomba serikali ya wilaya kuwasaidia kupitia mfuko wa maafa badala ya kuagiza wachangishane shilingi elfu ishirini kila mwananchi huku mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Erick Ndunguru akiiomba serikali kusaidia ujenzi wa shule hiyo kwani wanafunzi wamekuwa watoro kutokana na mazingira magumu ya kusomea.
Wanafunzi wa shule hiyo wanaelezea mazingira magumu wanayosomea na kuiomba saerikali kuharakisha ujenzi wa shule hiyo ambapo toka shule imefungua wanafunzi kumi na tano hawajaripoti kutokana na mazingira magumu ya kusomea.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Songea Bw. Sigsbert Valentine amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza jitihada zilizofanyika.
0 comments:
Post a Comment