Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.
Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.
Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa ameanza kuchanganya bangi na Cocaine kwa lengo la kupunguza msongo wa mawazo, jambo linalosababisha mabadiliko makubwa kwenye tabia yake. Diego naye anaanza kumshawishi wamuibie Msuya na kutoroka. Safari hii anatumia vitisho ambapo Arianna anakosa ujanja zaidi ya kukubaliana naye. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Kesho yake asubuhi, Msuya aliwahi kuondoka kuelekea kwenye shughuli zake kama kawaida. Alipoondoka tu, Arianna naye aliamka na kumfuata Diego, mkononi akiwa na funguo za gari moja la kifahari la Msuya.
Kwenye mkoba wake mdogo, alikuwa amebeba kadi za benki (ATM) karibu tano, zote akiwa tayari anajua namba zake za siri. Akamuamsha Diego na kumpa funguo za gari, wakawadanganya wafanyakazi kwamba wanaenda kliniki kwa sababu Arianna hakuwa anajisikia vizuri. Wakatoka Diego akiwa ndiyo dereva.
Breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye benki ya kwanza, Arianna na Diego wakateremka kwenye gari na kwenda mpaka kwenye mashine ya ATM na kutumbukiza kadi ya kwanza. Baada ya kuingiza namba za siri, Arianna alibonyeza kitufe cha ‘kutazama salio’.
Akaunti hiyo moja tu ya Msuya, ilikuwa na jumla ya shilingi milioni 47 za Kitanzania, wote wakashusha pumzi ndefu na kutazamana.
“Tuzitoe hizi kwanza mengine yatafuatia baadaye,” alisema Diego huku akionesha kuwa na papara zisizo za kawaida.
“Lakini si unajua hatuwezi kuzitoa zote mara moja, kwa leo tunaruhusiwa kutoa mpaka shilingi milioni mbili tu, tena kwa awamu, huo ndiyo utaratibu wa kutoa fedha ATM,” alisema Arianna na kuanza kumfafanulia Diego ambaye alikuwa mgeni na matumizi ya mashine za ATM.
“Basi siyo mbaya, leo tutoe hapa kidogo, tuhamie kwenye benki nyingine nako tukatoe kidogo mpaka tuzimalize kisha tutarudi tena kesho mpaka tutoe zote,” alisema Diego, wakakubaliana ambapo walitoa shilingi laki tanotano kwa awamu nne, jumla ikawa shilingi milioni mbili, wakarudi kwenye gari na kuhamia kwenye benki nyingine.
“Hebu angalia salio? Maana nahisi kama nashindwa kuzisoma hizo namba,” alisema Arianna baada ya kuwa wameshaingiza namba za siri kwenye mashine ya ATM. Salio lilisomeka kuwa shilingi milioni mia moja na laki mbili, wote wakapigwa na butwaa tena.
“Mh! Huyu mzee ana pesa nyingi kiasi hiki? Kumbe biashara ya madini inalipa namna hii?” Diego alisema akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona. Kama walivyofanya kwenye ATM ya kwanza, walichukua shilingi milioni mbili na kuhamia kwenye benki nyingine. Mpaka wanakamilisha mizunguko yao, tayari walikuwa na shilingi milioni kumi mfukoni.
“Umeangalia chumbani kwenu kama kuna fedha na madini kama nilivyokwambia?”
“Daah! Nilisahau ujue, turudi nyumbani sasa hivi nikaanze kupekua kabla muda wa Msuya kurudi haujafika,” alisema Arianna, wakaingia kwenye gari na kuziweka vizuri shilingi milioni kumi walizokusanya siku hiyo na kurejea nyumbani.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, Arianna alienda moja kwa moja mpaka chumbani kwao na kuanza kupekua kila sehemu. Kama Diego alivyokuwa amehisi, ndani kulikuwa na shehena ya madini ya Tanzanite iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kabati gumu chumbani humo.
“Whaoo! Madini mengi kiasi hiki?” alisema Arianna na kurudisha kila kitu mahali pake harakaharaka, akaendelea kupekua ambapo aligundua fedha nyingine nyingi, zaidi ya shilingi milioni sitini zikiwa kwenye droo ya kitanda. Ndani ya droo hiyo, pia Arianna alikutana na bastola ambayo bila hata kuuliza, alijua ni ya mumewe anayotumia kujilinda.
Hakutaka kupoteza muda, alitoka haraka na kwenda mpaka kwenye chumba cha Diego, akatazama huku na kule na alipohakikisha hakuna aliyekuwa anamuona, aliingia mpaka ndani. Akamueleza Diego kila kitu alichokiona.
“Mungu wangu, kumbe pia ana bastola? Sasa akigundua kwamba tunamfanyia njama si atatuua? Unaaonaje tutoroke leoleo?”
“Mh! Acha papara Diego, yaani wewe ukishaona pesa akili zinahama kabisa,” alisema Arianna, ikabidi Diego atulie.
“Kwanza jana aliniambia kwamba ndani ya siku chache hizi anaweza kusafiri kwenda New York, Marekani kibiashara, huoni huo ndiyo utakuwa muda muafaka wa sisi kuondoka?” alisema Arianna, kauli ambayo Diego alikubaliana nayo.
Baada ya kumaliza kuzungumza na Diego, Arianna alitoka na kurudi chumbani kwake, akajifungia na kuanza kuvuta madawa ya kulevya kama ilivyokuwa kawaida yake. Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa akielea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa, akauchapa usingizi mzito palepale alipokuwa amekaa.
Alikuja kuzinduka baadaye, alipotazama saa yake tayari ilikuwa ni saa kumi na mbili za jioni, harakaharaka akaficha ushahidi wote wa madawa aliyovuta, akapulizia ‘air freshner’ ili kusafisha hewa ya chumbani humo kisha akaenda kuoga na kuanza kujipodoa kama kawaida yake.
Muda mfupi baadaye Msuya alirejea na kumkuta mkewe amejilaza kitandani, akamkumbatia kimahaba na kumbusu bila kujua kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia.
“Mbona leo umetulia sana? Unaumwa?” Msuya alimuuliza mkewe kwani haikuwa kawaida yake kutulia na kuwa mpole kiasi kile. Swali hilo lilimshtua Arianna, ikabidi azuge kwamba hakuwa akijisikia vizuri.
“Asubuhi ilibidi niende kliniki, alinipeleka kaka Diego,” Arianna alijihami kwa kuongea uongo, Msuya akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye lakini akarudia kumsisitiza kwamba muda wowote anapojisikia vibaya, ni bora apige simu ili mumewe ndiyo ampeleke hospitali.
“Sawa nimekuelewa mume wangu, nakupenda sana mwenzio na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele naona hata mwanao naye anazidi kukupenda,” alisema Arianna huku akilishika tumbo lake, Msuya akapiga magoti kwa furaha na kulibusu tumbo la Arianna.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
0 comments:
Post a Comment