Sunday, 14 February 2016

Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally Aruhusiwa kutoka hospitali....Aitaka Serikali iboreshe hospitali za ndani

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, ameitaka Serikali iweke mikakati thabiti ya kuzipa uwezo hospitali za ndani ili kupunguza gharama kwa Watanzania wengi kwenda kutafuta matibabu nje ya nchi.

Mufti aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki moja akipatiwa matibabu.

Alisema kuna haja ya hospitali kubwa kama Muhimbili kuangaliwa kwa jicho la tatu ili iweze kutoa huduma za kimataifa, hilo litawezekana endapo kutakuwa na vitendea kazi vya kutosha na madaktari kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Mufti alisema kwa kufanya hivyo Watanzania watarudisha imani kwa hospitali za nyumbani na madaktari wake, tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya karibuni ambapo wengi walikuwa wakikimbilia nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta matibabu.

“Binafsi nilikuwa siamini kama naweza kutibiwa hapa nchini, tayari nilishakata tiketi kwa ajili ya kwenda nje ya nchi lakini nashukuru Mungu siku moja kabla ya safari nilihakikishiwa kwamba naweza kupata matibabu hapa.

“Niwasihi Watanzania wenzangu kuamini kwamba Tanzania nayo tuna madaktari bingwa wengi ambao wanafanya kazi nzuri, muhimu kwa Serikali ni kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi,”alisema Sheikh Zubeir 
Kwa upande wake Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ni matarajio ya Serikali kuona viongozi wote wanatibiwa hospitali za nyumbani, jambo litakalowashawishi Watanzania wengine kuamini huduma zinazotolewa.

Alisema kwa viongozi wakubwa kama Mufti kutibiwa nchini kumewasukuma kuongeza vifaa na huduma bora zaidi, ili kuifanya Muhimbili kuwa miongoni mwa taasisi zinazoheshimika.

“Kama Mufti ametibiwa hapa nyumbani kuna sababu gani ya kupeleka watu nje, kwa sasa tumepata hamasa ya kuongeza vitendea kazi na huduma, ili Muhimbili iendelee kuheshimika na ivuke mipaka itoe huduma ndani na nje ya nchi,” alisema Mwalimu 
Akitoa salamu za Bakwata Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Suleiman Said Lolila alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha matibabu ya Mufti.

“Madaktari wamefanya kazi kubwa tuna kila sababu ya kushukuru kwa hilo na Watanzania wote kwa ujumla kwa dua zao hatimaye leo Mufti ameruhusiwa kurudi nyumbani,” alisema Lolila 

 Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimualika Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally kuongea na wanahabari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger