Hukumu
ya kesi ya rushwa ya mkopo uliotolewa na Benki ya Standard ya nchini
Uingereza kwa Serikali ya Tanzania imepingwa na taasisi ya kimataifa
inayopambana na ufisadi, Corruption Watch, ikisema kuwa benki hiyo
ilijisalimisha kuepuka adhabu kali.
Hukumu
hiyo inatokana na kashfa ya ufisadi ambayo benki hiyo ilihusika baada
ya kushinda zabuni ya kuitafutia Tanzania mkopo wa dola 600 milioni za
Marekani (sawa na Sh1.2 trilioni) kwa mauzo ya hatifungani kwa ajili ya
miradi ya maendeleo, lakini ikaliingiza tawi lake la hapa nchini,
Stanbic katika kupata kamisheni, kinyume na taratibu.
Katika
makubaliano hayo haramu, kampuni ya EGMA ililipwa dola 6 milioni (sawa
na Sh1.2 bilioni) kwa maelezo kuwa ilitoa huduma za ushauri.
Taarifa
ya awali iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya
Ufisadi (SFO) ya Uingereza, ilibainisha kuwa EGMA haikutoa ushauri
wowote na kuhusishwa kwake ilikuwa ni njia ya kuwanufaisha viongozi wa
Serikali waliokuwa na mamlaka na taratibu za kukamilisha muamala huo.
Kwa
mujibu wa Corruption Watch, baada ya taarifa hiyo ya SFO, benki hiyo
ilipaswa kushtakiwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukue mkondo
wake, lakini Standard Bank ilitumia Sheria ya Ufisadi nchini humo
kumtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutofanya hivyo na kufanikiwa
kumshawishi.
Kwa
mara ya kwanza katika historia ya Uingereza, Jaji Mwandamizi wa
Mahakama ya Southwark Crown, Brian Leveon aliidhinisha na kutumia Sheria
ya Makubaliano ya Kutoshtakiwa (DPA) kuilipisha faini Benki ya Standard
na hivyo kukwepa kushtakiwa na kukumbana na adhabu za mahakamani.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Uingereza kutumia sheria hiyo kwa moja ya kampuni
zake kubwa, jambo lililosababisha wadau na wanaharakati wanaopinga
ufisadi wa kitaasisi, kuikosoa hukumu hiyo kwa maelezo kuwa
inaikandamiza Tanzania, ambayo ni nchi maskini inayoingizwa kwenye
vitendo vya rushwa kwa mipango kutoka nje ya mipaka yake.
Taasisi
ya Corruption Watch ya nchini humo imesema benki hiyo haistahili kupata
unafuu unaotokana na sheria hiyo ya DPA kwa maelezo kwamba iliratibu
rushwa hiyo na maofisa wake walihusika, hivyo haikustahili kupewa adhabu
ndogo kwa kutumia sheria hiyo.
“Serikali
ya Tanzania haitaridhika na uwajibikaji wa benki hii katika kukabiliana
na uhalifu ilioutenda. Corruption Watch inaona kuwa Tanzania imepunjwa
kiasi inachostahili kulipwa kutokana na ufisadi huu,” inasema taarifa ya Corruption Watch ya mwezi Desemba.
Katika
kuthibitisha udogo wa fidia ambayo benki hiyo imekubali kuilipa
Tanzania, taasisi hiyo imeeleza kuwa malipo halali yangeweza kuzidi mara
kumi ya makadirio ya awali, endapo madhara yote ya udanganyifu
uliofanywa yangezingatiwa.
Inasisitiza
kuwa faini hiyo ilitakiwa ifike dola 80 milioni (zaidi ya Sh160
bilioni) pamoja na riba ya faida ya dola 10 milioni (zaidi ya Sh20
bilioni) kutokana na kilichochumwa na taasisi hiyo ya fedha.
Wakati
hapa nyumbani Serikali ikiwa imetangaza kuwachukulia hatua za kisheria
maofisa wake wote waliohusika kwenye sakata hilo, akiwamo aliyekuwa
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambaye pia likuwa mwenyekiti
wa EMGA, Harry Kitilya, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya
maofisa wa benki hiyo walioratibu upatikanaji wa hatifungani hiyo.
“Hakuna
mtu yeyote aliyechukuliwa hatua za kisheria ama na benki yenyewe au
mahakama kutokana na uzembe wa kushindwa kuzuia vitendo vya rushwa. Watu
hawa wangali wanahudumu katika vyeo vya juu kwenye sekta ya huduma ya
fedha hapa Uingereza. Wanapaswa kuchunguzwa kwa lengo la kuwapunguzia
heshima yao ya kitaaluma,” inasema taarifa hiyo.
Kuhusu
utekelezaji wa sheria uliotumika mpaka Benki ya Standard ikapewa DPA,
taasisi hiyo imelalamikia utegemezi wa uchunguzi uliofanywa na benki
husika juu ya kashfa hiyo.
Imeeleza kuwa upo uwezekano mahakama na umma wakawa hawajaelezwa kinagaubaga uovu uliofanywa na kampuni hiyo.
Kwa
vile uamuzi huu wa DPA ni wa kwanza kutolewa Uingereza na kutakiwa
kutumika kama rejea kwa matukio yatakayofuata, taasisi hiyo imeonya
kuhusu kifungu cha 7 cha Sheria ya Ufisadi kinachotoa adhabu kwa kampuni
au mfanyakazi wake anayeshindwa kudhibiti vitendo vya rushwa dhidi ya
wateja wake.
“Kitendo cha kushindwa kuwachukulia hatua maofisa waliohusika ni kosa kubwa kisheria na kitaaluma,” inasema ripoti hiyo ya Corruption Watch UK.
“DPA
hii inadhihirisha kuwa kifungu cha 7 cha Sheria ya Ufisadi ndicho
kinachotoa adhabu ndogo kwa wavunjaji wake, hivyo kutia wasiwasi kama
kweli Uingereza imedhamiria kukomesha rushwa miongoni mwa kampuni zake.”
==>Hivi ni baadhi ya Vipande vya Ripoti hiyo
0 comments:
Post a Comment