Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani
Na Walter Mguluchuma -Malunde 1 blog - Katavi
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ernest Lyoba (61) Mkazi wa Kijiji cha Namanyere Kata ya Majimoto Wilaya ya Mlele amejeruhiwa vibaya katika sehemu yake ya uso na mgongoni baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akiwa njiani anaelekea nyumbani kwake .
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo la kikatili la kusikitisha limetokea June 25,2023 huko katika eneo la Kijiji cha Namanyere.
Amebainisha kuwa siku ya tukio Ernest alikuwa yuko njiani akiwa anaelekea nyumbani kwake majira ya saa tisa alasiri mara baada ya kuwa amemaliza shughuli zake za kujitafutia riziki ndipo watu wasiojulikana walimmwagia tindikali sehemu za usoni na mgongoni na kumjeruhi vibaya na kisha watu hao walitokomea mahali pasipojulikana.
Kamanda Ngonyani amesema baada ya muathirika wa tukio hilo kumwagiwa tindikali hiyo alipiga kelele za kuomba msaada na baada ya muda mfupi watu walifika kwenye eneo hilo na kumkuta Ernest Lyoba akiwa amejeruhiwa vibaya .
Ameeleza kuwa wasamaria wema hao walimchukua muathirika wa tukio hilo na kumkimbiza kwa haraka hadi kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe kwa ajiri ya matibabu hata hivyo kutokana na kuwa amejeruhiwa vibaya mhanga alipewa rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
Hata hivyo baada ya kuwa amefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi alipewa tena ya kwenda kupatiwa matibabu zaidi kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Mkoani Kilimanjaro ambako amelazwa hadi sasa.
Kamanda Ngonyani amesema juhudi za kuwanasa watuhumiwa hao zinaendelea kufanywa na jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi ili kuhakikisha linawakamata na kuwatia nguvuni na kuwafikisha mara moja Mahakamani ili wakajibu mashitaka ya tuhuma zitakazokuwa zinawakabili .
0 comments:
Post a Comment