Wednesday 3 June 2020

WASIOSHIRIKI MISIBA SASA KUCHARAZWA VIBOKO

...
Diwani wa Kata ya Mwangata, Manispaa ya Iringa, Edward Nguvu


Na Zuhura Zukheir, Iringa
Wakazi wa Kata ya Mwangata, Manispaa ya Iringa wamepongeza uamuzi wa Diwani wa Kata ya Mwangata, Edward Nguvu kutaka watu wasiohudhuria misibani wacharazwe viboko ili iwe fundisho kwa wengine.

Akizungumza na Majira kwa niaba ya wananchi wenzake, mmoja wa wananchi hao amesema hivi sasa kumekuwa na tabia ya waombolezaji kwenye kata hiyo kuchagua misiba, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.

Mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake kutochapishwa gazetini amesema zamani mwitikio wa wananchi kushiriki misibani ulikuwa mkubwa, lakini sasa hivi ni kinyume, ndiyo maana wanaunga ushauri wa diwani wao.

Diwani Nguvu alishauri watu hao wawe wanacharazwa viboko jana alipohudhuria mazishi ya mkazi wa kata hiyo, Wilbart Mgongolwa yaliyofanyika katika makaburi ya Mlolo Mjini hapa.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiendekeza majukumu yao ya kimaisha na kutojihusisha na shida za kijamii kama kushiriki shughuli za misiba na mazishi

Ameongeza kwamba vijana wamekuwa wakikimbilia kwenye misiba ya jamaa zao kwa kwenda kuchimba kaburi, huku misiba mingine wakiachiwa wahusika wenyewe hali inayoelezwa kuleta mpasuko ndani ya jamii.

Ametolea mfano msiba wa Wilbert Mgongolwa, Diwani Nguvu alisema watu wengi hawakuhudhuria katika msiba huo kwa dharau au kutokuwa na msukumo kutoka kwa viongozi wa mtaa.

Amesema kufuatia kuwepo kwa watu wasioshiriki shughuli za misiba wala kutembelea wagonjwa kwa makusudi hivi sasa ipo haja kwa Serikali ya Mtaa kuanza utaratibu wa kuwacharaza viboko wale wote wanaobaki nyumbani bila kuwa na udhuru wowote.

“Sasa hivi imejitokeza tabia ya dharau na watu kutokwenda misibani kwa makusudi, sasa tabia hii inabidi ikomeshwe kwa nguvu zote, nashauri wenyeviti mliopo kwenye kata yangu anzisheni utaratibu wa kuwacharaza bakora wale wote wasiohudhuria msibani ili kesho wao wawe wa kwanza kufika,”amesema Nguvu.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger