Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara (TAKUKURU) Holle Mkungu, amesema wanatarajia kuwafikisha katika Mahakama ya hakimu mkazi Manyara, maafisa wawili wa TRA mkoani hapa kwa makosa ya kudai na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni kumi.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Subilaga Mwangama na Ojungu Mollel, na kwamba makosa hayo ni kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, amesema kuwa Uchunguzi wa Takukuru ulibaini kwamba mlalamikaji (jina linahifadhiwa kwa sababu kwa za kiusalama) ni mlipakodi mzuri kwa mamlaka ya mapato kituo cha wilaya ya Mbulu ambapo kwa kipindi cha mwaka 2018 alilipa kodi zaidi ya million 9.
Hata hivyo mwezi machi 2020 mlalamikaji alipigiwa simu na washtakiwa hao wakimtaka afike ofisi za mamlaka ya mapato mjini Babati, ambapo mlalamikaji alifika na kukutana na Maafisa hao wawili kutoka mamlaka ya mapato Tanzania ambao walimfahamisha kuwa wamefanya ukaguzi wa biashara yake na kugundua kuwa alikadiriwa vibaya na hivyo kumtaka kulipa ongezeko la zaidi ya shillingi millioni tano [Sh.5.812,544,00.]
Makungu ameeleza kuwa mfanyabiashara huyo (mlalamikaji) alikubali ongezeko hilo na alianza kulipa kwa awamu baada ya kuomba na kukubaliwa kulipa kwa awamu na Meneja wa mamlaka ya mapato Wilaya ya mbulu, ambapo uchunguzi wa Takukuru mkoani hapa ulibaini kuwa mlalamikaji akiwa amelipa awamu ya kwanza ya ongezeko hilo na baadae alipigiwa tena simu na washitakiwa na kutakiwa kwenda Babati kwa ajili ya mahojiano kuhusu ulipaji kodi wa mwaka huo wa 2018 ambao ulikuwa tayari wamemkadiria ongezeko.
Aidha mlalamikaji huyo alikuwa na washitakiwa katika ofisi za mamlaka za mapato Babati na akajulishwa kuwa kuna ongezeko tena kwenye kodi ya biashara yake ya kiasi cha shilingi millioni arobaini na tano (45,000,000).
‘’Ongezeko hilo lilimuweka mfanyabiashara huyo kwenye wakati mgumu lakini hata hivyo washitakiwa walimpooza mfanyabiashara huyo kwa maelezo kuwa wanaweza kumpunguzia kutoka million 45 hadi kufikia ongezeko la million 9 endapo angekubali kutoa rushwa’’alisema Makungu .
Hata hivyo uchunguzi wa Takukuru uliendelea kubainisha kuwa mjadala wa kiasi gani cha rushwa atoe ili apunguziwe ongezeko uliendelea kati ya washtakiwa na mfanyabiashara huyo, ambapo dau la shilingi million 20 (20,000,000) waliloanzia lilipungua hadi kufikia million 10 (10,000,000) ambapo mfanyabiashara huyo alielekezwa kuzipeleka kwa mmoja wa mawakala waliopo mjini Babati na ilipofikia hatua hiyo ndipo makachero wa Takukuru walipoandaa mtego uliopelekea watuhumiwa kukamatwa.
Hata hivyo mkuu wa TAKUKURU mkoani hapa Holle Makungu ametoa wito kwa mamlaka ya ya mapato mkoa wa manyara na Tanzania kwa ujumla kwamba kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa ulipaji wa kodi ili kuwa na mfumo unaoeleweka kwa wafanyabiashara wote wa biashara za aina zote ili kudhibiti vitendo vya rushwa na kuondoa mianya inayotumiwa na baadhi ya maafisa wachache wa mamlaka hiyo waliokosa uadilifu kwa kuwabambikia wafanyabiashara kodi zisizolipika kwa nia ya kuwatisha kisha kujipatia rushwa kama walivyofanya watuhumiwa hao.
0 comments:
Post a Comment