Wagonjwa 37 waliokuwa wameambukizwa virusi vya Corona (COVID-19) wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya vipimo vya mwisho kuthibitisha kwamba hawana maambukizi ya COVID-19.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa wagonjwa hao 37 ni kati ya wagonjwa 108 waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona lakini sasa hawana dalili zozote za ugonjwa kama homa, mafua na kikohozi.
Waziri Ummy Mwalimu amewataka watu waliopona ugonjwa huo kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi mapya ya COVID-19 kwani zipo tafiti zilizofanyika nchi mbalimbali ikiwamo China zimeonyesha kuwa watu wanaweza kupata maambukizi mapya kama asilimia 14.
Waziri pia ametoa wito kwa watumishi wa afya kuendelea kutoa huduma za afya kwa watu wote wanaohitaji huduma za matibabu wakiwamo wenye dalili za ugonjwa wa Corona.
“Tumeona kumeanza tabia ambayo ni kinyume na taratibu za afya, hatutakiwi kuwakataa wagonjwa wenye dalili za maambukizi ya virusi vya Corona. Nasisitiza kwamba watumishi wa afya wanakumbushwa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia nwongozo wa Taifa wa kudhibiti maambukizi (National Infection Prevention and Control Guidelines for Health care Services in Tanzania) wa Juni, 2018 pamoja na mwongozo wa Menejimenti ya Matibabu ya Ugonjwa wa COVID-19 wa Januari, 2020 ili kujikinga na maambukizi wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
0 comments:
Post a Comment