Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya TASAF,Dr.Moses Kusiluka(mwenye miwani ) akikagua baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa TASAF katika shehia ya Kianga, kisiwani Unguja kama mojawapo ya njia ya kujiongezea kipato.
Mwenyekiti wa Kamati Uongozi wa Taifa ya TASAF ( aliyevaa miwani) akikagua bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa TASAF katika shehia ya Kianga,Unguja kama njia mojawapo ya kujiongeza kipato .Anayefuatia ni Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais-ZMZ- Mhe. Mihayo Juma Nunga.
Wajumbe wa kamati ya uongozi ya taifa ya TASAF wakipata
maelezo ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kisiwani Unguja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya TASAF Dr. Moses Kusiluka (aliyesimama ) akiwahutubia Wananchi wa Shehia ya Kianga kisiwani Unguja (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua miradi ya TASAF
kisiwani humo.
Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi ya taifa ya TASAF Dr.Moses Kusiluka (alivaa koti) akiongoza wajumbe
wa kamati hiyo kukagua ujenzi wa jengo la kituo cha Afya Kianga ,Unguja linalojengwa na TASAF kwa kushirikiana na wananchi, Katikati ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo Dr.Gwajima ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI
anayeshughulikia sekta ya Afya,kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga.
Sehemu ya Walengwa wa TASAF na wananchi wa shehia ya
Kianga,Unguja wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Taifa ya TASAFambaye pia ndiye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-IKULU Dr. Moses Kusiluka (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua miradi ya TASAF kisiwani humo.
**
Na Estom Sanga-ZANZIBAR
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- Dr. Moses Kusiluka amewataka Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF kutumia fursa hiyo kwa ukamilifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya serikali ya kupambana na umaskini nchini.
Dr. Kusiluka ambaye pia ndiye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-IKULU -ameyasema hayo katika shehia ya Kianga wilaya ya Magharibi ‘’A’’ Mkoa wa Mjini –Magharibi,Kisiwani Unguja ambako ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- kujionea utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo Kisiwani humo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi kubwa za kuweka mazingira mazuri kwa Wananchi kujiletea maendeleo na kuboresha maisha yao hivyo akawataka kutumia vizuri fursa hiyo kwa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa bidi ili kukuza uchumi wao na hatimaye kuchangia katika pato la taifa na kuondoa kero ya umaskini miongoni mwao kwa vitendo.
Dr. Kusiluka pia amewataka Walengwa wa TASAF kutobweteka na mafanikio waliyoanza kuyapata kutokana na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TASAF badala yake waendelee kuuchukia umaskini kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidi ili hatimaye waweze kuboresha maisha yao huku akisisitiza ustawi wa jamii kwa ujumla hususani watoto kama ilivyo dhamira ya Serikali.
Katika hatua nyingine Dr. Kusiluka ameuagiza Uongozi na Watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia Uzalendo kwani amesema Mfuko huo unagusa nyanja muhimu za Maendeleo ya Wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya,maji,uchumi,kilimo,mifugo na hifadhi ya mazingira na hivyo kuwa miongoni mwa sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi moja kwa moja.
“Serikali inathamini mchango wa taasisi hii katika jitihada zake za kupunguza umaskini nchini, endeleeni kufanya kazi kwa bidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa haraka na ufanisi mkubwa” amesisitiza Dr. Kusiluka.
Kwa upande wake, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Mihayo Juma Nunga akizungumza na Wananchi baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Shehia ya Kianga inayojengwa na TASAF kwa kushirikiana na Wananchi wa eneo hilo, amesema ujenzi huo ni miongoni mwa vielelezo vya namna serikali zote mbili,yaani ile ya Muungano na ile ya Mapinduzi zinavyowajali wananchi kwa kuondoa kero zao kwa vitendo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,TASAF-Bw.Ladislaus Mwamanga amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo yaliyochangiwa kwa kiwango kikubwa na Serikali,Wadau wa Maendeleo na Wananchi hususani Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao amesema kwa sehemu kubwa wameanza kuboresha maisha yao na kuonyesha namna wanavyouchukia umaskini kwa vitendo.
0 comments:
Post a Comment