Tuesday, 4 June 2019

Taarifa Kwa Umma Toka Jeshi La Polisi Makao Makuu

...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi wanavyoendelea kutoa ushirikiano  kwa kutoa taarifa na ufadhili unaowezesha kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu nchini kwani uhalifu unaendelea kupungua na kuifanya nchi yetu  kuendelea kuwa shwari na salama.

Yapo  matukio mchache ambayo tunaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wananchi wote katika kupeana elimu ya kuyaepuka kuyatenda matukio kama vile mauaji yanayotokana  na vitendo vya wananchi kujikulia sheria mikononi, wivu wa mapenzi na  ulevi.   Pia matukio ya ubakaji na ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva. 

Jeshi la Polisi Tanzania lina amini kama kila mtu  kwa nafasi yake akishiriki katika kutoa elimu, kuonya na kufiwachua wanaotenda uhalifu huo, kuanzia ngazi ya familia matukio ya aina hiyo yatapungua kwa kiasi kikubwa.

Mtakumbuka pia tarehe 01/06/2019 serikali ilitoa maelekezo kuwa,  ndiyo mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini na utekelezaji ukaanza kwa ufanisi mkubwa.  Jeshi la Polisi linatoa wito agizo hilo liendelee kuzingatiwa na wenye mifuko ya aina hiyo waisalimishe kama ilivyoelekezwa na kama kuna mwenye taarifa za mtu mwenye kumiliki mifuko hiyo atoe taarifa Polisi au mamlaka zingine ili hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni ziweze kuchukuliwa.

Aidha,  kama mnavyofahamu tunaelekea kipindi cha sikukuu ya Eid El Fitri ambayo husheherekewa  duniani kote baada ya mfungo wa  Mwezi  Mtukufu wa Ramadhani.  Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watanzania wote kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama ili waweze kusheherekea kwa amani na utulivu sikukuu hiyo kubwa na muhimu.

Kila  mmoja ajiepushe na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha  usalama wa maisha na mali zao kama vile kuacha nyumba bila waangalizi, ulevi wa kupindukia, kuruhusu vijana na watoto walio chini ya uangalizi wa wazazi kwenda katika nyumba za starehe au maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama na utu wao. Kujiepusha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama  barabarani kama vile kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa , mwendo kasi, pamoja na kujaza abiria kupita kiasi.

Pamoja na kwamba,  Jeshi la Polisi katika Mikoa yote  limejipanga kikamilifu kuimarisha  ulinzi  katika maeneo yote ya ibada na  maeneo mengine ambayo yatakayokuwa na mikusanyiko  mikubwa  ya watu tunaelekeza kila mmoja  usalama uanzie kwake  na kwa wale wanaomiliki maeneo ya starehe wazingatie maelekezo ya kiusalama waliopewa na
Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi  na watakayoendelea kuwapa.  Pia tunatoa onyo kwa wale wanaodhani wanaweza kutumia sherehe hizi kufanya uhalifu watambue kuwa watashughulikiwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za nchi.

Tunawaomba  wananchi wote pale watakapoona viashiria au kumtilia mtu mashaka kuwa huenda akawa  mhalifu watoe  taarifa kupitia  namba  za simu za bure  0787 668 306 au 111 au 112.
                   
Tunawatakia  Watanzania wote Sikukuu njema yenye amani na utulivu  ya Eid El  Fitri.
Imetolewa na:

……………………………..
DAVID A. MISIME - SACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger