Na. Erick Mwanakulya, Kagera.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unaendelea kutetekeleza miradi ya Ahadi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kukamilisha ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Km 2.76 kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Mhandisi Dativa Telesphory alifafanua kuwa utekelezaji wa miradi ya Ahadi za Mhe. Rais umekamilika kwa asilimia 100 baada ya ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami kukamilika na kuanza kutumika.
“Kabla ya TARURA kuanzishwa, Wilaya ya Muleba haikuwa na lami hata Mita 1 lakini hadi sasa kupitia kuanzishwa kwa Wakala na pia utekelezaji wa miradi ya Ahadi za Mhe. Rais tumetekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Km 2.76 ambazo zimekamilika na wananchi wameanza kunufaika na ujenzi wa barabara hizi”, alisema Mhandisi Dativa.
Mkazi wa Muleba Bi. Edvina Jackson ameishukuru Serikali kwa kutengeneza barabara za lami kwenye eneo lao ambalo lilikuwa limesahaulika kwa muda mrefu kwani kwa kiasi kikubwa ujenzi wa barabara hizo umesaidia kupunguza kero ya usafiri na kufanya barabara hizo kupitika muda wote.
‘‘Tunashukuru sana Serikali barabara ni nzuri na pia usimamizi ni mzuri, pale mwanzoni tulikuwa tunapata shida kwenda mashambani na hata masokoni, sasahivi barabara ni nzuri hakuna vumbi wala matope katika kipindi cha mvua na kiangazi”, Bi. Edvina.
Aidha, mbali na utekelezaji wa miradi ya Ahadi za Mhe. Rais, TARURA wilaya ya Muleba imetekeleza ujenzi wa Daraja la Kishara lenye urefu wa Mita 36 katika Mto Ngono linalounganisha Kata za Katoke, Kamachumu na Kata ya Mafumbo ambapo kwa mujibu wa meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, amesema wananchi walikua wanazunguka umbali mrefu lakini sasa kero hiyo imeisha.
Naye, Mkazi wa Kitongoji cha Kyamuhaya Bi. Goodselda Liberius alisema kuwa upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo hilo umerahisishwa na uwepo wa daraja hilo kwasababu umewasadia kuvusha mazao yao na bidhaa nyingine za biashara kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Tunashukuru kwa kujengewa daraja hili kwasababu limekuwa ni mkombozi kwa sisi wafanyabiashara kusafirisha mazao yetu na tunaishukuru Serikali kwa kutujengea daraja hili,” alisema Goodselda.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijni (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba unaendelea na kazi mbalimbali zikiwemo za matengenezo ya barabara na vivuko katika Wilaya hiyo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.
0 comments:
Post a Comment