Friday 1 May 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA AMIRI JESHI MKUU, MHESHIMIWA DAKTARI JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE UZINDUZI WA MELI VITA ULIOFANYIKA MAKAO MAKUU YA KAMANDI YA NAVY TAREHE 28 APRIL, 2015

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Dkt. Jakaya M Kikwete

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb);

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Mecky Sadick;
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Lu Youging;
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue;
Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT, Job Masima;
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange;
Makatibu Wakuu wa Serikali Mliopo;
Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Luteni Jenerali Samwel Ndomba;
Viongozi mbalimbali wa Serikali mliopo;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Wakuu wa Kamandi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania;
Majenerali mliopo;
Wawakilishi kutoka Jeshi la Ukombozi la Jamhuri ya Watu wa China;
Maafisa na Wapiganaji;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Shurani na Pongezi
Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi;
Nakushukuru Waziri na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa kunialika kwenye hafla hii muhimu ya uzinduzi wa Meli Vita za Jeshi la Wanamaji la JWTZ. Natoa pongezi nyingi kwa CDF, Kamanda wa Navy na wanajeshi wote kwa hatua nyingine muhimu tunayopiga katika kuimarisha uwezo wa Jeshi letu kutekeleza majukumu yake kwa upande wa mpaka wetu wa majini. Kwa niaba yenu napenda kuwashukuru ndugu zetu na marafiki zetu wa Jamhuri ya Watu wa China kwa kutupa meli hizi ambazo tunazizindua leo. Ni ukweli usiofichika kuwa hatuna mshirika mkubwa kwa maendeleo ya Jeshi letu kushinda Wachina.  Wamekuwa nasi tangu JWTZ lilipoanza miaka 51 iliyopita. Kwa kweli, hatuna maneno mazuri ya kuwashukuru zaidi ya kusema asanteni sana.  Natoa shukrani maalum kwa kampuni ya Poly Technologies Inc. kwa ushirikiano wenu.  Ni moja ya kampuni muhimu inayotupatia silaha na zana za kijeshi.
Tukio Linatuunganisha na Wananchi wa China
Maafisa na Wapiganaji;
Mabibi na Mabwana;
Kupatikana kwa MELI VITA MWITONGO na MELI VITA MSOGA kunaandika histori mpya katika kuliwezesha Jeshi letu la Wanamaji katika utendaji wake.  Kama mnavyojua,  Jeshi letu la Wanamaji lilianzishwa rasmi mwaka 1971 kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Serikali ya China ilitoa idadi ya meli 13 na kutujengea vituo vitatu vya Rada kwa ajili ya uchunguzi wa Pwani; na kutujengea karakana na chelezo (slipway).
Pia marafiki zetu wa China wametupa wataalam mbalimbali kwa ajili ya karakana na chelezo, wametupa nafasi nyingi za mafunzo nchini kwao kwa ajili ya maofisa na askari wetu; na wametuanzishia Kombania mbili za Marine Special Forces. Hii ni pamoja na kugharamia mafunzo na vifaa vyake.
Ndugu zetu hawa wanaendelea kutupatia waalimu na wakufunzi kwa ajili ya shule yetu ya Ubaharia. Kwa ujumla, kwa mrefu Kamandi ya Navy ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania imekuwa ikipata misaada mbalimbali kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China.
Usione vinaelea vimeundwa.  Haya yote ni ya udugu na urafiki baina ya nchi zetu ulioasisiwa na viongozi waasisi na mataifa yetu mawili: yaani Chairman Mao Tse Tung wa China na Julius Nyerere. Pia ni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na viongozi waliofuatia. Naahidi kuwa sisi Tanzania tutaenzi na kudumisha uhusiano huu wenye tija kubwa kwa nchi zetu mbili.
Meli Zimekuja muda Muafaka
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana;
Kwa mujibu wa maelezo niliyopewa, meli hizi - MELI VITA MWITONGO na MELI VITA MSOGA - zinaweza kwenda kwa kasi, zikiwa na  silaha za ulinzi kwa kiwango cha kuweza kutoa ulinzi wa kutosha.  Pia zinaweza kukaa baharini kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa umbali mrefu. Uwezo mkubwa wa meli hizi kulinda maji yetu na EEZ ni hazina kwetu na faraja kubwa kwa Taifa letu. Tuendelee  kuwa na ushirikiano na Serikali na Jeshi la Jamhuri ya Watu wa China ili tuzidi kuvuna zaidi kutokana na uzoefu wao.
Upatikanaji wa Meli Vita hizi umekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu inahitaji ulinzi wa bahari wa kutosha kwa kushirikiana na majirani zetu wa Kenya, Msumbiji na mataifa mengine katika kupambana na uharamia wa baharini. Kutokana na meli hizi, eneo letu la bahari sasa litakuwa salama kwani tunaweza kulilinda kwa uhakika. Zitasaidia kuchagiza maendeleo ya kiuchumi kwa taifa letu kupitia ulinzi wa rasilimali za baharini. Kama mjuavyo, tuna samaki wengi baharini wanaoibiwa bila sisi kujua. Tuna gesi asilia ambayo ni tumaini kubwa kuitoa nchi yetu hapa tulipo na kuipeleka mbele kwenye maendeleo. Lazima rasilimali hiyo tuilinde. Namna pekee ya kuweza kuhakikisha usalama wa mipaka yetu na rasilimali za bahari ni kuwa na vifaa vya kutosha na vya kisasa, kama meli vita hizi tunazozizindua leo.  Aidha, ari ya utendaji kazi kwa maafisa na askari wa Kamandi ya Navy pia itazidi kuongezeka.
Meli Zitumiwe kwa Ufanisi
Kamanda wa Navy;
Hongereni kupata zana na silaha mpya katika Kamandi yenu. Bila ya shaka itawaongezea ari ya utendaji kazi wa maafisa na askari. Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii pia, kuwasihi mzitumie vizuri meli hizi, na hasa hasa mzitunze ili ziweze kutimiza majukumu yaliyokusidiwa na kwa ufanisi mkubwa. Kufanya hivyo ni kwa manufaa ya Jeshi lenyewe na kwa  manufaa ya Taifa kwa ujumla, katika utendaji wenu wa shughuli za ulinzi katika maeneo yetu ya Bahari ya Hindi.  Aidha, tutunze kwa umakini mkubwa vifaa na zana mbalimbali kama hizi zinazowawezesha kutekeleza majukumu yenu.
Kila fursa ya kiuchumi inapojitokeza, Serikali  itaendeleza juhudi zake za kiliimarisha jeshi letu kwa kulipatia vifaa vya kisasa na kuwawezesha maafisa wake kuwa na uwezo mkubwa wa kulinda mipaka yetu. Pia tutazidi kuimarisha upatikanaji wa huduma nyingine muhimu za msingi ikiwa ni pamoja na malazi bora na mavazi nadhifu.
Hitimisho
Waheshimiwa Viongozi ;
 Mabibi na Mabwana ;
Mwisho, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na JKT, Mkuu wa Majeshi na wale wote kwa namna mbalimbali  walivyotoa michango yao kufanikisha kupatikana meli hizi. Nichukue nafasi hii pia, kuwashukuru na kuwapongeza  Maafisa na Askari wa Kamandi ya Navy kwa kazi nzuri wanayoifanya katika majukumu yao ya kulinda nchi yetu na hasa zinazohusiana na operesheni mbalimbali za baharini.
Aidha, nawapongeza pia wote walioshiriki katika maandalizi ya shughuli hii ya leo.  Wamefanya kazi kubwa inayostahili pongezi za dhati. Tuendelee kushirikiana katika majukumu kama haya ili kuliwezesha Taifa letu kusonga mbele katika maendeleo ambayo yanategemea sana ulinzi imara.
Asanteni sana!

BONYEZA HAPO CHINI KUANGALIA MAJINA YA AJIRA Z WALIMU 2015 NA SELECTION KIDATO CHA TANO 2015
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger