Na. Mwandishi wetu
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mwanza na Shinyanga utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 21 hadi 27 Agosti, 2024 ambapo jumla ya wapiga kura wapya 400,082 wanatarajiwa kuandikishwa.
Hayo yamesemwa leo tarehe 09 Agosti, 2024 kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa Uchaguzi iliyofanyika mkoani Mwanza na Shinyanga.
Mkoani Mwanza mkutano wa wadau umefunguliwa na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele na mkoani Shinyanga mkutano umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk.
Viongozi hao wa Tume wamewataka wadau hao wa uchaguzi kuhamasisha wananchi na wapiga kura kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi lifanyike kwa ufanisi.
Katika mikutano hiyo mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima Ramadhani imebainisha kuwa mkoani Shinyanga wapiga kura wapya 209,951 wataandikishwa na mkoani Mwanza wapiga kura wapya 190,131 wataandikishwa na kufanya jumla ya wanaotarajiwa kuandikishwa kuwa 400,082.
“Kwa mkoa wa Mwanza Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 190,131. Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ya wapiga kura 1,845,816 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Hivyo, Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Mwanza utakuwa na wapiga kura 2,035,947,” amesema Bw. Kailima.
“Kwa mkoa wa Shinyanga Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 209,951. Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ya wapiga kura 995,918 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Hivyo, Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Shinyanga utakuwa na wapiga kura 1,205,869,” amesema Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Seleman Mtibora ambaye amewasilisha mada kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi mkoani Shinyanga.
Bw. Kailima amefafanua kuwa idadi hiyo inatokana na makisio yaliyofanywa kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kwamba inaweza kuongezeka.
Uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 ambapo ulienda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi na kufuatiwa na mzunguko wa pili umejumuisha mikoa ya Geita na Kagera.
Kwa sasa, uboreshaji wa Daftari unaendelea kwenye mikoa hiyo ya Kagera na Geita hadi tarehe 11 Agosti, 2024 ambapo vituo vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
0 comments:
Post a Comment