Na Dotto Kwilasa,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DK. Samia Suluhu Hassan amekutana na Maafisa Ugani pamoja na Wanaushirika ambapo katika mkutano huo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za ugani ili kuboresha uzalishaji wa kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.
Rais Samia amewataka maafisa hao kuhakikisha kuwa wanawasaidia wakulima kwa mbinu bora na teknolojia za kisasa ili kufanikisha malengo ya kuongeza chakula na kipato kwa wananchi.
Hayo yamejiri Agosti 10,2024 Ikulu Chamwino,Dodoma ambapo ametumia nafasi hiyo kuvielekeza vyama vya ushirika kuwa chachu ya mabadiliko na vyenye kuleta mageuzi ya fikra ikiwemo kuchangia maendeleo mapana kwa kuhamasisha wanaushirika waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa na uhakika wa matibabu.
Dk.Samia pia ameitaka Wizara ya Kilimo kuandaa utaratibu wa kuwapima Maafisa ugani kwa tija inayozalishwa kwenye Kata au Kijiji nachokisimamia ili 4uwekezaji unaofanywa na serikali kupata matokeo tarajiwa .
Aidha amewataka Maafisa ugani katika ngazi ya Kata kukaa kwenye vituo vyao na kutumia usafiri ambao serikali imewapatia kuwafikia na kuwahudumia wananchi.
"Sisi kama Serikali tutaendelea kuunga mkono juhudi za wanaushirika kwa kuanzisha Benki ya Ushirika ya Taifa kwa kuchangia shilingi bilioni tano kama mtaji ili kuwezesha shughuli za Benki hiyo kuanza, " amesema Rais Samia
Pamoja na hayo amevitaka Vyama vya Ushirika kutokuwa sehemu ya kumnyonya mwanaushirika bali viwe mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea wakulima huku akisisitiza kuwa Serikali inadhamira ya kurudisha hadhi ya ushirika wa mazao hivyo kutaka ushirika uendeshwe kisasa.
0 comments:
Post a Comment