Na Hadija Bagasha Tanga,
Aliyekuwa Waziri wa afya ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa heshima kubwa ya kuwa Waziri wake kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu akiitumikia nafasi ya waziri ofisi ya Rais Tamisemi na baadaye wizara ya afya huku akisema ameyapokea mabadiliko hayo kwa moyo mkunjufu na kwa moyo wa shukrani.
Ummy ametoa shukrani hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa ndani katika ziara ya Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah ambaye ni mlezi wa kichama katika Mkoa wa Tanga.
Ummy amesema kuwa ameyapokea mabadiliko yaliyotokea kwa moyo mkunjufu na kwa moyo wa shukrani kwani Rais Samia ameonyesha Imani yake kwake Kwa kiwango kikubwa huku akiahidi sasa kuwatumikia wanatanga ipasavyo.
"Nimeyapokea mabadiliko haya kwa moyo mkunjufu lakini kwa moyo wa shukrani namshukuru Mwenyezi Mungu kwa yaliyotokea kubwa nikuahidi mheshimiwa Makamu wa Rais nitaendelea kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mwenyekiti wangu wa chama na chama kwaujumla lakini pia nikuahidi kwamba sasa nitafanya kazi kwa karibu sana na wananchi wangu ambao ndio walionipa heshima ya kuweka rekodi ya kuwa mbunge wa kwanza mwanamke katika jimbo la Tanga,"alisisitiza Ummy.
Aidha Ummy amesema kwamba kazi kubwa sasa iliyopo mbele yao ni kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi katika jimbo la Tanga kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa ccm Wilaya Tanga Meja Hamis Mkoba.
"Tunasimama kifua mbele watu wa Tanga kwa jinsi Rais Samia alivyorubeba ksa kuboresha bandari ya Tanga hili jambo nililisema kwa sauti kubwa na kwa nguvu kubwa wakati naomba kura tunamshukuru Rais kazi hii aliianza Rais Magufuli na sasa Rais Samia anaendeleza Bilioni 429 zimewekwa katika bandari ya Tanga, bandari ya Tanga imeboreshwa niliwaambia watu wa Tanga kwamba nataka Tanga iwe kama Singapore maana yake mameli makubwa yatie nanga katika bandari ya Tanga ndugu zangu wanatanga na sasa meli kubwa tunashuhudia zikitia nanga hapa, "alisema Ummy.
"Mheshimiwa Makamu wa Rais kwetu sisi hili moja tu tuna deni kubwa kwa Rais Samia kwani hatumdai lakini yeye anatudai ushindi wa kishindo kwa sababu mameli makubwa sasa yanatia nanga katika bandari yetu ya Tanga juzi imekuja meli ya magari 500 yamechochea ajira nimepokea vijana wa Tanga 200 na siku nyingine tutakuletea madereva wa kuendesha gari za IST wanasema kwanini wanaoendesha watoke Daresalaam wameanzisha umoja tunawafungulia ofisi ili sasa madereva wa IST watoke jiji la Tanga, "alisema Ummy.
"Nikuhakikishie Makamu wa, Rais tutakwenda nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka, kitanda kwa kitanda, kata kwa kata kutafuta ushindi wa chama cha mapinduzi katika mitaa yote 181 ya jiji la Tanga na kata zote 27,"alisema Ummy.
Aidha amewashukuru wanatanga Kwa kumuwezesha kutimiza historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kugombea Jimbo la Tanga na kushinda.
0 comments:
Post a Comment