Saturday 29 June 2024

WILAYA YA CHEMBA YAPATA BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA TANGU KUANZISHWA KWAKE

...

Wananchi wa Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma  wanakwenda kutatuliwa Kero yao ya Muda mrefu ya kukosekana kwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ambalo hutumika kutatua Migogoro mbalimbali ya Ardhi inayojitokeza.

Hayo yamebainishwa leo Juni 28, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary  Senyamule wakati akiwaapisha wajumbe Wanne wa Baraza hilo, hafla ambayo imefanyika katika ukumbi wa Ofisi yake Jengo la Mkapa Jijini Dodoma.

“Tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Chemba 2012, wananchi wake wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda katika Baraza la wilaya ya Kondoa kutafuta haki zao. Sasa wamepata baraza lao na kufanya Dodoma kuwa na jumla ya Mabaraza 6 hivyo, kero ya wananchi wa Chemba kutokua na Baraza la Ardhi na Nyumba inakwenda kutatuliwa” amesema Mhe. Senyamule

Mbali na hilo, Mkuu wa Mkoa amemtaka Katibu Tawala Mkoa pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Mkoa, kusimamia mchakato wa kuhakikisha Wilaya ya Chamwino nayo inapata baraza la Ardhi na Nyumba hivyo kukamilisha Mabaraza yote saba katika Mkoa wa Dodoma kwani ndiyo pekee imesalia bila kuwa na Baraza hilo.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Gerald Mongella, ameishukuru Serikali kwa kuifanyia kazi kero hiyo.

 “Tumekua tukipambana na Migogoro mingi ya Ardhi hivyo baraza hili litatusaidia kupunguza kero hizo, Kupitia Baraza hili, haki itapatikana na amani itatamalaki kama ilivyo matamanio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani  kumaliza migogoro yote ya Ardhi Nchini”.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Dodoma Bw. Omary Mbega, amesema kuwa jukumu kubwa la wajumbe hao ni kusaidia haki itendeke na kuwasihi kufuata maadili, kanuni na taratibu zinazoliongoza Baraza kwani ukiukwaji wake unaweza kupelekea kutenguliwa kwenye nafasi hiyo inayodumu kwa kipindi cha miaka mitatu tu.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger