Monday 10 June 2024

BEI ZA VOCHA ZA SIMU ZAPANDISHWA MIKOA 9 TANZANIA

...

Mikoa tisa imewasilisha malalamiko ya kupandishwa kiholela kwa bei za vocha za simu za mkononi.

Taarifa ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC), Mary Msuya iliyotolewa leo imesema hivi karibuni bei za vocha za mkononi zimepandishwa kinyemela ambapo vocha ya sh 500 inauzwa kati ya sh 550 hadi 600, vivyo hivyo vocha ya sh 1,000 kuuzwa kati ya sh 1,100, hadi 1,200 kinyume cha bei elekezi.

Ametajwa mikoa inayolalamika kuwa ni Dar es Salaam, Rukwa, Iringa, Ruvuma, Manyara, Lindi, Mbeya, Mtwara na Songwe.

Mary amesema katika kushughulikia changamoto hiyo, Baraza limeshauriana na watoa huduma za mawasiliano ya simu kufuatilia mawakala wao na kupiga marufuku upandishaji holela wa bei za vocha.

"Baraza limeshauri watoa huduma za mawasiliano ya simu kutoa taarifa kwa watumiaji kwa kuwataka kutonunua vocha kwa bei tofauti na inayoonekana kwenye vocha husika na utaratibu wa kutoa malalamiko wanapokutana na kadhia hiyo," amesema.

Ameshauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kununua vocha kwa kupitia simu zao za mkononi wakati changamoto hiyo ikitafutiwa ufumbuzi na kuendelea kutoa taarifa za kupanda bei kiholela katika maeneo mbalimbali ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na hali hiyo kukomeshwa.

Mary amesema, baraza linaendelea kufuatilia hali hiyo na kushauri hatua za kuchukua ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapata haki ya kupata huduma kwa bei halali na yenye ubora.

Imeandaliwa na Vicky Kimaro
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger