Sunday 9 June 2024

TANROADS, ZANROADS WAWEKA MPANGO KAZI WA MWAKA 2024/2025

...



Na Carlos Claudio, Dodoma.

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS) wameweka mpangokazi wa kipindi cha mwaka mmoja, ambao utekelezaji wake utaanza kutumika rasmi mwaka wa fedha 2024/25.


Akizungumza na wakala wa barabara Zanzibar, wenyeviti wa bodi za ushauri, wawakilishi wa bodi ya ujenzi pamoja na kamati ya wataalam jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mha. Mohamed Besta amezungumza katika kikao hiko cha uwasilishaji wa mpango kazi wa utekelezaji wa Hati ya mashirikiano kati ya TANROADS na ZANROADS uliofanywa na Kamati ya Wataalam amesema mpango kazi huo utaanza kufanya kazi rasmi baada ya kusainiwa na uongozi wa juu wa pande zote mbili.

Mha. Besta amesema kuwa mpango kazi huo ni wa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2024/25 hadi 2028/29 ambapo utakuwa unahuishwa kila mwaka, lakini kwa mwaka ujao wa fedha wataanza na vipengele vinne vya kuanzia kazi, ambavyo vimeainishwa kwenye rasimu hiyo, ambavyo ni kuandaa na kuendesha mafunzo, semina na warsha kwa ajili ya kujenga uelewa juu ya miongozo mbalimbali ya uendeshaji na usimamizi katika shughuli za ujenzi wa barabara.

Amesema vipengele vingine ni pamoja na kuandaa na kuendesha vikao kazi vya kuandaa miongozo na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa mizani, pia kuandaa mafunzo ya namna ya uendeshaji na utunzaji wa mizani kwa watumishi wa ZANROADS; na kutoa elimu kwa wadau wa usafirishaji kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa shughuli za mizani na umuhimu wake.

Mha. Besta amesema vipengele vingine ambavyo vitatekelezwa kwa kuanzia robo ya kwanza hadi ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25 ni pamoja na kuandaa nyaraka za uanzishwaji wa kitengo cha Ushauri elekezi Zanzibar (ZANROADS Engineering Consulting Unit - ZECU) kuandaa na kuifanya ziara za mafunzo na kubadilishana uzoefu; Ufuatiliaji wa maendeleo ya uanzishwaji wa kitengo cha ZECU na kuratibu shughuli za kijamii ikiwemo mashindano na michezo mbalimbali kati ya taasisi hizo.

“Tunaamini utekelezaji wa mpango kazi huu kutasaidia kuimarisha uwezo wa utendaji wa taasisi zetu hizi, sisi tuna la kujifunza kwa wenzetu na wao wanalo la kujifunza kutoka kwetu,” amesema Mha. Besta.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ZANROADS, Mha. Cosmas Masolwa amesema kutokana na mashirikiano hayo yataendelea kuleta na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili.

Mha. Masolwa amesema,“ Ushirikiano huu naamini utadumu na pande zote mbili kila mmoja atanufaika kutokana na jambo jipya kutoka kwa mwenzake, ukiangalia wenzetu wapo mbele mfano sisi hatuna mzani wa magari huku kwetu Zanzibar na sasa mahoteli makubwa makubwa yanajengwa na magari mengi yanayoleta malighafi ya ujenzi yanakuja na mawe, mchanga hivyo ni rahisi kuharibu barabara zetu, hivyo tunaamini tutajifunza kutoka kwa wenzetu.”

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ZANROADS, Msanifu Majengo Yasser de Costa amepongeza mashirikiano hayo yaliyochagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na anaamini yatafanikiwa kunilingana na utekelezaji wa vipengele vilivyopo kila mwaka.


Sambamba na hayo TANROADS na ZANROADS wameandaa ziara ambapo Juni 10, 2024 watatembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger