Friday 28 June 2024

TAMWA ZNZ, IDARA YA MICHEZO WEMA, ZAFELA, GIZ NA CYD KUANDAA MTOTO WA AFRIKA MARATHON

...
 
Ni katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Zanzibar

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Mashirikiano ya Ujerumani (GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), inatarajia kuadhimisha ya siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika tarehe 29 Juni 2024 kwa kuandaa mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali za Zanzibar.


Maadhimisho hayo yatawahusisha jumla ya washiriki 150 ambapo kati ya hao watakaoshiriki mashindano ni wanafunzi 75 kutoka katika skuli za Unguja ambazo zimeshajiandaa kushiriki mashindano hayo.


Tukio hili muhimu ambalo linalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo litawaleta pamoja wadau kutoka taasisi za kierikali na zisizokuwa za kiserikali ikiwemo wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja, wanamichezo, walimu wa michezo, na wadau wote wa masuala ya usawa wa kijinsia.


Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wasichana kuonesha vipaji vyao na uwezo wao wa kushiriki katika michezo mbalimbali, pamoja na kujadili changamoto na vikwazo vinavyowazuia kushiriki katika michezo na kuhimiza uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika taasisi za michezo.


Mashindano haya ya riadha yataanza saa 12 na nusu asubuhi, yakianzia maeneo ya Forodhani na yataishia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar yakishirikisha wanafunzi wa jinsia zote  kutoka skuli mbalimbali za Unguja.


Kaulimbiu ya wadau katika maadhimisho ya mwaka huu ni Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote”. Tukio hili linatarajiwa kuleta mwamko na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa nafasi sawa watoto wote kushiriki katika michezo, bila kujali jinsia zao. Mashindano hayo yatatoa washindi watatu zaidi wanawake na watatu wanaume na kutambuliwa rasmi.  


Tunaamini kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kujifunza stadi za maisha, kujenga ujasiri, na kushirikiana kwa amani na kuheshimiana.


Tunawaalika wanahabari, wazazi, walezi, na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuunga mkono tukio hili la kihistoria katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wote kufikia ndoto zao katika Nyanja mbali mbali bila vizuizi vyovyote.


Imetolewa na Idara ya mawasiliano,

TAMWA ZNZ.

info@tamwaznz.or.tz 

www.tamwaznz.or.tz 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger