Friday 28 June 2024

TBS KANDA YA KUSINI YATEKETA TANI 3.5 ZA BIDHAA HAFIFU

...

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kusini inayojumulisha Mikoa ya Lindi Mtwara na Ruvuma limetekeleza tani 3.5 za bidhaa hafifu zenye thamani ya sh. 20,054,000 ambazo zilikamatwa kwenye mikoa ya kanda hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuteketeza bidhaa hizo eneo la dampo la Manispaa ya Mtwara Mikindani, Kaimu Meneja wa Kanda ya Kusini, Bw.William Mhina alisema zilikamatwa kwenye ukaguzi uliofanywa na TBS ili kuhakikisha bidhaa hafifu zinaondolewa sokoni kwa lengo la kulinda usalama wa watumiaji wa bidhaa hizo.

Alisema bidhaa hizo zilikamatwa katika ukaguzi uliofanyika Januari 2024 hadi Juni, mwaka huu. Alitaja bidhaa zilizoteketezwa kuwa ni nguo za ndani za mitumba ambazo ni sidiria pamoja na chupi.

Aidha, alitaja nyingine kuwa ni vipodozi vilivyokatazwa kisheria kuingia nchini na kuuzwa kwenye soko laTanzania na za chakula ambazo zimeisha muda wake wa matumizi. "Bidhaa zote hizi zimekuwa zikikamatwa na wakaguzi wetu, wakati wa ukaguzi uliofanyika kwenye kanda yetu," alisema.

Alitaja sababu ya kuteketezwa kwa vipodozi hivyo, Bw. Mhina alisema ni kutokana na kuwa na viambata sumu.

Alisema vipodozi hivyo vimepigwa marufuku nchini kwa sababu husababisha kuathirika kwa mifumo ya uzazi kwa wanawake na wanaume, kuharibika kwa ngozi, kusababisha madhara kwa mtoto anaenyonyeshwa na aliyepo tumboni, kusababisha saratani za aina mbalimbali ikiwemo ya ngozi na kuathirika kwa mifumo wa umeng'enyaji wa chakula.

Alisema vipodozi vilivyoteketezwa vimepigwa marufuku katika soko la Tanzania kwa sababu vina viambata sumu ikiwemo hydroquinone, butylmethyl propional, steroids, zinc pyrothione na zebaki.

Kwa upande wa nguo za ndani, alisema nguo hizo zimepigwa marufuku kwa sababu zinasababisha maradhi ya ngozi kama vile fangasi na maambukizi ya bakteria yanayopelekea magonjwa ya ngozi kwenye maeneo mbalimbali za mwili

Alisisitiza wananchi kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa wanazotaka kununua ili kujua kama hazijaisha muda wake wa matumizi na kama zimethibitishwa na TBS.

Kuhusu bidhaa zilizoisha muda wake, alisema usababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo ya matumbo, hivyo alitoa rai kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa wanazotaka kununua ili kujua kama hazijaisha muda wake wa matumizi na kama zimethibitishwa na TBS.

Kwa upande wa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali aliwataka kuhakikisha kuwa wanaingiza sokoni bidhaa zenye Ubora

"Rai yetu ni kuwa wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa kufuata kanuni, taratibu na Sheria ili kuepuka kupata hasara na kuchukuliwa hatua za kisheria. Ni vema wakawa wanawasiliana na Shirika la Viwango kwa kufika ofisi za TBS zilizo karibu nao au kwa mifumo yetu ya mtandaoni au kwa kupiga simu ya bure 0800110827 ili waweze kupewa maelezo au msaada," alisema .
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger