Saturday, 19 December 2020

Waziri wa Kilimo Prof.mkenda Apongeza Jeshi La Magereza Kwa Kilimo Bora Cha Michikichi

...


Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la serikali la kuongeza uzalishaji wa zao la michikichi ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula.


Ametoa pongezi hizo jana (18.12.2020) mkoani Kigoma wakati alipofanya ziara ya kukagua shamba na kitalu cha michikichi katika gereza Kwitanga ambapo amefurahishwa kuona miche bora zaidi ya 223,231 na mbegu bora 286,125 za michikichi aina ya tenera zenye kuzalisha mafuta mengi ya kula.


“Nawapongeza Gereza Kwitanga kwa kazi nzuri ya kupanda shamba jipya la michikichi lenye ukubwa wa ekari 450 msimu huu na pia kuzalisha miche na mbegu bora za michikichi hali itakayosaidia uzalishaji mafuta ya kula kuongezeka muda mfupi ujao” alisema Prof. Mkenda.


Prof. Mkenda alisema lengo la ziara yake Kigoma ni kufanya ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuhakikisha mkoa wa Kigoma unapanda michikichi mipya aina ya tenera yenye kutoa mafuta wastani wa tani 5 kwa hekta na kuachana na miche iliyozeeka aina ya Dula yenye ufanisi mdogo wa takribani tani 1.6 hadi 2 kwa hekta.


Waziri huyo wa Kilimo amewahakikisha wakulima wa Kigoma kuwa wizara yake itaendelea kuzalisha miche bora kwa kutumia kituo cha utafiti cha Kihinga hivyo waendelee kuandaa mashamba na kupanda miche bora iliyofanyiwa utafiti wa kisayansi ili wawe na uhakika wa mavuno mengi.


Awali Mkuu wa Gereza Kwitanga Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Dkt. Uswege Mwakahesya alitoa taarifa kuwa Jeshi la Magereza limejipanga na linatekeleza agizo la serikali la kupanda miche bora ya michikichi kwa kulima mashamba mapya ya zao hilo.


Dkt. Mwakahesya aliongeza kusema kuwa uwepo wa miche bora inayozalishwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) wana uhakika wa mbegu na miche hivyo kuendelea kupanda mashamba hayo.


“Gereza Kwitanga linatekeleza agizo la serikali la kuanzisha mashamba mapya ya michikichi ili kuwa na uhakika wa malighafi ya kuzalisha mafuta ya kula ambapo kwa sasa tunaendelea kuzalisha mafuta ya mawese yanayotumika kwenye magereza yetu mengi hapa nchini kwa kutumia miti iliyopo hapa shambani kwetu” alisema Dkt. Mwakahesya.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo alimweleza Waziri wa Kilimo kuwa taasisi yake imefanikiwa kuzalisha mbegu na miche bora ya michikichi milioni nne na laki mbili ambayo inasambazwa kwenye halmashauri sita za mkoa wa Kigoma.


Dkt. Mkamilo alisema kituo cha utafiti Kihinga kinashirikiana na taasisi za umma ikiwemo Gereza Kwitanga, JKT Bulombora ,Halmashauri za wilaya na miji pamoja na sekta binafsi kuzalisha mbegu na miche bora ili kufikia lengo la kila mwaka kusambaza mbegu milioni tano kwa wakulima wa Kigoma .


Waziri wa Kilimo yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ambapo kesho atashiriki kongamano la wadau wa zao la michikichi litakalofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.


Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger