Mkurugenzi wa Shirika la UWEZO Zaida Mgala akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya mradi huo kilichofanyika katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali.
Na Grace Mwakalinga, MBARALI
Asilimia 70 ya Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika katika wameweza kusoma ndani ya siku 30 kupitia mradi wa jifunze.
Mkurugenzi wa Shirika la UWEZO Zaida Mgala amesema hayo wakati wa katika kikao cha tathmini ya mradi huo kilichofanyika katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali.
Ameeleza kuwa kwa muda wa siku 30 walimu wa Shule zilizopo kwenye utekelezaji wa mradi huo wamefanikiwa kuwasaidia watoto waliokuwa hawajui kusoma na kuandika kwa kutengeneza mazingira rafiki na mbinu shirikishi ambazo zimesaidia kujifunza.
Amesema watoto wanajifunza kwenye mazingira rafiki ambayo yanawavutia kusoma, na kwa vitendo huku walimu kutumia lugha yenye upendo pamoja na michezo mbalimbali ili kutowachosha wanafunzi.
Ameongeza walimu walipewa mafunzo maalum kwa ajili ya kuwafundisha watoto, wazazi kushirikishwa kwenye meza za majadiliano na kuhamasika kuchangia chakula ambacho kinamsaidia mtoto katika suala la kujifunza.
"Jitihada hizi zimepunguza utoro kwa watoto kwa madai kuwa awali walikuwa wanakaripiwa au kugombezwa, mradi huu umewasaidia kuwapa mbinu za kujifunza kwa vitendo, kushirikiana hakuna kuchapwa viboko wala kugombania madawati bali wanakaa chini, wazazi wameshiriki kuchangia chakula ili kukaa muda wa ziada kujifunza," alisema Mgala.
Mratibu wa Shirika la ELIMISHA, Debora Mwanyanje amesema mradi wa Jifunze ulilenga watoto wasiojua kusoma na kuandika ambapo amezitaja miongoni mwa shule zilizonufaika na mradi huo kuwa ni Rujewa Nsonyanga na Mpakani.
Baadhi ya walimu waliofanya kazi hiyo ya tathmini wamesema licha ya uchache wa siku za kuwafundisha watoto wasiojua kusoma na kuandika lakini kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wanafunzi hao.
Mdhibiti ubora wa Elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Teobadina Mjimu, amewaomba walimu waliopata mafunzo hayo kuwapa mbinu za ufundishaji walimu ambao hawapo kwenye mradi huo ili waendelea kuwasaidia watoto wa madarasa yote wenye tatizo la kutojua kusoma na kuandika.
0 comments:
Post a Comment