Monday, 21 December 2020

Serikali Yapunguza Msongamano Wa Wafungwa Magerezani

...


Na Veronica Mwafisi-MOHA-Dodoma
SERIKALI imefanikiwa kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani kupitia Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291, Sheria ya Majaribio na Ujenzi wa TabiaSura ya 247 na Sheria ya Magereza Sura ya 34/1967, Kifungu cha 52.

Kwa mujibu wa sheria hizo, wahalifu waliohukumiwa vifungo visivyozidi miaka mitatu hutumikia adhabu nje ya magereza.

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uangalizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye Katibu wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii, Aloyce Musika aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya idara hiyo.

Taarifa hiyo iliwasilishwa kwenye kikao cha kamati ya idara hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki Ukumbi wa Mikutano wa TANAPA, Jengo la Kambarage, jijini Dodoma.

“Lengo la kuanzishwa idara hii ni kuipunguzia serikali gharama za kuhudumia wafungwa magerezani, kudhibiti tatizo la urudiwaji uhalifu,kupunguzwa msongamano wa wafungwa magerezani.

“Hadi kufikia Novemba 30, 2020, wafungwa 1,781 walikuwa wanaendelea kutumikia adhabu za nje ya gereza, wafungwa 1,447 walimaliza kutumikia adhabu zao,” alisema Musika.

Alifafanua kuwa, mafanikio mengine yaliyofikiwa na kamati hiyo ni kudumisha amani na utulivu katika jamii, kuimarika mahusiano kati ya idaara na wadau ambapo hivi sasa idara inafanya kazi kwa karibu na wadau wote wa haki jinai.

Mafanikio mengine ni kupanua wigo wa kutekeleza majukumu ya idara katika mikoa yote Tanzania Bara, kununua vitendea kazi, kuipunguzia serikali ghaarama za kuendesha magereza.

“Dira yetu ni kuwa chombo kinachozingatia weledi, taratibu, vigezo vya kitaifa na kimataifa katika urekebishaji wahalifu ndani ya jamii,” alifaafanua Musika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Huduma kwa Jamii, Jaji Zephrine Galeba aliitaka kamati hiyo iendelee kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

“Umefika wakati wa kamati kujitathmini kama inaenda mbele au inarudi nyuma, naomba msirudi nyuma wala kujipangia kiwango kikubwa ili mtekeleze majukumu yenu,” alisema.

Alimuomba Musika amfikishie salamu za shukrani kutoka kwenye kamati kwenda kwa Maafisa Huduma kwa Jamii kutokana na utendazi mzuri wa kazi, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Aliwataka Maafisa Huduma kwa Jamii waendelee kufanya kazi kwa weledi wakitambua kuwa wamepewa majukumu makubwa hivyo wana mamlaka ambayo si madogo.

Pia aliwataka wawe na maadili, waaminifu, kuwashukuru wageni wote waalikwa na baadhi ya Wakuu wa Idara kutoka wizarani kwa kushiriki kikao hicho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger