Sunday, 20 December 2020

Serikali Kwa Kushirikiana Na Vyama Vya Wafanyakazi Madereva Na Vyama Vya Wamiliki Wa Vyombo Vya Usafirishaji Wajipanga Kuimarisha Sekta Ya Usafirishaji Nchini

...


Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji kwa pamoja wamejipanga kushirikiana katika kupata ufumbuzi wa kero na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili sekta hiyo ya usafirishaji nchini.

Hayo yamebainishwa jana Disemba 19, 2020 Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha mashauriano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo jengo la PSSSF.

Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho Kamishna wa Kazi, Brig. Gen. Francis Mbindi alieleza kuwa sekta ya usafirishaji inatoa mchango muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo serikali imekua ikuchukua hatua madhubuti ili kuimarisha sekta hiyo.

“Sekta ya usafirishaji ni moja ya nyenzo muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani, na ni dhairi serikali katika kulitambua hilo imeendelea kuimarisha sekta hiyo na kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika sekta hiyo,” alieleza Brig. Gen. Mbindi

Alieleza kuwa, wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akifungua Bunge la 12 tarehe 13 Novemba, 2020 aliahidi kuwa serikali itahakikisha wamiliki wa magari wanatoa mikataba ya ajira kwa madereva ili kuipa hadhi inayostahili kazi hiyo na kuchochea shughuli za huduma za usafirishaji.

“Ninyi kama wadau muhimu wa sekta hii mna mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa ahadi hiyo, na tuliona ni vema tukutane na kushauriana na kuweka mikakati ya pamoja,” alisema Brig. Gen. Mbindi

Alifafanua kuwa baadhi ya kero na changamoto zimeweza kupatiwa ufumbuzi ikiwemo kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi madereva ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa katika kuleta uhuru wa madereva kwenye utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria za kazi. Pia maboresho yamefanyika katika mkataba wa ajira ya madereva sambamba na makubaliano kuhusu viwango vya posho za safari kwa madereva ndani na nje ya nchi.

“Katika kusimamia utekelezaji wa mkataba ulioboreshwa mara kadhaa tumekuwa tukishirikiana nanyi katika kufanya ukaguzi kwenye vituo vikuu vya mabasi na baadhi ya maeneo ya kazi na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili waweze kuzingatia matakwa ya sheria,” alisema

Aliongeza kuwa, pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali katika kusimamia utekelezaji wa sheria lakini bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa sheria za kazi huku akitolea mfano wa baadhi ya waajiri wamekuwa hawatoi mikataba ya ajira kwa madereva, kutowapa haki wafanyakazi haki ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi na kutowasajili na kuwachangia madereva kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

 Aidha Kamishna wa Kazi amewataka Wafanyakazi Madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji kuzingatia matakwa ya sheria za kazi wanapotekeleza majukumu yao.

Naye, Mwakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (CHAWAMATA) Bw. Greyson Wimile alieleza kuwa wamefarijika na namna ambavyo serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikitatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi madereva ikiwa ni kipaumbele kwa madereva kutambua wanathaminiwa na kazi hiyo wanayoifanya.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger