Jopo la majaji pamoja na uongozi wa LHRC wakiwa katika picha ya pamoja na mwakilishi wa familia ya Hayati Godfrey Luena, Frank Luena baada ya kukabidhiwa Tuzo ya Maji Maji
Frank Luena, mwakilishi wa familia Hayati Luena akiwa ameshikilia tuzo katika picha ya pamoja na Ally Masoud (Kipanya) (kushoto kwake) pamoja na Robby Samwelly (kulia kwake). Wengine ni mwakilishi wa Fatma Karume (wa kwanza kushoto) na mwakilishi wa Vicky Ntetema (wa kwanza kulia)
***
Usiku wa Disemba 10, 2020 ulishuhudia tukio la kihistoria la utoaji tuzo za Haki za Binadamu za Maji Maji tukio ambalo hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano. Usiku wa Tuzo ya Maji Maji ulikuwa pia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambayo huadhimishwa Disemba 10 kila mwaka.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilikutanisha wadau wa haki za binadamu kushuhudia zoezi la kuwatambua watetezi wa haki za binadamu waliotetea haki za binadamu kwa ujasiri katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015 mpaka 2020.
Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Hayati Godfrey Luena alitunukiwa tuzo hiyo baada ya kupata alama nyingi zaidi kutoka kwa jopo la majaji. Jopo la majaji lililoundwa na watu mashuhuri na wenye uzoefu mkubwa katika utetezi wa haki za binadamu lilipitisha majina matano kutoka katika majina 32 yaliyochujwa kutoka katika mapendekezo ya wananchi na baadae kutoa alama kwa wanaharakati hao walioingia tano bora na hatimaye kumpata Godfrey Luena.
Jopo la majaji ambalo liliongozwa na mwanaharakati nguli na Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa LHRC, Dkt. Helen Kijo-Bisimba liliundwa na Dkt. Helen mwenyewe, Jenerali Ulimwengu (mwanahabari nguli na mtetezi wa haki za binadamu), Tom Bahame Nyanduga (Mwenyekiti wa Zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na mtetezi wa Haki za Binadamu), Dkt. Benson Bagonza (Kiongozi wa dini na mtetezi wa Haki za Binadamu) pamoja na Aidan Eyakuze (Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza na mtetezi wa Haki za Binadamu).
Watetezi wengine walioingia katika orodha ya tano bora ya majaji ni pamoja na Ally Masoud (Kipanya) – ambaye amekuwa akitetea haki za binadamu na kuhimiza utawala bora kupitia kazi yake ya uchoraji katuni na utangazaji. Fatma Karume ambaye amekuwa akitumia taaluma yake ya sheria kuhimiza utawala wa sheria pia aliingia tano bora. Roby Samwelly, mtetezi wa haki za wasichana na wanawake mkoani Mara pia aliingia tano bora. Vicky Ntetema ambaye ni mwanahabari nguli na mtetezi mashuhuri wa haki za watu wenye ualbino alihitimisha orodha ya tano bora.
Wote walioingia tano bora walitunukiwa vyeti vya utambuzi kama watetezi wa Haki za Binadamu waliojitoa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kutetea haki za binadamu bila kujali vitisho.
Hayati Godfrey Luena ametunukiwa tuzo ya Haki za Binadamu ya Maji Maji kufuatia kujitoa kwake katika kusimamia haki za wananchi wa mkoa wa Morogoro hasa wilaya ya Kilombero, Ifakara na Ulanga.
Katika kipindi cha uhai wake Hayati Luena alijitoa bila kujali vitisho na maslahi yake binafsi kutetea haki za wananchi waliodhulumiwa haki ya kumiliki ardhi na walioonewa na mamlaka kwa kusingiziwa makosa na kunyimwa haki ya dhamana. Hayati Luena alipitia changamoto mbalimbali katika kutetea haki za binadamu ikiwemo kutishiwa maisha na kubambikiwa kesi ili kukatisha juhudi zake za kutetea haki na maslahi ya wananchi.
Kabla ya kuuawa kikatili mwaka 2018 na watu ambao mpaka sasa hawajatambulika, Hayati Luena aliwahi kubambikiwa kesi saba ambazo alishinda zote kwa msaada wa kisheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Pia, Hayati Luena aliripoti kupokea vitisho dhidi ya usalama wake na usalama wa familia yake kutokana na harakati zake za utetezi wa haki za binadamu.
Hayati Godfrey Luena akiwa nje ya jengo la LHRC enzi za uhai wake
Wasifu kamili wa Hayati Godfrey Luena
Mahali Alipozaliwa & Familia
Godfrey Joachim Sinandugu Luena alizaliwa tarehe 12 mwezi Juni mwaka 1976 katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, eneo la Ifakara katika Wilaya ya Kilombero. Alikuwa ni mtoto wa nne kati ya watoto kumi na mbili wa Joachim Sinandugu Luena na Joyce William Tayari, wakazi wa Kijiji cha Namwawala kilichopo katika Tarafa ya Mgeta wilayani Kilombero. Aliyaishi maisha yake vizuri hadi alipouawa kikatili na watu wasiojulikana mwaka 2018. Hayati Godfrey Luena alijaaliwa watoto saba.
Elimu
Safari ya elimu ya Hayati Godfrey Luena ilianzia katika Shule ya Msingi Namwawala kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995, kisha akaendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Kwiro, ambapo alisoma kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 1999.
Taaluma, Kazi, na Utambuzi wa Kazi Alizofanya
Hayati Godfrey Luena alikuwa ni mkulima na mfanyabiashara wilayani Kilombero. Pia, alikuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na haki za ardhi, ambapo alifanya kazi ya uangalizi wa haki za binadamu chini ya LHRC, sambamba na kuwa msaidizi wa kisheria. Kutokana na kazi alizokuwa anafanya na kuwasaidia watu kupata haki zao, Godfrey Luena alijipatia umaarufu, jambo lililopelekea pia kushawishiwa kuingia katika siasa, ambapo mwaka 2000 alijiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na kugombea udiwani katika Kata ya Idete. Hata hivyo hakufanikiwa kushinda katika uchaguzi wa madiwani. Mwaka 2007 alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo aligombea mara mbili nafasi za udiwani na hatimaye kushinda kiti cha udiwani katika Kata mpya ya Namwawala mwaka 2015. Hayati Luena alishika wadhifa huo hadi alipouawa mnamo mwezi Februari mwaka 2018. Harakati zake za kutetea haki za binadamu na haki za ardhi, akiwapambania wananchi wa Wilaya ya Kilombero kupata haki zao kulipelekea watu kumuomba kugombea udiwani ili awasaidie zaidi. Hata hivo juhudi zake zilipelekea kupokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana, hadi pale alipouawa.
Hayati Luena anakumbukwa zaidi kwa kazi zake za utetezi wa haki za ardhi wilayani Kilombero. Aliwapigania kwa hali na mali wahanga wa ukiukwaji wa haki za ardhi kufikia haki na alitumia muda wake mwingi kuwasaidia kupata haki zao katika mahakama na majukwaa mengine. Pia, alikuwa ni mwangalizi mzuri wa haki za binadamu.
Mchango wake katika Kukuza Haki za Binadamu
Hayati Luena alikuwa na mchango mkubwa katika ukuzaji na utetezi wa haki za binadamu wilayani Kilombero. Alifanya vizuri kazi ya uangalizi wa haki za binadamu wilayani humo na kutoa usaidizi wa kisheria pale ilipohitajika, sambamba na kutoa elimu ya sheria na haki za binadamu. Alikuwa mtetezi mahiri wa haki za ardhi (haki ya kumiliki mali) na haki za binadamu kwa ujumla. Alitumia muda wake kueneza uelewa kuhusu masuala ya ardhi, akitumia ufahamu na uzoefu wake kuhakiksha watu wanajua kuhusu haki yao ya kumiliki mali na haki zao pale ambapo ardhi yao imetwaliwa kwa ajili ya uwekezaji na sababu nyingine. Alipendelea kuona haki ikitendeka na alijitoa sana katika kuwasaidia watu wengine. Pia, alisaidia kuwalea na kukuza uwezo wa watetezi wengine wa haki za binadamu ndani ya Bonde la Mto Kilombero (Ulanga, Malinyi, na Kilombero).
Kesi na migogoro ambayo Godfrey Luena alisaidia kufanyia utetezi ni pamoja na:
Kulinda haki za ardhi za wanakijiji waliopo kwenye vijiji vya pembezoni mwa Bonde la Kilombero (Ramsar), ambapo alisaida kufungua kesi dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Kesi na. 161 ya mwaka 2015) katika Mahakama Kuu – Kitengo cha Ardhi. Mahakama iliamua kwamba Serikali iende kupitia upya mipaka ya bonde hilo na maamuzi yake yalinufaisha asilimia 65 ya vijiji.
Kushiriki utetezi wa mgogoro wa ardhi kuhusu Mto Luipa/Kilombero, uliopelekea wananchi kutoka katika Kijiiji cha Luipa kuunda tume ya watu kumi na moja, akiwemo yeye, ambayo ilipanga kwenda kuonana na Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete (Rais mstaafu) katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo. Hata hivyo, tume hiyo haikuweza kutekeleza majukumu yake baada ya wajumbe wake kuandamwa na kesi za kubambikizwa, ambapo Hayati Luena alibambikiwa kesi saba. Hata hivyo, hakukata tamaa. Kwa kushirikiana na wenzake, alifungua kesi katika Mahakama Kuu- Kitengo cha Ardhi mwaka 2012 (kesi na. 40 ya mwaka 2012), ambayo iliisha mwaka 2014. Katika hukumu yake, Mahakama Kuu ilidai kwamba Serikali haina budi kufuata taratibu za kisheria katika utwaaji wa ardhi, ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapewa fidia stahiki. Juhudi za Luena zilisaidia kushinda kesi hii.
Kushirikiana na wenzake wawili kuwatetea wananchi wa Kijiji cha Chita katika mgogoro wao wa ardhi dhidiya Chita JKT, mgogoro ambao ulitatuliwa kwa usuluhishi na Chita JKT kuridhia kuwaachia wananchi hao ekari 1600.
Kuwasaidia wanakiji wa Kijiji cha Chiwachiwa katika mgogoro wao dhidi ya kampuni ya usafirishaji iitwayo UNION, ambapo aliwasaidia kufungua keshi na. 9 ya mwaka 2015 katika Mahakama Kuu – Kitengo cha Ardhi.
Kushirikiana na wenzake watatu kuwasaidia wanakiji wa Kijiji cha Katindiuka kudai fidia baada ya ardhi yao kutwaliwa. Wanakiji hao walikuwa na mgogor na Halmashauri ya mji wa Ifakara. Juhudi za Hayati Luena zilichangia wanakijij hao kupewa fidia.
Pia, mwaka 2015 Hayati Luena aliwasaida wananchi 35 wilayani Kilombero na Ulanga ambao walikamatwa kwa tuhuma za kuchoma majengo ya Serikali, ikiwemo jengo la baraza la ardhi, baada ya kunyimwa dhamana. Walitakiwa kuweka rehani mali isiyohamishika yenye thamani ya Tshs. 60,000,000 ili waachiwe huru kwa dhamana, lakini hawakuwa na mali hiyo, hali iliyopelekea wakae mahabusu kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Hayati Luena alijitolea kuweka rehani hati ya nyumba yake na kufanikisha zoezi la wananchi hao kuachiwa kwa dhamana. Aliendelea kufuatilia kesi hiyo hadi wananchi hao walipoachiwa huru baada ya kesi kufutwa. Pia, aliwasaida wanakijiji 13 ambao walikamtwa kwa tuhuma za kufanya vurugu katika Kampuni ya KPL na kunyimwa dhamana. Alishirikiana na wenzake wawili kuhakikisha wanakiji hao wanaachiwa huru kwa dhamana.
Kabla ya kifo chake mnamo mwezi Februari mwaka 2018, Godfrey Luena alikuwa anajiandaa kuanzisha maktaba ndogo ya machapisho ya sheria na haki za binadamu kwa lengo la kukuza uelewa wa sheria na haki za binadamu katika jamii yake. Pia, alikuwa anafanyia kazi mradi wa kujenga kisima kirefu, chenye thamani ya Tshs. 60,000,000 ili kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Namwawala kupata na kutumia maji safi na salama. Hata hivyo, tarehe 22 mwezi wa 2 mwaka 2018, mida ya saa saba usiku, Godrey Luena alivamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kuuawa kikatili kwa kukatwa mapanga nje ya nyumba yake. Alitoka nje kuangalia mita ya umeme baada ya umeme kukatika ghafla, ndipo alipovamiwa na kuuawa kikatili.
Kuhusu Tuzo ya Haki za Binadamu ya Maji Maji
Tuzo ya Haki za Binadamu ya Maji Maji hutambua wanaharakati hodari wa haki za binadamu Tanzania. Tangu ilipoanzishwa mwaka 2005, tuzo ya Maji Maji hutolewa kila baada ya miaka mitano kwa mtanzania aliyeonesha uthubutu na umahiri wa kipekee katika kulinda na kutetea haki za binadamu, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora.
Watanzania watatu ambao waliwahi kutunukiwa tuzo hii ni pamoja na Jaji James Mwalusanya (hayati), Dkt. Wilbroad Slaa, na Ludovick Utoh. Tuzo tatu za kwanza za Maji Maji zilitolewa kwa watetezi wa haki za binadamu ambao waliwakilisha mihimili mitatu ya dola ambayo ni mahakama, bunge na serikali. Kwa mwaka 2020, tuzo ya Maji Maji itatambua mchango wa raia wa kawaida anayejitoa kusimamia haki.
Tuzo ya Maji Maji ilianzishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambalo ni shirika la utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania.
0 comments:
Post a Comment