Friday, 11 December 2020

AFARIKI DUNIA KWA KULA MZOGA WA NGURUWE PORI... NANE WALAZWA KATAVI

...
Nguruwe pori
Na Walter Mguluchuma -Katavi
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Katarina Zebedayo (38) mkazi wa Kijiji cha Kabanga Kata ya Ilangu, Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi amefariki dunia baada ya kula nyama ya mnyama pori aina ya nguruwe pori huku watu  wengine nane wakilazwa katika kituo cha afya Mishamo kwa ajili ya matibabu.

Kamanda wa polisi mkoa wa katavi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Benjamin Kuzaga amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tisa alasiri katika Kijiji cha Kabage Kata ya Ilangu.

Amesema kuwa katika tukio hilo wananchi wa kijiji hicho waliona mnyama adhaniwaye kuwa ni nguruwe pori akiwa amekufa porini jirani na mashamba yao ndipo walimchuna ngozi na kugawana nyama na kuondoka nayo majumbani kwa ajili ya kitoweo. 

Kamanda Kuzaga amewataja wahanga wengine katika tukio hilo kuwa ni Leonard Kabula, (17) Sifa Kabula, (04), Levis Kabula, (03), Boniphace Kabula, (01) Seth Eliya, (30) Lidness Mayokolo, (09) Noadia Balasiano, (36), Sostenes Phillipo, (01) wote wakazi wa Kijiji cha Kabanga.

Wananchi hao wanadaiwa baada ya kutumia kitoweo hicho na kupata madhara walianza kutumia dawa za kienyeji mpaka baada ya mmoja wao kuzidiwa na kufariki ndipo mwenyekiti wa Kijiji hicho Theodoli Philipo, (30) alibaini na kufanya jitihada ya kuwafikisha wahanga wengine katika kituo cha afya Mishamo

Kamanda Kuzaga amesema kuwa baada ya mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi huku sampuli zikiwa zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kubaini hasa sumu iliyopelekea kifo pamoja na madhara kwa watu hao.

Aidha, ameongeza kuwa wahanga wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Mishamo na hali zao zinaendelea vizuri. 

Pia amewataka wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi kutojihusisha na uwindaji haramu, na kuacha tabia ya kula vitoweo ambavyo vinakuwa vimakufa katika mazingira ambayo si salama ili kuweza kujiepusha na madhara yanayoweza kuepukika
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger