Wamikili wa nyumba saba Zanzibar ambazo ni maarufu kwa kufanyiwa biashara ya ukahaba ‘machangudoa’ wametakiwa kuripoti kwa Kamanda wa Polisi, Mjini Magharibi, Zanzibar ifikapo kesho.
Hatua hiyo kwa wamiliki wa nyumba hizo visiwani humo kunatokana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo kufanya operesheni ya kudhibiti biashara hiyo ambapo watu 22 wanaofanya biashara hiyo walikamatwa katika nyumba hizo zilizoko katika maeneo ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alitoa agizo hilo baada ya operesheni hiyo.
Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Mkuu wa mkoa huyo, alisema wamiliki wa nyumba hizo wanatakiwa kuripoti ifikapo saa nne asubuhi na atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua.
Alizitaja nyumba hizo ni zilizoko katika maeneo ya Raha Leo, Mwembe Shauri, Miembeni, Kikwajuni Juu na Kilimani na kwamba kamati ya ulinzi na usalama imejiridhisha kwenye nyumba hizo zinafanywa biashara za ukahaba.
Alisema biashara hiyo si halali, hivyo aliwataka wanaofanya biashara hiyo kuacha na watafute shughuli nyingine ya kujipatia kipato halali.
Wakati wamiliki wa nyumba hizo Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar wakitakiwa kuripoti polisi kesho, Polisi mkoani Singida imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11 wakiwemo wanawake 10 na mwanaume kwa tuhuma za kujihusisha na kufanya biashara ya ukahaba mjini Singida.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa huo , Sweetbert Njewike, alisema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na misako wa kubaini vitendo vya uhalifu na wahalifu wa makosa mbalimbali katika Mji wa Singida na viunga vyake.
Alisema msako huo ulifanyika Desemba 18 na 19, mwaka huu, katika maeneo ya Serengeti, kata ya Majengo na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao.
0 comments:
Post a Comment