Wamiliki wa Maabara binafsi za Afya wametakiwa kufuata sheria na kanuni za kumiliki Maabara binafsi ikiwemo kulipa ada stahiki za uhakiki wa ubora wa huduma na ukaguzi za kila mwaka na yeyote atakeyekiuka hatua kali za kisheria dhidi yake zitachukuliwa. Akizungumza na waandishi wa Jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi wa Tiba WAMJW na ni Mwenyekiti Bodi ya usajili wa maabara binafsi za Afya (PHLB)Dkt Dorothy Gwajima amesema kuwa wasiofuata sheria na kutoa huduma bubu huku wakiwa karibu na ngazi za serikali za mitaa hivyo bodi itashirikiana na tamisemi kuhakikikisha…
Monday, 31 December 2018
MWILI WA MWANASIASA MKONGWE NDEJEMBI KUZIKWA KESHO DODOMA
Mwili wa mwanasiasa mkongwe nchini Pancras Ndejembi unatarajia kuzikwa kesho Jumanne Januari Mosi, 2019 katika kitongoji cha Chizomoche kijiji cha Bihawana Jijini Dodoma.
Ndejembi (90) alifariki dunia Jumamosi Desemba 29, 2018 saa 2 asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Mweyekiti wa kamati ya mazishi, David Mzuri amesema leo Jumatatu Desemba 31, 2018 kuwa maandalizi yote yamekamilika ikiwemo watoto wa marehemu ambao walikuwa wanasubiriwa kutoka nje ya nchi.
Mzuri amesema mwili wa marehemu ulitarajia kuchukuliwa hospitali leo na kulala nyumbani kwake mtaa wa Uzunguni kata ya Kilimani.
“Kesho saa sita mchana tutapeleka mwili wa mpendwa wetu Kanisa la Mtakatifu Paul wa Msalaba na ibada itafanyika pale kisha msafara utaelekea Chizomoche kwa ajili ya mazishi,” amesema.
Baadhi ya viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu ni mawaziri wakuu wastaafu Mizengo Pinda na John Malecela. Viongozi wengine wastaafu ni Balozi Job Lusinde, Joseph Butiku, William Kusila na Hezekia Chibulunje.
POLISI DODOMA WAKANUSHA MTOTO WA MTOTO KUFUNGIWA KABATINI
Wakati binti wa kazi akieleza jinsi mwanaye mwenye umri wa miezi mitano alivyofungiwa kabatini na mwajiri wake mkoani Dodoma kwa muda wa miezi sita, Jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini.
Binti huyo wa miaka 15, jana Desemba 30, 2018 akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alidai kufanyiwa ukatili kwa kupigwa na kufanyishwa kazi hadi usiku wa manane na bosi wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu na kwamba amekuwa akimwambia amfungie hadi usiku mtoto wake na kila alipovunja masharti alikumbana na kipigo.
Leo Desemba 31, 2018 polisi mkoani Dodoma imekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini kama inavyodaiwa, lakini wamekiri binti huyo kushambuliwa na mwajiri wake.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto amesema polisi wamefanya upekuzi katika nyumba ya mwajiri wa binti huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu, Anitha Kimako na kubaini hakuwa na kabati nyumbani kwake.
"Kesi ya shambulio ipo na ameshambuliwa kweli na ndiyo maana tunamshikilia. Anashikiliwa kutokana na usalama wake kwani kelele za watu ni nyingi, ila hili suala la kuwekwa mtoto kabatini halipo," amesema Muroto.
Amesema uchunguzi wa kina unafanyika na kwamba lazima mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Medali afikishwe mahakamani.
SERIKALI YATOA MAAGIZO KWA WAMILIKI WA VITUO VYA AFYA NA MAABARA BINAFSI
Wamiliki wa maabara na vituo vya afya nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao mara moja bila shurti kabla ya Januari 15 2019 kwa kuhakikisha wanakamilisha vigezo vyote vya umiliki maabara hizo kwa kuwa muda wa kutoa elimu umepita na sasa ni muda wa kazi tu.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto na Mkurugenzi wa bodi ya usajili wa maabara Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa hadi kufikia Septemba 2018 bodi ya usimamizi wa maabara binafsi ilitambua jumla ya maabara 641 zinazojitegemea na maabara 719 zilizoshikizwa kwenye vituo vya tiba vya watu binafsi vya ngazi mbalimbali.
Amesema kuwa kutokana na baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi hasa zilizoshikizwa kutofuata maadili ya uwajibikaji kisheria kufikia Septemba 20, bodi kupitia ziara yake imebaini kuwa kati ya vituo vya tiba 1731vya watu binafsi vyenye maabara ndani ni maabara 1012 sawa na asilimia 58 pekee ndizo zilizotimiza wajibu wake wa kujiandikisha kwenye bodi ya usimamizi wa maabara binafsi na kutekeleza matakwa ya kisheria.
Amesema kuwa wamiliki ambao hawatatekeleza wajibu wao wa kumiliki maabara hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo pamoja na faini au vyote kwa pamoja.
Amewataka wamiliki hao kuhakikisha kuwa kila mmoja awe amekidhi vigezo vyote vya umiliki wa maabara ikiwa ni pamoja na kulipa ada zote stahiki zikiwemo malimbukizo ya nyuma na faini stahiki pamoja na kuwa na risiti halali za malipo hayo. Pia amewataka wamiliki wa maabara hizo kulipa tozo stahiki kila mwaka ili kuwezesha bodi kufanya uhakiki wa kudumu wa huduma zitolewazo katika maabara hizo.
Vilevile amesema kuwa katika kutekeleza hilo watatoa orodha za zahanati katika gazeti la Serikali na zahanati isiyokuwapo kwenye orodha hiyo haitatakiwa kutoa huduma yoyote na watakaokiuka watakutana na mkono wa dola. Gwajima ametoa mwito kwa serikali katika ngazi zote kushirikiana na kutoa taarifa dhidi ya wavunja sheria na kufanikisha kuipeleka mbele sekta hiyo.
Akieleza kuhusiana na faini zitakazotolewa Kaimu Afisa msajili wa bodi ya usimamizi ya maabara binafsi Neema Halliye amesema kuwa kwa mujibu wa sheria watakaokiuka sheria hiyo watapigwa faini ya kulipa kiasi cha shilingi laki mbili au kufungwa miaka miwili au vyote kwa pamoja na bado maboresho ya sheria hiyo yanafanyiwa kazi ili kuweza kutoa kibano zaidi.
HII NDIYO SABABU YA BASI LA MWENDOKASI KUUNGUA MOTO
Kampuni inayotoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (UDA-RT) imeeleza chanzo cha ajali iliyoyokea mchana Desemba 25, mwaka huu eneo la Ubungo Maji ilitokana na hitilafu ya mfumo wa umeme.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, John Nguya kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 155 ,lilikuwa likitokea Kimara kwenda Gerezani lilishika moto kwenye injini na kuwatia hofu abiria na wananchi wengine.
Alisema kuwa moto huo ulidhibitiwa kwa ushirikiano wa wananchi waliokuwa eneo hilo,Jeshi la Zima Moto na Uokoaji , Jeshi la Polisi na wafanyakazi wa UDART kwa kutumia vifaa vya kuzima moto vilivyomo kwenye magari hayo.
“Tungependa wananchi wafahamu kwamba usalama wa mabasi yote ya UDA -RT umedhibitiwa kwa asilimia 100 kuwa matengenezo take yanafanyika kwa umahiri ,viwango vya kimataifa kwa wasimamizi na watalaam kutoka kampuni ya Xiamen Golden Dragon ya China, Cummings ya Marekani ya kimataifa na Voith ya Ujerumani.
“Ndani ya mabasi hayo eneo la injini vipo vizimia koto vitatu vilivyotengenezwa humor na kuzima moto baada ya koto kuzidi na ndivyo ilivyokuwa wakati wa tukio na pia mabasi makubea kuna vizimia moto vinne vyenye ujazo wa kilogramu tatu katika kila mlango mikubwa ya pande zote mbili kwa akili ya dharura,” alisema Nguya.
Nguya alisema kuwa kwa mujibu wa sheria katika mabasi yote makubwa vipo vizimia moto vine vyenye ujazo wa kilogramu tatu kila kimoja na milango mikubwa pande zorte mbili kwa ajili ya dharura na matumizi ya kawaida.
AFGHANISTAN YAONGOZA VIFO WANATASNIA YA HABARI 16 WAUAWA 2018
Shirikisho la mashirika ya waandishi wa habari, IFJ imesema kuwa idadi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa tasnia ya habari waliouawa mwaka wa 2018 imepanda na kufika 94. Miongoni mwa hao 84 walikuwa waandishi wa habari, wapiga picha, mafundi mitambo na madereva. Kulingana na ripoti ya shirika hilo, nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari mwaka huu unaomalizika ilikuwa, Afghanistan ambako wafanyakazi 16 wa taaluma ya habari walipoteza maisha, ikifuatiwa na Mexico ambako 11 waliuawa. Nchi zingine ni Yemen, Syria, India, Somalia, Pakistan na Marekani.
CCM TABATA YAPIGA MARUFUKU KUTOA TAARIFA ZA CHAMA MITANDAONI
Na Heri Shaban CHAMA cha Mapinduzi CCM Tabata Mtambani kimetoa Elimu na kuwapiga msasa Jumuiya za Chama hicho kwa kuwapa elimu kila kiongozi afahamu majukumu yake. Semina hiyo iliandaliwa na CCM Tabata Mtambani ilifunguliwa Dar es salaam hii leo,na Katibu wa CCM Tabata Haruna Aliphonce ambapo katika ufunguzi alipiga marufuku taarifa za chama cha mapinduzi kujadiliwa mitandaoni badala yake aliwataka wana CCM masuala ya chama yasijadiliwe mitandaoni yafanyike katika vikao halali. Haruna aliwataka wana CCM kutumia vikao vyao vya kanuni na kufuata taratibu za chama cha Mapinduzi waachane na utandawazi…
SIMBA YAONESHA UTII
Kocha wa Simba Patrick Aussems
Licha ya kukabiliwa na mechi ya klabu bingwa Afrika hatua ya makundi klabu ya Simba, imesema itasafiri siku ya Jumatano ya tarehe 2.01.2019, kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Simba imeeleza kuwa inaondoka na kikosi kamili ili kufanya vizuri kwenye mashindano hayo, na pia kuipa mazoezi timu hiyo ambayo inajiwinda na mechi ya kwanza ya kundi D ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria.
Mechi dhidi ya JS Saoura inatarajiwa kupigwa Uwanja wa Taifa hapa Jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi ya tarehe 12 Januari saa kumi alasiri.
''Iwapo tutafuzu kuingia nusu fainali ya Mapinduzi, kikosi cha pili kitabaki Zanzibar na baadhi ya wachezaji, huku wengine wakirejea Dar es Salaam kuwakabili JS Saoura'', imeeleza taarifa ya Simba.
Aidha Simba wameeleza kuwa kwa kuwa fainali ya Mapinduzi itafanyika Januari 13, na kama watafuzu kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kurejea Zanzibar kucheza fainali hiyo.
Kwenye kombe la Mapinduzi Simba ipo kundi A na timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba.
Taharuki ! KABURI LAFUKULIWA..SANDA YACHOMWA MOTO
Taharuki katika kitongoji cha Kipondoda wilayani Manyoni mkoani Singida baada ya kaburi moja ambalo linadaiwa kuzikwa mtu siku tano zilizopita na kukutwa limefukuliwa huku sanda ikiwa imechomwa moto upande wa miguuni.
Mwajiri wa marehemu ambaye alishiriki maziko ya ndugu huyo, amesema marehemu Jamal Mkumbo alizikwa Desemba 25, mwaka 2018 kwa kufuata tararibu zote lakini ameshangazwa kukuta kaburi limefukuliwa na sanda kuchomwa moto kutokana nakudaiwa kuwa inawezekana ni imani za kishirikina.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji hicho bw. Jackson Job amekiri kutokea kwa tukio hilo na wamekemea tabia za aina hiyo.
Matukio ya makaburi kufukuliwa wilayani Manyoni yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kudaiwa wanaofanya hivyo wamekuwa wakijihusisha na imani za kishirikina.
ANUSURIKA KIFO KWA KUCHOMWA MKUKI KISA UGOMVI WA SHAMBA
Na,Naomi Milton Serengeti Mwita Mtatiro(30) mkazi wa Kijiji cha Kwitete wilayani Serengeti amenusurika kufa baada ya kuchomwa mkuki na mtu aitwaye Nkori Mwita mkazi wa Kijiji cha Kwitete chanzo kikielezwa kuwa ni mgogoro uliopo baina yao kuhusu mpaka wa shamba Mtatiro aliyelazwa wodi ya wanaume kitanda namba 2 katika hospital Teule ya Nyerere Ddh anaugulia maumivu huku akiwa na jeraha eneo la kifuani na ubavuni wakati hali yake ikionekana kuwa sio nzuri kwani mpaka sasa hajaweza kuinuka wala kuzungumza Akisimulia chanzo cha tukio mmoja wa majirani aliyemfikisha Hospitalini hapo Chacha…
UHURU MEDIA GROUP YAWAPA MOTISHA WAFANYAKAZI WAKE WOTE
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group Faustine Sungura akimkabidhi mmoja wa wafanyakazi kutoka Idara ya Utawala,Banga Lucas kiasi cha fedha ikiwa ni sehemu ya motisha iliyotolewa kwa wafanyakazi wote wa kampuni hiyo ikiwa kama sehemu ya kuthamini mchango wao.Picha na Michuzi Jr-MMG.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group ambayo inasimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Faustine Sungura akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo kuwapa motisha wafanyakazi wote wa kampuni hiyo kama sehemu ya kuthamini mchango wao,aidha mbaliya kutoa motisha atatumia nafasi hiyo kufanya uhakiki wa wafanyakazi waliopo kwenye vyombo hivyo na iwapo kutakuwa na wafanyakazi hewa atawabaini.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group Faustine Sungura akielezea mbele ya Waandishi wa habari leo Ofisini kwake jijini Dar,namna kampuni hiyo inavyojipanga ,amesema kuanzia mwakani wataanza kufanya utafiti utakaochukua muda wa miezi mitatu na lengo ni kufahamu wasomaji wao,wasikilizaji wao na watazamaji wao wanataka nini."Pia Februari mwaka
2019 tutafanya 'uzinduzi laini' wa vyombo vyetu na Aprili 2019 tutafanya uzinduzi rasmi,ambapo ndio tutazungumza malengo na mikakati yetu.",alifafanua Sungura.
***
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MKURUGENZI Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group ambayo inasimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Faustine Sungura ameamua kuwapa motisha wafanyakazi wote wa kampuni hiyo kama sehemu ya kuthamini mchango wao.
Amesema motisha hiyo inakwenda sambamba na uhakiki wa wafanyakazi wote wa kampuni hiyo huku akielezea namna ambavyo amefurahishwa na utendaji kazi wa wafanyakazi wote na hasa katika kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli ambaye amefanya mambo makubwa kwa mwaka 2018.
Akizungumza leo ofisini kwake Sungura amesema Desemba 28 mwaka huu wa 2018 amekutana na wafanyakazi wote kwa kada mbalimbali na alitumia sehemu hiyo kuelezea mikakati ya kampuni hiyo ambayo imedhamiria kufanya mambo makubwa.
"Tulipokutana na wafanyakazi kuna mambo mengi ambayo tumeyazungumza.Pia nilitumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya. Rais wetu amefanya mambo makubwa kwa mwaka huu yakiwamo ya kuboresha sekta ya anga, miundombinu kwa upanuzi wa barabara na ujenzi wa madaraja, umeme wa mto Rufiji ,ununuzi wa korosho, elimu bure na mambo mengine mengi ambayo yamefanyika.Hivyo wafanyakazi hawa wamekuwa wakiunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais,"amefafanua.
Ameongeza wafanyakazi wa Uhuru Media Group kwa mwaka huu wa 2018 wamefanya kazi kwa bidii, hivyo ameamua kuwapongeza kwa kuwapa motisha kwani kesho ni Januari moja ni vema wakauanza mwaka vizuri."Kila mfanyakazi aliyeajiriwa na wasioajiriwa lakini wanafanya kazi kwenye vyombo vya habari vya chama tutawapa motisha hiyo.Tutafanya kwa walioko Dar es Salaam na wa mikoani," amesisitiza.
Aidha mbali ya kutoa motisha atatumia nafasi hiyo kufanya uhakiki wa wafanyakazi waliopo kwenye vyombo hivyo na iwapo kutakuwa na wafanyakazi hewa atawabaini."Nataka kumuona kila mfanyakazi uso kwa uso .Rais wetu aliamua kufanya uhakiki kwa watumishi wa Serikali ,nami namuunga mkono kwa kufanya uhakiki wa wafanyakazi wetu."amesema Sungura.
Amesema baada ya uhakiki wa majina ,hatua ya pili itakuwa ni uhakiki wa vyeti vyao vya kitaaluma na mwisho wa siku atatoa taarifa lakini ameeleza nia yake ni kuona wote ambao wanalipwa wawe ni wafanyakazi sahihi na wapo kwenye orodha yake.
Kuhusu mipango yao,amesema kuanzia mwakani wataanza kufanya utafiti utakaochukua muda wa miezi mitatu na lengo ni kufahamu wasomaji wao,wasikilizaji wao na watazamaji wao wanataka nini.Pia Februari mwaka 2019 watafanya 'uzinduzi laini' wa vyombo vyao na Aprili 2019 watafanya uzinduzi rasmi na hapo ndio watazungumza malengo na mikakati yao.
Amesema wanao mkakati wa kibiashara wa miaka minne na mkakati wa miaka 10 kwa ajili ya kulishika soko.Pia watajiimarisha kwenye mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wanawafikia wasomaji wengi zaidi kwani utafiti unaonesha nusu ya watu wote duniani wanapata habari kutoka mtandaoni"Hivyo ili mambo yaende lazima mtandaoni nako tujiimarishe na mapema mwakani tutaweka nguvu kubwa katika eneo la mtandaoni kwa kuwa na timu maaluma," amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuwatakia heri ya mwaka mpya wafanyakazi wote wa Uhuru Media Group huku akiwasisitiza waendelee kufanya kazi kwa bidii na kujituma kama ambavyo wamefanya mwaka 2018.
Good News : NJIA RAHISI KABISA YA KUPAKUA APP MPYA YA MALUNDE1 BLOG...
Usikubali kupitwa na habari yoyote..Ili uwe wa kwanza kupata habari na matukio yanayojiri Tanzania na dunia kote tafadhali pakua/ Download App mpya ya Malunde 1 blog ili tukuhabarishe usiku na mchana.
App hii imeboreshwa kukupa vitu roho inapenda...Pia tutakuwa tunakutumia habari zote moja kwa moja kwenye simu yako.
App hii imeboreshwa kukupa vitu roho inapenda...Pia tutakuwa tunakutumia habari zote moja kwa moja kwenye simu yako.
STAND UNITED KUISHTAKI TFF, BIGIRIMANA KUSAJILIWA ALLIANCE FC
Dr. Ellyson Maeja
Uongozi wa klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga umepanga kulishtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na hatua yake ya kumruhusu aliyekuwa mchezaji, Bigirimana Blaise, kusajiliwa na timu ya Alliance FC ya Mwanza.
Mwenyekiti wa Stand United, Dk. Ellyson Maeja, alisema klabu yake bado inatambua mchezaji huyo wana mkataba naye, hivyo hatua ya TFF kumwidhinisha Alliance wao wametafsiri kama uonevu.
“Tunasikitishwa na kitendo cha TFF kumruhusu Bigirimana kuitumikia Alliance wakati Stand United tayari imewasilisha malalamiko, nasisitiza kwamba sisi hatujampa barua ya kumruhusu kuondoka.
“Kwa kawaida na jinsi mfumo ulivyo mchezaji haruhusiwi kusajiliwa na timu nyingine, lazima kwanza aandikiwe barua na uongozi wa kule alikokuwa anachezea awali na wenye mamlaka ya kutoa barua ya ruhusa ni kiongozi wa TFF au kiongozi wa timu yake ya kwanza?” alihoji Dk. Maeja.
Bigirimana alikuwa sehemu ya kikosi cha Alliance ambacho kililazimishwa sare ya bao 1-1 na Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Katika mchezo huo uliopigwa Ijumaa iliyopita, Alliance FC ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya 24 lililofungwa na Dickson Ambundo kabla ya Musa Hafidh kuisawazishia Stand United dakika ya 89.
Sam Bahari - Shinyanga
MANARA AWAINGIZA YANGA MTEGONI
Msemaji wa Mabingwa Watetezi, Klabu ya Simba, Haji Manara amehoji Mamlaka ya mapato Tanzania juu utaratibu wa watani zao wa jadi kuhusu kuchangisha kwa ajili ya klabu yao na kuuliza kama utaratibu huo ni sahihi.
Manara amehoji iwapo kama Klabu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara kama inalipia kodi katika Mamlaka hiyo huku akisistiza kwamba hata kama ukweli ukiwa mchungu kiasi gani lazima usemwe.
"TRA nakumbuka mlienda katika kanisa la Mchungaji Kakobe kufuatilia ile michango na zile sadaka za waumini, Vipi kwa hawa wanaochangisha kila uchwao? wana mashine za EFD? wanalipia kodi za hizi Rambirambi za kujitakia?", ameandika Manara.
Katika kusisitiza kauli yake, Manara amesema "Nategemea 'soon' (mapema) wahusika watatoa maelekezo sahihi ya huu utamaduni unaotufedhehesha Watanzania na ambao ukiachwa unaweza kusababisha kizungumkuti cha kukokotoa hesabu".
ZITTO KABWE AANIKA ORODHA YA VITABU 49 ALIVYOSOMA MWAKA 2018
Tangu Mwaka 2012 nimekuwa naorodhesha vitabu nilivyosoma katika mwaka. Si vitabu vyote huviweka hapa kwani vingine huwa nasoma na kuviacha njiani ama kutopendezwa navyo au kwa kusahau tu.
Vitabu vingine huwa vitabu rejea na huvirudia kwa ajili ya mafunzo ili kufanya maamuzi Fulani Fulani au kwa ajili ya ibada (kwa mfano Quran) au kwa sababu nyenginezo. Nafurahi kuwa hivi sasa kwenye mitandao duniani kote watu wamekuwa wakiorodhesha vitabu ili kujengana katika utamaduni wa kusoma. Barack Obama yeye alianza kuweka orodha yake mwaka 2015 na tayari ameshaweka orodha ya mwaka huu. Obama pia huweka orodha ya muziki aliyopenda mwaka huo. Inavutia.
Mwaka huu nimesoma vitabu 49 (kutoka vitabu 36 + 3 vya mwaka 2017). Wakati natoa orodha yangu 23/12/2017 nilikuwa bado nasoma riwaya za Jumba Maro ya Ally Saleh na The Feast of the Goat cha Mario Vargos Llosa ambazo nilizimaliza nikiwa Maputo, Msumbiji.
Pia niliweza kuongeza Simulizi iitwayo Zeitoun ya Dave Eggers kuhusu kimbunga cha Katrina huko New Orleans, Marekani. Hii ni simulizi ya wahamiaji kutoka Syria walivyoshiriki kuokoa makumi ya watu kutoka kwenye maafa ya Hurricane Katrina.
Mwaka 2018 nimesoma mchanyato kidogo kuliko mwaka 2017 ambapo dhima (themes) kadhaa ziliniongoza. Hata hivyo bado njaa yangu ya kuwasoma madikteta duniani iliendelea kuniongoza kwa lengo la kupata ufahamu na maarifa ya namna ya kuchangia katika kuzuia nchi yetu kuangukia kwenye utawala wa Imla. Pia nilijaribu kutafuta majawabu ya changamoto hizo. Kwenye dhima hiyo nilisoma:
- The Death of Democracy: Hitler’s Rise to Power
Benjamin C Hett
- The Plots Against Hitler
Danny Orbach
- Franco: Anatomy of a Dictator
Enrique Moradiellos
1 The New Sultan: Erdogan and the Crisis of Modern Turkey
Oner Cagaptey
- How Democracies Die
D Ziblatt and S Levitsky
Kama nilivyopata kusema, ninapenda na kujivunia sana historia ya ukombozi dhidi ya ukoloni barani Afrika na haswa Ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Mwaka huu niliongeza maarifa katika eneo hilo kwa kusoma sio tu habari nzuri za vyama vya ukombozi bali pia baadhi ya makosa waliyofanya viongozi wetu. SWAPO Captive kilichoandikwa na Bwana Angula ni simulizi muhimu sana kusoma ili kuona namna baadhi ya watu walivyoonewa kwenye harakati za ukombozi. Kwa jina la ukombozi watu huonewa, huteswa na hata huuwawa. Pia nilisoma kuhusu mashujaa wa ukombozi na athari kwa familia zao. Katika dhima hii ya Ukombozi nilisoma:
- Cuito Cuanavale: 12 Months of War That Transformed a Continent
Fred Bridgland
- Africa Tomorrow
Edem Kadjo
- Umkontho we Sizwe: The ANC Armed Struggle
Thula Simpson
- Mozambique: Sowing the Seeds of Revolution
Samora Machel
- 491 Days
Winnie Mandela
- Thabo Mbeki
Adekeye Adebajo
- Umkontho we Sizwe
Janet Cherry
- Chris Hani
Hugh Macmillan
- Being Chris Hani’s Daughter
Lindiwe Hani and Melinda Ferguson
- SWAPO Captive: A Comrade’s Experience of Betrayal and Torture
Oiva Angula
Pia nilisoma vitabu vya hali ya sasa ya Afrika Kusini baada ya ukombozi:
- No Longer Whispering to Power: The Story of Thuli Madonsela
Thandine Gqubule
- How to Steal A City: The Battle for Nelson Mandela Bay, An Inside Account
Crispian Olver
- How to Steal A Country? State Capture and Hope for the Future in South Africa
Robin Renwick
- Coalition Country: South Africa After the ANC
Leon Schreiber
Kama Mtanzania ninayejiandaa kwa majukumu muhimu ya kitaifa nimekuwa nikipenda kupata maarifa Zaidi kuhusu Historia ya Zanzibar. Mwaka 2018 niliongeza maarifa kwa kusoma vitabu kadhaa ikiwemo:
- The Threat of Liberation: Imperialism and Revolution in Zanzibar
Amrit Wilson
- Social Memory, Silenced Voices and Political Struggle: Remembering the Revolution in Zanzibar.
(Ed) W. Cunningham and M. Fouere
Vitabu vinavyofuata ni mchanyato wa riwaya, historia za watu na mataifa mengine, mafunzo ya uchumi na kadhalika. Vitabu vinavyohusu Marekani na utawala wao mpya chini ya Trump ni kwa lengo la kujifunza nini kinaendelea huko. Kitabu cha Deng Xiaoping nilipewa na ndugu yangu Harith Ghassany katika mjadala wa kisomi wa kutafuta modeli sahihi ya kimaendeleo kwa nchi zetu za Afrika.
- Pakistan: Personal Story
Imran Khan
- Making Africa Work: A Handbook for Economic Success
Gregg Mills, O Obasanjo, et al
- Sidetracked
Henning Mankell
- In Praise of Blood: The Crimes of Rwandan Patriotic Front
Judi Rever
- Thomas Sankara Speaks
Thomas Sankara
- A Higher Loyalty
James Comey
- State Secrets: Deathly High Stakes in the Corridors of Power
Quintin Jardine
- Deng Xiaoping and The Transformation of China
Ezra F Vogel
- Gorbachev: His Life and Times
William Taubman
- Tell Tale
Jeffrey Archer
- The Growth Delusion
David Pilling
- CTRL ALT DELETE: How Politics and The Media Crashed Our Democracy
Tom Baldwin
- Unhinged: An Insider’s Account of The Trump White House
Omarosa Manigault
- Fire and Fury: Inside The Trump White House
Michael Wolf
- Why The Dutch are Different
Ben Coates
- The French Revolution: What Went Wrong
Stephen Clarke
- An Extra Ordinary Life: A Passion for Service
V J Mwanga
- Uwajibikaji Ndani ya Kalamu Isiyokuwa na Wino
Ludovich Utouh
- Betting the House: Inside Story of the 2017 Elections
Tim Ross and Tom McTaguwe
- In Defence of Bolsheviks
Max Shachtman
- The Future That Works: Selected Writings of A M Babu
(Ed) Salma Babu and Amrit Wilson
- Our Commonwealth: The Return of Public Ownership in USA
Thomas Hanna
- Democracy, Direct Action and Socialism: A Debate of Fundamentals
Michael Foot and Sean M
Mwaka huu ukiwa unaelekea ukingoni, Wachapishaji wa Vitabu Mkuki na Nyota Publishers walichapisha upya vitabu vya harakati za Willy Gamba, mpelelezi maarufu barani Afrika. Rafiki yangu katika kusoma vitabu Fadhy Mtanga (ambaye pia ni adui yangu kwenye soka – maana yeye ni shabiki mandazi wa Manchester United FC na mimi shabiki wa mabingwa watarajiwa Liverpool FC) alininunulia vitabu vyote 4 vya Mzee Elvis Musiba. Nilikuwa na muda wa kutosha na kuvisoma vyote bila kuweka chini. Namshukuru sana Fadhy kwa zawadi yake murua kabisa. Vitabu hivi ni:
- Kikosi Cha Kisasi
A E Musiba
- Njama
A E Musiba
- Kufa na Kupona
A E Musiba
- Hofu
A E Musiba
Kitabu changu cha mwisho mwaka 2018 ni :
- Dear Ijeawele OR A Feminist Manifesto in 15 Suggestions
Chimamanda Adichie
Vitabu 3 vilivyonigusa sana
The Death of Democracy: Hitler’s rise to power cha Benjamin Hett kilinigusa sana kutokana na namna wanasiasa wanavyoweza kufanya makosa yenye kudidimiza nchi kwa sababu tu ya kulinda madaraka. Katika kitabu hiki somo kubwa ni namna Wabunge wa vyama vyote vya Siasa walivyomruhusu Adolf Hitler kutunga sheria inayompa mamlaka makubwa wakiamini kuwa Hitler ana nia njema na atawalinda.
Wabunge wa Chama cha SDP ndio pekee walikataa, walizomewa, kuzodolewa na hata kuuwawa. Wengine walikimbilia uhamishoni. Ndani ya miezi michache, hata wale waliomwunga mkono Hitler walishughulikiwa na Taifa la Ujerumani likaingia kwenye taharuki kubwa na hatimaye vita vya pili vya dunia.
Waliompa madaraka Hitler waliamini kuwa watamdhibiti. Hawakuweza. Historia kama hii ipo lakini wanaadam hatujifunzi tunarudia makossa hayo kila wakati katika nchi mbalimbali duniani.
How Democracies Die cha Ziblatt na Levitsky kilinigusa sana kwa kuwa kinatoa majawabu ya changamoto za demokrasia kuanguka. Licha ya kwamba ni kitabu maalumu kwa muktadha wa nchi ya Marekani, kitabu hiki nilicholetewa na rafiki yangu Rakesh Rajani, kinatazama mifano ya nchi mbalimbali duniani kama Colombia na njia walizotumia kuhami demokrasia (walitumia sana Bunge na Mahakama), Venezuela (jinsi mgomo wa vyama vya upinzani kutoshiriki chaguzi ulivyotoa nafasi ubwete kwa chama tawala) na hata Ujerumani ambayo hali yake nimeeleza hapo awali.
Somo kubwa kabisa kutoka kitabu hiki ni kwamba ni lazima wadau wote wa demokrasia kushirikiana pamoja kupambana na udikteta bila kujali tofauti ndogo ndogo au kubwa kubwa miongoni mwao. Bila ushirikiano dikteta husaga saga kila mmoja. Ni Kitabu nashauri kila mwana demokrasia akisome.
Dear Ijeawele Or A Feminist Manifesto in 15 Suggestions cha Chimamanda Adichie ni kitabu kidogo sana kwa idadi ya kurasa. Kwa hakika ni barua ambayo Chimamanda kamwandikia rafikiye ambaye amepata mtoto wa kike na anamshauri amkuze vipi mtoto huyu. Kijitabu hiki kimenigusa kwa sababu kinatoa changamoto kadhaa kwa sisi wanaume katika malezi.
Kuna mambo ambayo tunafanya tunaona kama ni msaada kumbe inapaswa kuwa wajibu kwa familia. Kwa mfano, mara nyingi husikia wanaume tukisema ‘leo nafanya kazi ya kulea mke wangu kasafiri’ ama kwa kimombo ‘baby-sitting’. Chimamanda anatuambia hapa, Baba mtoto hafanyi ‘baby-sitting’ bali anatimiza wajibu wake kama baba. Pia kinachoitwa ‘gender roles’ kwenye nyumba zetu kiasi kwamba tunazuia watoto wa kike kukua na kukuza vipawa vyao vyote.
Nashauri wenye watoto wa kike wasome kijitabu hiki, wababa na wamama kwani kinaweza kuchangia kubadili mtazamo wako wa namna tunalea watoto wetu wa kike. Mapendekezo 15 ya Chimamanda unaweza usiyakubali yote lakini yana mafunzo mengi ambayo yanaweza kukufaa kwenye malezi ya mabinti zetu.
Heri ya Mwaka mpya 2019
Zitto Kabwe
Dar es Salaam
30/12/2018
WENYE MIZANI FEKI WAENDELEA KUBANWA
Katika kuhakikisha kwamba mnunuzi wa bidhaa hapunjwi, Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), wameendelea kufanya ukaguzi wa mizani zinazotumika sehemu tofauti hasa kwa wauzaji wa zao la korosho.
Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kubaini mizani zisizo na viwango ambazo hazitoi kipimo kinachostahili.
WMA ilitembelea baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika ili kushuhudia hali halisi ya upimaji korosho za wakulima.
Meneja wa WMA, mkoa wa Pwani, Evarist Masengo, alisema katika kuhakikisha wakulima wanauza mazao yao kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na wakala huo, mizani 109 zimehakikiwa na kupigwa chapa ya Serikali.
Alisema mkoa wa Pwani una jumla ya vyama vya msingi (AMCOS) 95, ambavyo vinapatikana katika wilaya saba.
Wilaya na idadi ya vyama kwenye mabano ni Mkuranga (39), Kibaha (8), Bagamoyo (3), Chalinze (3), Kisarawe (2), Mafia (1), Rufi ji (13) na Kibiti (26).
Masengo alisema kutokana na elimu ambayo hutolewa na WMA kwa wakulima wa korosho na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kabla ya msimu, imesaidia kujua matumizi sahihi ya mizani.
Hatua hiyo imesaidia kupungua kwa tofauti ya uzito wa korosho unaotoka katika chama cha msingi na uzito unaopimwa kwenye ghala.
Pia, Masengo aliongeza kuwa hivi sasa wakala wa vipimo katika mkoa wa Pwani, unafanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye mizani inayopatikana kwenye vyama vya msingi na ile ya maghala makuu ili kujiridhisha kama walivyohakiki na kuziruhusu, zinapima kwa usahihi.
“Nawapongeza vyama vya msingi, wamejitahidi mizani nyingi tunakopita tunakuta ni sahihi na pale tunapogundua dosari ndogo ndogo zinafanyiwa marekebisho mara moja ili mkulima aendelee kupata faida ya jasho lake la kulima korosho,”alisema Masengo.
Kwa Mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340, Wakala wa Vipimo ndiyo yenye jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika au vinavyotarajiwa kutumika kufanyia biashara kwa lengo la kumlinda muuzaji na mnunuzi.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Stella Kahwa kutoka WMA Makao Makuu, alipongeza juhudi zinazofanywa na ofi si ya wakala wa vipimo mkoa wa Pwani.
RC MWANRI AIAGIZA BODI YA PAMBA KUNUNUA PAMBA YA WAKULIMA
Na Tiganya Vincet
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagiza Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuhakikisha inanunua pamba iliyobaki Daraja B (fifi) ya wakulima wa Urambo ili kutowakatisha tamaa ya kuendelea na kilimo hicho.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kufuatia malalamiko kutoka kwa wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Itengamatwi wilayani Urambo juu ya uwepo wa pamba ambao hadi hivi sasa iko katika maghala na wakulima hawajalipwa fedha.
Aliwataka wakulima kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa jitihada zinaendelea ili kuhakikisha pamba yao fifi(daraja B) ambayo hadi hivi sasa bado iko katika maghali ya kuhifadhi mazao inanunuliwa na Bodi ya Pamba Tanzana baada ya wanunuzi wa awali kusimamisha ununuzi na kuzima mashine.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wakulima kuzingatia kanuni 10 za kilimo cha zao hilo ili kuepuka kuzalisha pamba Daraja B ambalo ndio wakati mwingine linakuwa kigezo cha wanunuzi kuwapa bei mbaya na wakati mwingine kukataa kununua pamba yao.
Alisema azimo la Mkoa wa Tabora katika msimu wa kilimo cha zao ujao ni kila mkulima ni lazima azingatite kanuni kumi za zao hilo ikiwemo kuvuna kwa wakati na kuhifadhi katika hali ya usafi.
Mwanri alisema hatua hiyo itasaidia kulinda ubora wa zao hilo na kumsaidia mkulima kupata Daraja A na kulipwa bei ya juu itakayompa fedha nyingi ambazo zitasaidia kuboresha maisha yake.
Kwa upande wa Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Modest Kaijage aliwahakikishia wakulima wa pamba wilayani Urambo ambao wana pamba fifi(Daraja B) kuwa Bodi imeamua kuinunua na itawalipa malipo yao.
Alisema Mkurugenzi Mkuu wa TCB amesema kuwa wanafanya utaratibu ili waweze kununua pamba iliyobaki ambapo wao ndio wataifanyia uchambuzi kwa ajili ya msimu ujao.
Awali baadhi ya wakulima walisema kuwa walipokuwa wakihamasishwa kulima pamba na wakati wa ununuzi waliambiwa kuwa pamba ina madaraja mawili lakini wakati wa mauzo pamba yao daraja B haikununuliwa na bado ipo katika maghali jambo linalowakatisha tamaa kuendelea na kilimo hicho.
TETESI ZA SOKA ULAYA JUMATATU DEC, 31 2018
Kiungo wa kati wa Real Madrid Isco, 26, amepuuzilia uwezekano wake wa kuhamia klabu ya Chelsea ya England. Amesema hataondoka Bernabeu wakati wa kipindi cha kuhama wachezaji Januari. (Deportes Cuatro, kupitia Metro)
Manchester City wanamfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Real Betis Junior Firpo lakini wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Real Madrid ambao pia wanataka saini ya mchezaji huyo mwenye miaka 22. (Mirror)
Mshambuliaji wa Liverpool Dominic Solanke, 21, amefanyiwa vipimo vya matibabu katika klabu ya Crystal Palace huku akikaribia kuhamia Selhurst Park kwa mkopo. (Mail)
Winga wa klabu ya Lille ya Ufraansa Nicolas Pepe mwenye miaka 23 ambaye amehusishwa na Arsenal, Barcelona na Manchester City, anaonekana kuwa tayari kuhama mwisho wa msimu. (Le Voix du Nord, kupitia Star)Dominic Solanke alichezea timu ya taifa ya England mara ya kwanza Novemba 2017 mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil.
Kiungo wa kati wa Chelsea Tiemoue Bakayoko, 24, amesema yuko radhi kusalia AC Milan hata baada ya kipindi chake cha kuwa na klabu hiyo ya Italia kwa mkopo wa msimu mmoja kukamilima mwisho wa msimu. (MilanNews, kupitia Mail)Bakayoko alichezea Chelsea mechi 43 msimu uliopita
West Brom wanakaribia kutia saini mkataba na beki wa Everton Mason Holgate, 22, kwa mkopo Januari. (Express na Star)
Klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani imejitosa kwenye mbio za kutaka kumnunua winga wa Chelsea mwenye miaka 18 Callum Hudson-Odoi. (Kicker - German)Callum Hudson-Odoi alijiunga na Chelsea mwaka 2007
Mchezaji anayenyatiwa sana na Liverpool ambaye kwa sasa Borussia Dortmund Christian Pulisic, 20, anaonekana kukaribia kujiunga na Chelsea kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na msambuliaji wa zamani wa Marekani Eddie Johnson kwenye mitandao ya kijamii. (Calciomercato)
Middlesbrough wanatumai wataweza kumsaini kiungo wa kati wa Huddersfield Rajiv van La Parra, 27, kwa mkopo kukiwa na uwezekano wa kumchukua kwa mkataba wa kudumu baadaye mwisho wa msimu. (Yorkshire Post)Christian Pulisic
Meneja Brendan Rodgers amesema Celtic wana kazi kubwa ya kufanya sokoni Januari kuwanunua wachezaji wapya. (Irish Times kupitia Celtic TV)
Meneja msaidizi wa timu ya taifa ya England Steve Holland amesema timu hiyo haikujiandaa na kucheza nusufainali yao ya Kombe la Dunia Urusi ilivyofaa. (Telegraph)
BWANA HARUSI AFARIKI GHAFLA KANISANI AKISUBIRI KUFUNGA NDOA
Sherehe ya harusi iliyokuwa ifanyike juzi jioni katika Kanisa la Nabii wa Utukufu wa Bwana lilipo Olmatejoo, Kata ya Sakina jijini Arusha na kwenye ukumbi wa Sariko Olasiti Garden, iligeuka msiba baada ya bwana harusi kufariki dunia ghafla akiwa kanisani.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11 jioni katika kanisa hilo ambapo bwana harusi huyo, Heaven Makupa (47) alikuwa kanisani tangu saa saba mchana akisubiri kufunga ndoa na Jane Kimaro.
Hata hivyo, wakati sherehe, nderemo na vifijo vikiendelea vikiongozwa na kikundi cha matarumbeta nje ya kanisa huku bibi harusi akiingia kanisani, Heaven alianza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.
Kutokana na hali hiyo alikimbizwa Hospitali ya St Elizabeth, lakini alifikishwa akiwa tayari amefariki na mwili wake kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe na kiongozi wa kanisa hilo, Nabii Peter Alayce na tayari taratibu zote zilikuwa zimekamilika tangu mchana alipofika bwana harusi na ujumbe wake.
Wakati kifo hicho kinatokea mamia ya watu walikuwa tayari wamefika katika ukumbi wa Sariko Olasiti Garden kuwasubiri maharusi hao ili kuendelea na sherehe.
Mmoja wa wageni waalikwa, Juliana Mosha alisema kabla ya kifo hicho hakukuwa na taarifa yoyote ya kuugua kwa bwana harusi na walishikiri naye vikao vya harusi hadi dakika ya mwisho. “Hili ni jambo la miujiza, hatujui kilichotokea nadhani hii ni kazi ya Mungu,” alisema Juliana.
Alisema baada ya taarifa kufikishwa ukumbini juu ya msiba huo, watu walianza kutawanyika na kurejea majumbani.
Na Mussa Juma,Mwananchi
RADI YAUA,KUJERUHI TUNDURU
Mkazi wa Kijiji cha Nambalapi mashambani, Kata ya Masonya, wilayani Tunduru, Awetu Adam (33), amefariki dunia baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na upepo mkali akiwa shambani.
Mvua hiyo iliyonyesha Desemba 29, mwaka huu kwa saa nne kuanzia saa 9 hadi 12 jioni imeripotiwa pia kuezua na kubomoa zaidi ya nyumba 250 za wananchi wa tarafa hiyo.
Pia imeharibu na kuvunja miundombinu ya Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kung`oa baadhi ya nguzo na kusababisha ukosefu wa nishati hiyo katika baadhi ya maeneo ya mji huo.
Mbali na tukio la kifo, mtoto wa miaka miwili Bakari Said, alijeruhiwa kwa kupigwa na radi wakati akiwa amebebwa mgongoni na mama yake ambaye alikufa kwa kupigwa na radi.
Diwani wa Kata ya Mchangani, Haillu Hemed Mussa, alisema jumla ya nyumba 141, madarasa matano na ofisi za walimu katika Shule ya Msingi Mchangani, zimezuliwa.
Alifafanua kuwa pamoja na uharibifu huo pia kata yake iliripoti kujeruhiwa wananchi watatu waliotambuliwa kama, Kawale Bakari, Alli Ambe na Shekhe Mohamed Salum, ambao walikimbizwa Hospitali ya Serikali ya Wilaya kwa ajili ya matibabu.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Majengo, Abdalah Rajabu, alisema kuwa tukio la mvua hiyo limesababisha kuezuliwa kwa mapaa ya maghala mawili ya kuhifadhia korosho mali ya Chama Kikuu cha Wakulima (TAMCU) na kulowesha tani 536 za korosho, mali ya serikali.
Alisema pamoja na madhara hayo pia upepo na mvua hizo ziliezua nyumba 13 mali ya wakazi wa eneo la kata yake.
Diwani Rashid Mkwawa kutoka Kata ya Nanjoka, alisema kuwa jumla ya wakazi 11 walikosa makazi kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua hizo.
Taarifa zilizotolewa na maofisa tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, zinaeleza kuwa majeruhi wote wanaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na tayari amewaagiza viongozi wa serikali za vijiji kuzunguka katika maeneo yao na kufanya tathmini ili kubaini hali halisi ya uharibifu huo.