Tuesday, 20 June 2023

WATUMISHI OFISI YA MSAJILI WA HAZINA WAHIMIZWA WELEDI KAZINI

...

Na Mwandishi Maalumu

WATUMISHI katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) wamehimizwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuhakikisha kila mmoja anatoa mchango wake katika kuleta tija kwa Ofisi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma leo jijini Dar es Salaam.

Mauki alisema wajibu na weledi huo unatokana na ukweli kuwa ofisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kusimamia uwekezaji mkubwa wa serikali wenye thamani ya Sh trilioni 70 kwenye taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa.

Katika kuadhimisha wiki hiyo, viongozi na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wameungana katika kuhudumia wateja na wadau wa ofisi kwa kutenga eneo maalumu katika makao makuu ya ofisi, Mtaa wa Mirambo, Dar es Salaam.

Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu inayosema; “Kufanikiwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika Kunahitaji Usimamizi wa Utumishi wa Umma Wenye Mtazamo wa Kikanda” yanayotarajiwa kufikia tamati Ijumaa wiki hii, Mauki aliwataka watumishi hao kushughulikia malalamiko ya wadau na wateja wanaofuata huduma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina na kutunza kumbukumbu ya namna wateja wa ndani na wa nje wanavyohudumiwa huku wakihakikisha kuwa wanatatua changamoto zao.

Aidha, Mauki alisema katika maadhimisho hayo, ofisi imejikita katika maeneo matatu ambayo ni viongozi wa Idara na Vitengo kufanya vikao na watumishi wanaowasimamia ili kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuiwezesha ofisi kufikia malengo yake kwa ufanisi mkubwa.

Alisema katika kuhitimisha maadhimisho hayo Juni 23, 2023 watumishi wote watatembelea Kituo cha Wazee cha Nunge kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam kwa lengo la kufanya shughuli za kijamii na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wazee hao.

Kutokana na umuhimu wa wiki ya utumishi wa umma, Mauki aliwasisitiza watumishi kutoa huduma sawa kwa wateja na wadau wote wa ndani na nje ya ofisi.

“Ninawakaribisha wateja na wadau wote wa ofisi kufika katika Ofisi yetu ya Msajili wa Hazina kuja kupata huduma wanazohitaji kutoka kwetu. Karibuni sana,” alisema.

Maadhimisho haya yanayofanyika kati ya Juni 16 na 23 ya kila mwaka, ni moja ya matukio katika kalenda ya Umoja wa Afirika (AU) ambapo nchi wanachama huadhimisha kwa kufanya maonesho ya kazi mbalimbali na kongamano kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma. Kwa Tanzania, yanaratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger