Pamba safi ikiwa kwenye kituo cha pamba ununuzi kwaajili ya kununuliwa
Mwandishi wa Makala haya Daniel Limbe akishuhudia ubora wa pamba inayo nunuliwa kwenye Amcos ya Chato
Mwonekano wa zao la pamba likiwa bado shambani
**
Na Daniel Limbe,Chato
KENGE ni mnyama anayefanana na mamba mdogo kwa umbile, na hupenda kuishi nchi kavu pamoja na kwenye madimbwi ya maji, huku mafuta yake yakitajwa kuwa matibabu ya masikio.
Nikutokana na wataalamu wa tiba asilia kuamini kuwa mafuta ya kenge yanatibu ugonjwa wa sikio linalouma au kutokwa usaha.
Mbali na kuwa ni tiba ya ugonjwa wa sikio,Baadhi ya wakulima wa zao la pamba wilayani ya Chato mkoa wa Geita, wanasema kuwa mafuta ya Kenge ni muhimu katika kuongeza uzito wa zao hilo na hivyo kuwaongezea kipato zaidi.
IMANI POTOFU
Inaelezwa kuwa kuchanganya mafuta ya Kenge kwenye zao la pamba ni imani potofu na ni kichocheo cha kuporomoka kwa bei na thamani yake ndani na nje ya nchi.
Uchunguzi umebaini uwepo wa mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya wakulima wa pamba kwa kuichanganya na mafuta ya Kenge wakiamini kuwa huongeza uzito wakati wa kuuza zao hilo.
Baadhi ya wakulima wanaamini kuwa wakitumia mafuta ya kenge (Uru)kunyunyizia pamba safi iliyokwisha vunwa shambani kabla ya kufikishwa kwenye masoko ili kuuzwa huongeza uzito kwenye zao hilo kwa lengo la kujipatia fedha nyingi.
Mwandishi wa makala haya amefanikiwa kuzungumza na familia ya Nyangeta Masatu, ambaye ni mkulima wa pamba kwa zaidi ya miaka 34 bila shaka anakiri kuwepo kwa tabia hiyo kwa baadhi ya wakulima wa pamba.
Anasema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuamini kuwa mafuta hayo huongeza uzito wa pamba, hivyo kumsaidia mkulima kupata kilo nyingi anapouza pamba yake.
Anataja namna ambavyo mafuta hayo hutumika na kusema kuwa hupakwa kwenye pindo za shuka (nguo) inayotumika kuuzia pamba kabla ya zao hilo kupandishwa kwenye mzani wa kupimia.
Masatu anasema kuwa njia nyingine ni kupaka mafuta ya kenge kwenye jiwe dogo ambalo huwekwa ndani ya kifungashio kilichobeba pamba hiyo.
Ernest Philipo, mkazi wa Nyarubungo anasema uharifu wa kutumia mafuta ya kenge aliushuhudia mwaka 1976 baada ya rafiki yake kutumia wakati wa msimu wa mauzo ya pamba.
Anasema pamoja na kuwa yeye hakuwahi kutumia mafuta hayo ila anatambua kuwa baadhi ya wakulima wa zao hilo hutumia mafuta hayo kujiongezea kipato hasa wakulima waliopo maeneo ya ukanda wa ziwa viktoria.
Zacharia Kapandekado, mkazi wa kijiji cha Katemwa Muganza, anakiri baadhi ya wakulima kutumia mafuta ya kenge pamoja na maji kuongeza uzito wa pamba.
Anasema vitendo hivyo hufanyika kwa kificho kwa kuwa wanatambua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, huku akidai wanafanya uharifu huo hutokana na kuwa na pamba kidogo ikilinganishwa na wenye pamba nyingi.
MWENYEKITI CCU AELEZA THAMANI YA PAMBA
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika Chato (CCU) Greon Chandika, anasema kuwa zao la pamba lina manufaa makubwa kwa jamii iwapo usimamizi wake utaimalishwa kuanzia ngazi ya familia, kitongoji, kijiji, kata, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Anasema kuwa usimamizi huo unapaswa kuenenda sambamba na miongozo na maelekezo ya serikali katika kuhakikisha elimu zaidi inaongezwa kwa wakulima,kupitia taasisi zake pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Chandika anasema pamba ina faida rukuki iwapo itatunzwa na kuvunwa vizuri kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo hicho kwa kuwa inapovunwa na kuuzwa mkulima huanza kunufaika moja kwa moja kwa kujipatia fedha.
Mbali na mkulima, makampuni nayo huchakata na kutengeneza nyuzi (robota) ambazo huuzwa kwenye soko la dunia na nyingine hubaki nchini kama mali ghafi ya viwanda vya kutengeneza nguo.
Anadai kuwa mbegu ya pamba hukamuliwa mafuta ya kupikia ambayo hupendwa sana na wananchi wengi kutokana na ubora wake huku makapi ya mbegu hizo yakitengenezwa chakula cha mifugo (mashudu) pia hukamuliwa na kutengenezwa sabuni za kufulia na kuoshea vyombo.
Kadhalika magugu ya zao la pamba nayo yakitumika kama kuni za kupikia chakula hasa maeneo ya vijijini, hivyo kusababisha zao hilo kupata umaarufu na kupewa jina la dhahabu nyeupe.
KAULI YA MKAGUZI UBORA WA PAMBA
Ofisa Mkaguzi Ubora wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba(TCB) wilayani Chato mkoani Geita,na Biharamulo mkoani Kagera, Samweli Mdidi, anathibitisha kuwepo kwa uharifu huo kutoka kwa baadhi ya wakulima wenye kuamini kufanikiwa kwa kutumia mafuta hayo.
Licha ya baadhi ya wakulima kuamini hivyo, anasema imani hiyo haina ukweli wowote zaidi ya kusababisha kuozesha pamba.
"Ni kweli kuna hayo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wetu wa pamba...tunaendelea kukagua na kutoa elimu kwa wakulima kuachana na imani hizo potofu kwa kuwa hakuna ukweli wowote wa kilo kuongezeka iwapo mkulima atatumia mafuta ya kenge badala yake ni kuozesha pamba"anasema Mdidi.
Anasema kuwa madhara mengine yanayoweza kutokea kutokana na uchafuzi huo ni kushuka kwa bei ya pamba kutokana na wanunuzi kupata hasara kwa kununua pamba isiyokuwa na ubora pamoja na kushuka thamani ya robota zetu kwenye soko la dunia.
OFISA WANYAMA PORI
Kwa upande wake, Daktari mwandamizi kitengo cha wanyama pori nchini, Dk.Emmanel Macha, anasema kitaalamu hakuna uhusiano wowote kati ya mafuta ya kenge na suala la kuongezeka uzito ndani ya pamba.
"Kwanza itambulike kuwa ili kupata mafuta hayo lazima kenge auawe...mbali na kuwa ni imani potofu zisizo kuwa na ukweli wowote lakini kuna wasiwasi kubwa ya kuwaangamiza wanyama hao wasio na madhara yoyote kwa jamii"anasema Dk. Macha.
"Suala hilo halihitaji hata elimu kubwa...kama wanapakashia mafuta hayo kwenye jiwe halafu uzito umaongezeka kwenye pamba basi watambue kinachokuwa kimeongeza ni jiwe wala siyo mafuta hayo"anasema.
Aidha anawataka wakulima kuachana na imani hizo badala yake walime pamba kwa kuzingatia majira ya msimu wa kilimo, kuzingatia kanuni bora pamoja na kusikiliza na kuzingatia kwa kina ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo hatua itakayo wasaidia kupata tija.
MKURUGENZI TCB
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga, anasema kuwa umaskini wa wakulima wa pamba hausababishwi na ukosefu wa nguvu kazi bali nikutokana na tija ndogo inayotokana na kutokuzingatia kanuni za kilimo bora.
"Wanatumia nguvu nyingi bila maarifa hivyo kuwafanya mara nyingi kulalamikia bei ndogo hali inayosababisha kuuza hata pamba chafu.
"Bila kutatua tatizo la tija ndogo, hata bei ikipanda maradufu, bado umaskini hautaondoka...uzalishaji wa kilo 300 kwa ekari ni mdogo sana"anasema Mtunga.
"Wakulima wengi wa pamba wamekuwa wakishindwa kuwapa ushirikiano wakaguzi wanapobaini kuwepo kwa pamba chafu katika vituo vya kuuzia pamba kwa kuhofia kutouza pamba yao...pasipo kujua kuwa pamba chafu ndiyo chanzo kikuu kinachofanya bei ya pamba kuporomoka kwenye soko la dunia"anasema.
Mtunga anawataka wakulima kutoa ushirikiano kwa wadau wa pamba na serikali ili kuwa na uzalishaji wa pamba wenye tija lakini pia wakulima wajiunge kwenye ushirika ili kuleta mabadiliko chanya badala ya kuendelea kuwa walalamikaji.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye tovuti ya TCB, Zao la Pamba hulimwa katika mikoa 17 ya Tanzania bara,na kwamba hutengenezwa nyuzi (robota) na kuuzwa kwenye soko la dunia, ambapo serikali hujipatia fedha za kigeni na kuchangia uchumi wa taifa.
Inaelezwa kuwa mkoa wa Singida, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita, Tabora na Kigoma inazalisha aslimia 90 ya pamba mbegu yote inayolimwa nchini.
Huku aslimia 10 ya pamba mbegu ikilimwa na mikoa ya Kagera,Dodoma, Katavi, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Manyara na Pwani.
Miongoni mwa mikakati ya serikali ni kukuza uzalishaji wa pamba kutoka wastani wa tani 300,000 hadi kufikia tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2025.
Hatua hiyo inakuja huku baadhi ya mataifa mengi duniani ikiwemo nchi ya Misri huzalisha kilo 2,000 kwa ekari tofauti na Tanzania ambapo inazalisha kilo 300.
Tovuti hiyo inaonyesha kuwa tangu uzalishaji wa pamba uanze hapa nchini mwanzoni mwa karne ya 20, uzalishaji wa juu kabisa ulifikiwa msimu wa 2005/2006 ambapo jumla ya tani 376,000 sawa na robota 700,000 zilizalishwa.
WAZIRI WA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anasema ili kuinua kilimo cha pamba nchini,serikali imeamua kuwaondolea wakulima makato ya fedha ya dawa na mbegu walizokopeshwa wakati wa kilimo.
"Pesa hizo wakulima walitakiwa kurejesha wakati huu wa msimu wa 2022/23 wa ununuzi wa zao la pamba ambao umeshaanza nchi nzima"anasema Bashe.
Bashe anawataka wakulima wa pamba kutokubali kuibiwa na wanunuzi, na kwamba bei watakayoikuta kwenye vituo vya kununulia pamba haitakiwi mkulima kukatwa hata senti kwa madai serikali imetoa ruzuku kwa zao hilo.
Anasema Chato ni moja kati ya wilaya zilizokuwa zinalima pamba kwa wingi lakini zao hilo liliporomoka kutokana na sababu mbalimbali hali iliyosababisha kiwanda cha kuchakata pamba cha Chato Co-operative Union (CCU)kufa.
PAMBA YOTE KUNUNULIWA
Mwenyekiti wa Chama cha wakulima wa Pamba nchini (TCA) Boaz Ogolla, anasema kwa msimu wa 2022/23 TCA imejipanga kununua pamba yote itakayozalishwa na wakulima kwa njia ya ushindani kwa kuzingatia mwenendo wa soko la kimataifa la ununuzi wa pamba.
Inaelezwa kuwa mkakati wa serikali kufufua zao la pamba, kuanzia msimu wa mwaka jana 2021/22 na mwaka huu 2022/23 umewezesha serikali kuwapatia wakulima pembejeo ikiwemo mbegu na dawa bure ili kuongeza tija.
NINI KIFANYIKE
Jamii iendelee kuelimishwa kuzingatia kanuni bora 11 za kilimo cha pamba kupitia maofisa ugani vijijini,ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata pembejeo mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Maofisa ugani kwa kushirikiana na ofisa maendeleo ya jamii vijijini wasaidie kuelimisha wakulima kujiepusha na imani potofu za kutumia mafuta ya kenge kuongeza uzito wa pamba.
Bodi ya pamba waendelee kukagua ubora wa pamba kabla na baada ya kununuliwa hatua itakayosaidia kusafirisha pamba nyuzi zenye ubora unaotakiwa kwenye soko la dunia.
Wananchi wahamasishwe kuendelea kulima pamba, kutokana na kuwa ni zao la biashara lenye manufaa rukuki kwa manufaa ya kaya na serikali.
Serikali iweke ruzuku kwenye zao la pamba hasa kipindi bei inapo shuka kwenye soko la dunia, hali itakayo wavutia wakulima wengi kuendelea na kilimo hicho.
0 comments:
Post a Comment