Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF , Lulu Ng'wanakilala
Meneja Mwandamizi wa Programu kutoka LSF, Deo Bwire
Na Mwandishi wetu
UPATIKANAJI wa haki kwa wote ni jambo linalotarajiwa na kila mtu bila kujali mazingira aliyopo kwa wakati huo. Ndio maana hakuna mtu anayependa kutafuta msaada wa kisheria lakini umuhimu wake hudhihirika pale mtu anapohitaji msaada huo lakini kwa upande mwingine ikawa kama ndoto kwake kupata huduma hiyo ya msaada wa kisheria.
Katika maeneo mengi ya nchini watu wa matabaka mbalimbali hukumbana na changamoto za kisheria ambazo nyingi kati yake hutatuliwa ndani ya muda unaokubalika huku wengine wakipitia mlolongo mrefu wenye matokeo hasi.
Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kuwa mtu anaweza kuwekwa mahabusu na hata kufungwa kabisa kwa kukosa msaada huu wa kisheria.
Lakini Taasisi ya Legal Services Facility (LSF) ilipoanzisha Mpango wake wa Upatikanaji wa Haki miaka 10 iliyopita, ilijipanga kwa kuzingatia kwamba katika nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 60 ambao wengi wao wanaishi vijijini, ni idadi ndogo yenye uwezo wa kupata huduma za msaada wa kisheria.
Kwa maneno mengine ni kwamba Watanzania wengi hawakuwa na sehemu ambazo wanaweza kuwasilisha migogoro yao na kutatuliwa kwa urahisi au hata maeneo ambayo wangeweza kupata fursa ya ufahamu wa kisheria.
Kwa mtu ambaye hajavaa viatu vya watu hawa wa kawaida anaweza asione uchungu kuhusu hali wanayopitia lakini hii inaleta tafsiri kwamba ni kwa namna gani wamepitia changamoto ya muda mrefu kupata msaada wa usaidizi wa kisheria.
Kupitia mfuko wa msaada wa kifedha, LSF imetoa ruzuku kwa mashirika mengi yasiyo ya kiserikali (NGOs) na asasi za kiraia (CSOs) bara na Zanzibar ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria hadi ngazi za chini kabisa kwenye jamii. Lengo ni kuwa na jamii iliyojengwa kwa misingi ya usawa unaozingatia haki.
Kimsingi, lengo mfuko huo limeanzisha dhana ya haki kwa kuweka msingi ambao kila mtu anaweza kupata haki bila kizuizi chochote.
Kazi nyingi zinazofanywa na mashirika yanayoungwa mkono na LSF, zinaonekana kwa urahisi kutokana na ukweli kwamba walengwa ni wanawake, wanaume na watoto tunaowaona kila siku kwenye jamii zetu - ofisini, sokoni, shuleni, mahali pa ibada, na hospitali.
Kuna kundi moja ambalo wengi wao hawana uwezo wa kutoka na kuchangamana na wengine kusaka haki, hao ni wanawake, wanaume na watoto ambao wako mahabusu. Kiuhalisia hili ni kundi linalochukuliwa kama limesahaulika.
Hali hii imetokea kwa miaka iliyopita, lakini kupitia Mpango wa Upatikanaji wa Haki wa LSF, umewapa fursa nyingine ya kupata haki kwani kitendo cha kuwa gerezani si lazima iwe mwisho wa matarajio ya mtu kupata haki.
Miongoni mwa mashirika yanayofanya kazi kwa usaidizi kutoka LSF ni Envirocare. Hili ni shirika binafsi lililosajiliwa mwaka 1993 lisilofanya kazi kibiashara.
Shirika hilo linafanya kazi ya zinazohusu uhifadhi wa mazingira, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na utawala bora.
Shirika la Envirocare lilianza kujihusisha na utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika miaka iliyofuata baada ya kukidhi matakwa ya kisheria.
Shirika hilo liliendelea kuwafikia watoto, wanaume na wanawake ambao hawakuwa na uwezo wa kupata huduma hizo, pia kwa wale waliokuwa katika mahabusu za polisi na magereza yote nchini.
Msukumo wa kutoa kipaumbele kwa watu wanaoshikiliwa katika taasisi kama hizo ulianza mapema mwaka 2000. Hali hii ilitokana na msongamano uliokuwa mkubwa kwenye magereza jambo ambalo limeendelea kuwa changamoto kwa miongo kadhaa nchini.
Baada ya kupata ufadhili kwa mara ya kwanza kutoka LSF mwaka 2012, shirika la Envirocare na Jeshi la Magereza, lilifanya uchunguzi katika mhabusu mbalimbali nchini na kubaini uwepo wa watuhumiwa 4,737 ambao walikuwa ni wengi mara mbili kuliko uwezo wa mahabusu hizo.
Kwa mfano katika gereza la Keko lilikuwa na wafungwa kati ya 1,100 na 1,500 ilihali uwezo wake ni watu 340 pekee hali iliyosababisha mahabusu hao kushikiliwa katika mazingira ambayo si salama wala ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa Envirocare, mahabusu za polisi nazo zilikuwa hivyohivyo na msongamano.
Kimsingi lengo la mradi wa kwanza wa mashirika chini ya ufadhili wa LSF ambao ulifanyika kuanzia 2012 – 2015, ulilenga kupunguza msongamano katika magereza 20 na magereza manne ya watoto.
Pia mradi huo ulilenga kuhakikisha watu wote walioko rumande katika magereza na mahabusu mbalimbali nchini wanapata haki.
Akizungumzia kuhusu mradi huo, Naibu Mkurugenzi wa Envirocare, Catherine Jerome anasema, “Mradi huu ulituwezesha kutambua na kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 88 walioko magerezani; tulisaidia kuongeza uwezo wa kazi kwa maofisa wa polisi 25, mahakimu 25 na wafungwa 50 wa magereza kuhusiana na sheria muhimu, haki za binadamu na uchunguzi.
“Vile vile tulifikia watu wazima 3,961 waliokuwa rumande, kati yao 546 walikuwa wanawake, wanaume 3,415, na watoto 145.
“Kati ya kesi hizo 3,961, kesi 1,284 zilidhaminiwa, 510 waliachiliwa, 484 walibaki rumande na kesi 1,683 ziliendelea.
“Tunafurahi kwamba hadi sasa miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa kutokana na kazi za mradi huu ni pamoja na uanzishwaji wa madawati ya msaada wa kisheria ndani ya magereza, kupunguza msongamano magerezani, kuboreshwa kwa mahusiano kati ya wasaidizi wa kisheria, polisi na mahakimu, kuweka taarifa za kutosha kuhusu takwimu na rekodi nyingi za kazi hiyo.
“Ni muhimu zaidi kutambua kwamba mpango huu pia uliongeza idadi ya vituo vya polisi katika mikoa ambayo mradi ulifika”, anasema.
Matokeo haya yanatokana na mchango wa kipekee na wa moja kwa moja ulitolewa na Mpango wa Upatikanaji wa Haki wa LSF kwa kujumuisha watu ambao mipango mingi huwa haiwalengi licha ya kwamba wanahitaji huduma za msaada wa kisheria.
Mara nyingi inadhaniwa kuwa programu hii inalenga zaidi kuwasaidia wananchi wa kawaida, hata hivyo upatikanaji wa haki ni dhana kamilifu na imekusudiwa kuwafikia wale walio na dhamana ya kutenda haki sawa na wale wanaotarajiwa kunufaika nayo bila kujali hali zao.
Katika awamu ya pili iliyoanza 2017 na inayotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka 2021, Envirocare imekuwa ikifanya kazi ya kupunguza msongamano katika magereza ya mijini kupitia utoaji wa msaada wa kisheria.
Zaidi ya hayo, kazi yake ndani ya kipindi hiki pia inajumuisha kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, na kwamba kuna uratibu na ushirikiano ulioboreshwa kati ya wadau husika katika mfumo wa haki ya jinai.
Katika kutekeleza mzunguko huu wa ruzuku, shirika limesambaza machapisho ya elimu ya sheria na kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 272 kati yao 160 ni maofisa wa polisi na wasimamizi wa magereza 112, na kutoa mafunzo kwa maofisa uhusiano 27.
Hadi sasa, mahabusu 21,841 wamepata usaidizi wa kisheria pamoja na watoto 292.
Katika kipindi ambacho janga la Covid-19 limepamba moto, shirika lilianzisha mfumo wa simu za dharura ambapo watu 3,292 waliendelea kunufaika na huduma za msaada wa kisheria.
Elimu ya msaada wa kisheria ilitolewa kwa ushirikiano wa Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi na Magereza na kufikia jumla ya watu wazima 8,881 na watoto 197. Shirika la Envirocare pia linatumia vipindi vya redio na majukwaa mengine kwa ajili ya kuwafikia watu nchini kote na katika kipindi hiki ambacho awamu ya pili ya ufadhili inakaribia kufikia mwisho tayari watu 35,297 walio mahabusu na magereza wamepata huduma za msaada wa kisheria.
Meneja Mwandamizi wa Programu kutoka LSF, Deo Bwire anasema, "Kujitolea na ubunifu ambao Envirocare wameonyesha katika kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa haki katika mfumo wetu wa kidola, umesaidia kupunguza mateso ya maelfu ya watu nchini ambao wanajikuta wameangukia kwenye kibano cha sheria.
“Haki ni thamani ya wote na tunaendelea kuunga mkono kila mpango adhimu unaolenga kuhakikisha kuna upatikanaji wa kutosha wa huduma za msaada wa kisheria popote nchini bila kujali hali ya mlengwa.
“Mchango mkubwa wa Envirocare kwa ushirikiano wa karibu na wadau wengine ambao umetolewa kwa miaka yote hii, umedhihirisha kuwa programu yetu ina manufaa makubwa na sasa idadi kubwa ya Watanzania wameweza kutoka kwenye kifungo na kupata haki yao ya msingi kama binadamu,” anasema.
LSF inapofikisha miaka 10, matokeo ya mpango huu wa upatikanaji wa haki unaweza kuthibitishwa na washirika wake kama Envirocare ambao wanaendelea kuweka rekodi kila kukicha.
Kazi kubwa ya kupunguza msongamano magereza inawanufaisha wanaume, wanawake na watoto walio mahabusu na magerezani kupata haki bila vikwazo huku pia ikisaidia kuimarisha mfumo wa upatikanaji haki kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment