Friday 26 November 2021

eGA YAZIONYA TAASISI ZA UMMA ZINAZOANZISHA MIFUMO YA TEHAMA BILA IDHINI YA MAMLAKA HIYO

...

Meneja wa Huduma za sheria mamlaka ya Serikali Mtandao[eGa] ACP. Raphael Rutahiwa

Na Faustine Gimu Galafoni, Dodoma.
Mamlaka ya Serikali Mtandao [eGa] imezitaka taasisi za umma zinazoanzisha mifumo ya Tehama bila idhini ya mamlaka hiyo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu zilizoanzishwa na mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa leo Novemba 26,2021 jijini Dodoma na Meneja wa Huduma za sheria mamlaka ya Serikali Mtandao[eGa] ACP. Raphael Rutahiwa wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambapo amesema taasisi zote za Umma zinapotaka kuanzisha mifumo lazima ziwasililiane na Mamlaka hiyo.

“mamlaka inaelekeza taasisi yoyote ya umma isijenge au kuendeleza mradi wa wowote wa TEHAMA bila kupata idhini ya mamlaka,pia inasisitiza kutoa taarifa mara kwa mara kwa mamlaka katika utekelezaji pia sheria inasisitiza kujenga mifumo kwa kutumia wataalam wa ndani”amesema.

Aidha,amesisitiza kutumia wataalam wa ndani katika kuokoa gharama pamoja na kulinda usalama zaidi wa kimfumo.

Pia meneja huyo wa Huduma za sheria eGa ametoa msisitizo kwa taasisi zote za kiserikali kuzingatia sheria Na.10 ya mwaka 2019 ya mamlaka serikali mtandao kuwa na utayari wa kuweka miundombinu ya TEHAMA pindi zinapoanzisha majengo ili kuepusha gharama zinazoweza kujitokeza baadae.

“Sheria inaelekeza kwamba tunapoelekea TEHAMA inaenda kutumika kila sehemu ,hivyo panapokuwa na mpango wa ujenzi wa miundombinu mfano majengo,reli,barabara ,madaraja lazima pawepo utayari wa mifumo ya TEHAMA ,kwa kufanya hivyo tunashirikiana na taasisi husika ,isiwe kesho kutwa ukitaka kujenga mfumo wa TEHAMA ubomoe ukuta ,mfano pale Dar Es Salaam barabara ya Mwendokasi kama unaelekea BRT ile barabara inajengwa kwa zege lakini ikifika muda ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA panakuwa na gharama nyingine “amesema.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Ni taasisi yenye mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.

Kuanzishwa kwa Mamlaka hii mwaka 2019 kunaendeleza afua za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na kuchukua sehemu ya mipango yake kwa sababu majukumu ya taasisi hizi yanafanana ingawa yanatofautiana katika mamlaka ya utendaji.

Mamlaka ya Serikali Mtandao ni taasisi iliyoirithi Wakala ya Serikali Mtandao iliyoundwa Aprili 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 Sura ya 245 ya mwaka 1997 yenye jukumu na Mamlaka ya Kuratibu, Kusimamia na Kukuza Jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania.

Kabla ya kuanzishwa Wakala ya Serikali Mtandao, matumizi ya TEHAMA Serikalini yalikuwa yanaratibiwa na kusimamiwa na Idara ya Usimamizi wa Mifumo (DMIS) iliyopo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo kwa sasa ni Idara ya Huduma za TEHAMA Serikalini (DICTS).

Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 imeainisha majukumu na mamlaka yanayoiongoza Mamlaka ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini Tanzania.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger