Sunday, 28 November 2021

SERIKALI YAIAGIZA TAKUKURU KUWA WAKALI KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI ZILIZOTOLEWA NA RAIS SAMIA

...

Naibu Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora Deo Ndejembi akifunga Mkutano wa mwaka wa wakuu wa Takukuru Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa mwaka wa wakuu wa Takukuru Jijini Dodoma.
Viongozi wakuu wa Takukuru kutoka mikoa 28 nchini wakiwa katika picha ya pamoja katika mkutano wao wa Mwaka wenye lengo la kutathmini utendaji kazi.


Na Dotto kwilasa, Malunde 1 blog_Dodoma

SERIKALI imeiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) kufuatilia,kusimamia na ikibidi kuwa wakali katika fedha zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule na vituo vya afya.

Hatua hii imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia azindue Mpango wa Serikali kuinua uchumi na kukabikiana na ugonjwa wa virusi vya Corona kwa kutumia mkopo wa fedha wa shilingi Trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kutoa onyo Kwa watendaji kuzielekeza fedha hizo kwenye malengo yaliyokusudiwa.


Naibu wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Deogratius Ndejembi amesema hayo jana Wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa wakuu wa TAKUKURU jijini Dodoma na kusema kuwa kuna viashiria vya rushwa katika fedha hizo huku akidai kuna maeneo tofali linafuatwa umbali wa kilomita 150 wakati kuna uwezekano wa kupatikana kwa urahisi.

Ndejembi amekosoa pia uamuzi wa baadhi ya watendaji kuchukua muda mrefu kwenye ushindani wa zabuni na kushindwa kukidhi mahitaji muhimu ya muda wa utekelezaji wa miradi ndani ya miezi tisa kuanzia sasa na kubainisha kuwa hali hiyo huenda ikawa ni kiini cha rushwa, uzembe, upendeleo, pamoja na uwezo mdogo wa mzabuni.

“Nawaagiza TAKUKURU nendeni mkasimamie fedha za miradi zilizotolewa na Rais, kuna viashiria vya rushwa katika fedha hizo ,maeneo mengine tofali linafuatwa umbali wa kilomita 150 mtu mmoja anapewa tenda za kununua matofali,kuna maeneo mengi ujenzi umesimama ukiuliza unaambiwa nondo zimeisha,hapa kuna viashiria vya rushwa,niwaombe sana mfuatile na muwe wakali,”amesema.

Aidha,Naibu waziri huyo ameitaka TAKUKURU kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwa na mipango ya katika kuzuia zaidi ili kuleta faida.

“Tusimame imara tuwadhibiti watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea simamieni rushwa na mmomonyoko wa maadili huku mkizingatia utoaji wa haki,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni,amesema katika Mkutano huo wa siku tatu uliohusisha viongozi wa Taasisi hiyo kutoka mikoa 28 wameweza kutathmini utendaji wao na kujadili namna Bora ya kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa.

"Kwa muda wa siku tatu tumejifunza mengi kupitia mada mbalimbali za misingi ya maadili na mashauri ya kinidhamu,yote haya ni kuhakikisha chombo hiki kinakuwa cha mfano, kwa ujumla kila mmoja wetu amépata tiba anayostahili,"amesema Mkurugenzi huyo.

Sambamba na hayo amesema Taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti kubaini njia bora za kuziba mianya ya rushwa na kwamba kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla ya shilingi billioni 29.3 ziliokolewa na kwamba billion 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslim na utaifishaji mali huku kiasi cha bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.

Ameeleza miradi ya kimaendeleo 1,188 yenye thamani ya billion 714.17 katika sekta ya afya maji elimu ziliweza kufatiliwa na kuona makosa ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumejifunza namna ya kudhibiti hisia hasi na mahusiano kazini,hali hii itatupa nguvu zaidi ya kuzuia vitendo vya rushwa na kuongeza kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watuhumiwa Mahakami kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya mashtaka", amefafanua.

Vile vile ameeleza kuwa jumla ya majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa huku majadala 339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakani esi mpya zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger