Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametatua mgogoro wa muda mrefu kati ya mmliki wa machimbo ya dhahabu ya Kwandege yaliyopo wilayani Handeni mkoani Tanga, Godfrey Bitesigirwe na wananchi wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika machimbo hayo mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tanga yenye lengo la kukagua shughuli za madini na kutatua changamoto mbalimbali.
Mara baada ya kusikiliza kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi kupitia mkutano wa hadhara mapema jana tarehe 25 Juni, 2020 alielekeza mmiliki wa leseni ya madini, Godfrey Bitesigirwe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho, Afisa Mgodi Mkazi wa Handeni na wananchi kukaa pamoja na kuweka makubaliano ya pamoja yatakayowezesha wananchi na mmiliki wa leseni kunufaika kwa pamoja huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Aidha Naibu Waziri Nyongo alielekeza kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho kwa mkataba kati ya wachimbaji wa madini na mmiliki wa leseni ili kuondoa kasoro zilizokuwa zinalalamikiwa na wananchi hao.
Alisema kuwa ili kuhakikisha wananchi maskini wananufaika na rasilimali za madini, Serikali imeweka utaratibu wa kurasimisha wachimbaji wasio rasmi na kuwasaidia ili waweze kutajirika huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Katika hatua nyingine Nyongo aliwataka wananchi kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni za madini huku wakijikinga na magonjwa hatarishi kama COVID 19.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alimpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe kwa hatua za awali za utatuzi wa mgogoro zilizofanywa kwa mafanikio makubwa.
Awali akisimulia historia ya mgogoro huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho alieleza kuwa awali ofisi yake ilipata taarifa za kuwepo kwa uvamizi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la kijiji cha Kwandege kwenye leseni inayomilikiwa na Godfrey Bitesigirwe ambapo ofisi ilimshauri kuchukua hatua za kuzuia uchimbaji usio rasmi ili kuepusha ajali pamoja na upotevu wa kodi za serikali pamoja na utoroshaji wa madini.
Alisema kuwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Handeni na Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Handeni ilifanya ukaguzi ili kujionea hali halisi na kubaini wachimbaji 300 wakiendelea na shughuli za uchimbaji kwenye leseni husika na kuwataka wachimbaji hao kusubiri utaratibu maalum utakaowekwa kabla ya kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Aliendelea kusema kuwa katika hatua nyingine, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga iliwaelekeza wamiliki wa ardhi katika maeneo yenye leseni za uchimbaji wa madini kukutana na mmiliki wa leseni ambapo mara baada ya kukutana walikubaliana wamiliki wa mashamba katika maeneo yatakayofanyika uchimbaji wa madini ya dhahabu kupata asilimia saba ya thamani ya madini baada ya tozo za Serikali na gharama zote za uchimbaji wa madini kuwa chini ya mmiliki wa leseni.
Makubaliano mengine yalikuwa ni pamoja na umiliki wa mashamba kuendelea kuwa chini ya wamiliki na tozo za Serikali ambazo ni mrabaha asilimia 6 ada ya ukaguzi asilimia 1 na ushuru wa huduma za jamii 0.3 ya thamani ya madini zitakatwa kabla ya mgawanyo wa makubaliano.
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti mbali na kuipongeza Wizara ya Madini kwa kumaliza mgogoro wananchi hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutozwa kodi ambazo zingetakiwa kulipwa na mmiliki wa leseni ya madini na ukosefu wa vifaa vya uchimbaji wa madini.
0 comments:
Post a Comment