Friday, 1 May 2020

“sijaridhishwa Na Utendaji Kazi Wa Chama Kikuu Cha Ushirika Geita” - Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo

...
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ametembelea Chama Kikuu cha Mkoa wa Geita (Geita Cooperative Union-GCU) kilichopo Kasamwa wilaya ya Geita  na kutoridhishwa na hali ya kiwanda cha kuchambua pamba kushindwa kufanya kazi muda mrefu.

Ametoa kauli hiyo leo (01.05.2020) wakati alipotembelea na kukagua shughuli za taasisi zilizo chini ya wizara yake na kusema kiwanda cha kuchambua pamba (ginnery) Kasamwa kimeshindwa kujiendesha kutokana na mitambo na majengo yaliyopo kuwa ya kizamani yaliyotumika toka mwaka 1956

“Nimekagua na sijaridhishwa na jinsi kiwanda (ginnery) hii ya Kasamwa kuona haina hata mtambo mmoja unaofanya kazi hali inayopekea pamba ya ya wakulima kuchakatwa kwenye viwanda binafsi “ alisema Kusaya

Amewaagiza viongozi wa Chama kikuu cha ushirika Geita kushirikiana na serikali ya mkoa na wadau kufufua kiwanda hicho ili kitumike kuongeza thamani ya zao la pamba inayozalishwa wa wakulima wa Geita kwa kutafuta mitambo ya kisasa.

Awali Katibu Mkuu Kusaya  alikagua kiwanda cha Matongo Farming Limited cha Geita na kukuta  kimesimama kuzalisha marobota ya  pamba kutokana na upungufu wa malighafi.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Samson Ng’walida kilianzishwa mwaka 2018 na kina  uwezo wa kuzalisha marobota 450 kwa siku na kuchambua pamba mbegu tani 270 kwa siku.

“Uwezo wa kiwanda ni kuchambua tani 48,600 kwa mwaka na msimu huu wa 2019/2020 tumefanikiwa kuzalisha jumla ya robota 9,412 za pamba nyuzi sawa na asilimia 19 ya uwezo wa kiwanda” alisema Mwalida Samson ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa kiwanda cha Matongo Ginery.

Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu Kusaya alitoa wito kwa mikoa yote 17 inayozalisha pamba nchini kutengeneza mazingira rafiki kwa wananchi na wawekezaji ili waongeze uzalishaji wa pamba kukidhi malengo ya Serikali ya awamu ya Tano kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.

 “Napenda kuona uchakataji wa pamba unafanyike mwaka mzima badala ya miezi mitatu au minne ya  sasa kutokana na ukosefu wa malighafi  hali inayosababisha ajira kupungua na serikali kukosa mapato kutokana na viwanda kutozalisha bidhaa za pamba” alisema Kusaya.

Amewataka wataalam wa kilimo nchini kuwasaidia wakulima kupata ya mbegu bora za pamba zinazozalishwa kituo cha utafiti TARI Ukiriguru pamoja na matumizi ya pembejeo na mbolea ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga alisema takwimu zinaonesha mkoa wa Geita umezalisha kilo milioni 33 za pamba katika msimu wa 2019 kiasi ambacho ni kidogo kulingana na mahitaji makubwa ya viwanda vilivyopo mkoani humo.

Aliongeza kusema uwezo wa viwanda vya ndani nchini kwa sasa ni kuchakata pamba ni tani milioni 1.2 wakati uzalishaji umefikia tani 348,910 na kusema bodi yake itaendelea kubuni mikakati mizuri ili uzalishaji pamba uongezeke.

Mwisho
Imetolewa na :
Kitengo cha mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Kilimo


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger