Dk. Mayrose Majinge, amekuwa mwanachama wa kwanza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza nia ya kuomba ridhaa ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Dk. Mayrose alisema kuwa lengo la kuwania nafasi hiyo ni kutaka kuona Tanzania inakuwa taifa imara lenye watu wenye afya bora na wenye uhuru kamili.
Alisema tangu mwaka 2005 alianza harakati hizo akiwa miongoni mwa watia nia kuwania nafasi ya kugombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, kabla halijagawanywa na kuwa majimbo mawili (Segerea na Ukonga), lakini kura hazikutosha jambo ambalo alidai limempa uzoefu mkubwa wa kisiasa.
“Nilipata uzoefu mwingine wakati nilipowania nafasi ya ubunge Bunge la kwanza la Afrika Mashariki, ndiyo maana kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015 sikuonekana katika ulingo tena, siyo kama niliacha kwa kutopenda ubunge, bali niliamua kujikita katika maandalizi ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi wa nchi,” alisema Dk. Mayrose.
Alisema uongozi ni dhamana, ni lazima watu wakujue na kukuamini kwa kujitolea kusaidia katika nyanja mbalimbali ili waweze kukupa dhamana ya kuongoza nchi.
Dk. Mayrose alisema mwaka 2014/2019 alifanya kazi kubwa ya kuzuru nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kujenga uhusiano wa kimataifa.
Alisema katika masuala ya diplomasia pia ameshiriki mijadala ya nchi zaidi 51 duniani iliyomsaidia kupata taarifa na uzoefu kuhusu masuala ya utawala bora, haki na usalama wa raia.
“Nimeamua kwenda nje na kuwaacha watoto wangu wanne na mume wangu ili kukisaidia chama changu kupata uzoefu katika uwendeshaji wa vyombo vya maamuzi, utungaji wa sera na shughuli za siasa kwa vyama vya siasa ndani ya jamii kutoka kwa mataifa yaliyoendelea.
“Uwezo wa kuongoza ninao. Ili tuondokane na umaskini ni lazima jitihada za makusudi za kushughulikia upatikanaji na utumiaji wa silaha sahihi (siasa safi) zitiliwe mkazo,.
“Ni vema tutambue kuwa siasa safi ni nguzo ya uongozi bora ambayo ni chachu ya maendeleo endelevu,” alisema Dk. Mayrose.
Alisema Chadema inaamini kuwa kanuni miongozo pamoja na katiba ya chama hicho vinatoa haki kwa mwanachama yeyote mwenye sifa kuwania nafasi ya uongozi wa dola ikiwamo urais.
Dk. Mayrose alisema kuwa amejipima na kuona kwa hakika anatosha kuwa mwakilishi sahihi kama chama kitamteua kuwania nafasi hiyo ili aweze kupambana na wagombea wa vyama vingine.
0 comments:
Post a Comment