Thursday 23 January 2020

Waziri Mpina Aunda Timu Uchunguzi Ukwepaji Wa Kodi Kampuni Ya Ufugaji Samaki

...
NA MWANDISHI WETU, MAFIA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda timu ya wataalamu kufanya uhakiki wa takwimu, mauzo, uzalishaji na uendeshaji wa Kampuni ya Alphakrust inayojishughulisha na uzalishaji wa samaki aina ya Kambamiti pamoja na uhalali wa mapato ya Serikali kufuati kuwepo udanganyifu kwenye biashara hiyo.

Kulingana na takwimu za mauzo ya Kambamiti nje ya nchi kampuni hiyo ilipaswa kulipa shilingi milioni 300 kama ushuru wa huduma kwa Halmashauri hiyo lakini imekuwa ikilipa shilingi milioni 100 kwa mwaka na hivyo kuipunja Serikali kiasi cha shilingi milioni 200 kila mwaka.

Waziri Mpina amebaini njama hiyo inayofanywa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kushirikiana na Mwekezaji wa Kampuni ya Alphakrust inayofuga samaki aina ya Kambamiti kisiwani humo kwa lengo la kuiibia Serikali mapato yake yanayotakiwa kutozwa kama ushuru wa huduma yaani ‘Service Levy’

Alisema Halmashauri ya Mafia imetengeza makadirio ya kutoza ushuru wa huduma ya shilingi milioni 9 kwa mwezi kutoka Kampuni ya Apha Krust na kuacha Kanuni maalumu iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya ukokotoaji wa mapato yanayopatikana ya kutakiwa kulipa asilimia 3 ya mapato yote yanayopatikana kwenye biashara husika.

Udanganyifu huo umebainika wakati wa ziara ya Waziri Mpina ya kukagua Kituo cha kutotoleshea vifaranga na Shamba la ufugaji samaki aina ya Kambamiti lilomilikiwa na Kampuni ya Alphakrust kisiwani Mafia.

Waziri Mpina katika ziara hiyo aliambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mafia ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma, Wakurugenzi na Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mpina alihoji iweje Halmashauri ya Mafia itoze ushuru kinyume cha Sheria wakati kanuni za ukokotoaji wa mapato zinajulikana na hivyo kuamini kuwa huo ni mkakati wa siri uliosukwa baina ya Halmashauri ya Mafia na Kampuni ya Apha Krust kwa lengo la kukwepa kulipa mapato stahiki ya Serikali.

“Haiwezekani Halmashauri ya Mafia ikaacha kufuata fumula ya uchukuaji wa ‘service levy’ uliowekwa na Serikali na kutengeneza utaratibu wake yenyewe..mwisho wa siku watu wa nje tunachoweza kukielewa ni njama inayowekwa baina ya Halmashauri na Mwekezaji kuiibia Serikali” alisema Mpina.

“Kwanini mkokotoo huo usizingatie sheria takwimu za makusanyo zipo, bei inayotumika kuuza na masafirisho ya nje ipo kwanini haikutumika kukokotoa..kwanini itumike fumula ya kukubalina nje ya utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria”alihoji Waziri Mpina.

Waziri Mpina alisema kama halmashauri inatoza fedha nyingi zaidi za ushuru wa huduma tofauti na iliyowekwa kwenye Sheria ni makosa kwani Serikali haiwezi ikatoza fedha ambazo haziko kwenye utaratibu wa sheria lakini kama halmashauri inakusanya fedha kidogo kuliko sheria inavyosema nalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

“Kwanini uchukue fedha kidogo wakati fomula ya kupata makusanyo halisi kwa niaba ya wananchi ipo..kwanini wewe utumie fumula ya kwako ya kubuni wewe wakati fumula ya kisheria ipo”alihoji Waziri Mpina.

Mbali na dosari hizo za ukwepaji kodi, Waziri Mpina alielezea kusikitishwa kwake na kitendo cha mwekezaji huyo kushindwa kuwashirikisha wananchi wanaozunguka eneo hilo kujifunza teknolojia hiyo ili kukuza sekta ya ukuzaji viumbe maji hasa ufugaji wa Kambamiti.

Alisema Serikali haijapokea maombi yoyote ya upungufu wa wataalamu wenye utaalamu na uzoefu maalum kuendesha mradi kwani wataalamu hao wanazalishwa katika vyuo vyetu kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Vyuo vya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).

“Mradi huu unaendeshwa kwa usiri na wivu mkubwa kiasi kwamba wananchi wa kawaida hawawezi kupata utaalamu kupitia mradi huu..kwenye taarifa yenu sikuona mkichukua vijana wanaomaliza vyuo au kuingia makubaliano na vyuo (MOU) kufanya mafunzo ya vitendo kwenye mradi huu na kuwalipa kima cha chini cha mshahara”alihoji Waziri Mpina.

Alisema wawekezaji kutoka nje wanapofika nchini wanalojukumu katika mikataba yao ya kusambaza taaluma katika eneo lao la uwekezaji ili kuwawezesha watanzania wengi kunufaika na uwekezaji wao na kueleza kusikitishwa kwake na kampuni hiyo kuwabagua wazawa na kuwapa nafasi wageni hata kwenye kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania.

“Toka nimeanza kutembelea miradi hii kuanzia Dar es Salaam nimekuja kwenye shamba la kambamiti na kituo cha kutotoleshea vifaranga mapokezi na utolewaji wa maelezo na ufafanuzi unafanywa na wageni hii ni ishara kwamba uongozi wote umeundwa na wageni au ni sehemu ya kuficha ukweli juu ya undeshaji wa biashara hiyo’ alihoji Waziri Mpina

Mbali na hilo Waziri Mpina alisema Serikali inazo taarifa za vijana wanaokwenda kufanya kazi kwenye uwekezaji huo wanashindwa kufanya kazi kutokana na ujira mdogo wanaolipwa na mwekezaji huyo na kuvunjika moyo na kisha kuondoka.

“Kulipwa mshahara mdogo haijulikani wanalipwa hivyo ili wakate tamaa waondoke na baadae itengeneze nafasi ya ajira kutoka nje ya nchi au tatizo ni nini”alihoji Waziri Mpina.

Kwa upande wake Meneja wa Alphakrust, Ganeshan Vedagiri amelalamikia kukosa wataalamu wenye weledi na pindi watanzania wanapoajiriwa wanakaa muda mfupi na kuondoka huku akilalamikia kudaiwa ushuru kwenye halmashauri zaidi ya moja

Alisema mradi huo wa Mafia una mabwawa 31 ya Kambamiti ambapo kwa mwaka huzalisha wastani wa tani 400 huku asilimia 90 ya samaki hao wakiuzwa nchini ufaransa huku asilimia 10 zikiuzwa hapa nchini. 
 
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Chuchu Silvery licha ya kuwepo kwenye ziara hiyo hakuweza kuzungumzia chochote kuhusiana na dosari hizo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger