Wednesday, 29 January 2020

Waziri Kairuki Atikisa Wilaya 6 Za Mkoa Wa Pwani, Awahakikishia Wawekezaji Mazingira Mazuri Ya Uwekezaji.

...
NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki amewahakikishia wafanyabiashara na Wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya Uwekezaji nchini.

Pia, Amesema Serikali imejipanga kuboresha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali zenye tija katika kuliingizia pato taifa.

Ameyasema hayo hivi karibu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 6 katika Wilaya 6 za mkoa wa Pwani ikiwemo; Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga, Mafia na Rufiji pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.

Akieleza lengo la ziara hiyo Mhe.Kairuki amesema mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali; Uvuvi, kilimo na ufugaji na amefanya  ziara hiyo ili kujionea mazingira  pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akitoa majumuisho ya ziara hiyo Mhe. Kairuki amezitaja changamoto zilizojitokeza katika maeneo mengi aliyotembelea kuwa ni ukosefu wa maji ya kutosha, ubovu wa barabara, ucheleweshwaji wa vibali vya kazi, kukosa umeme wa uhakika na utitiri wa tozo.

Mbali ya changamoto hizo, Mhe. Kairuki ametaja vikwazo vingine kuwa ni kutotengwa kwa maeneo ya uwekezaji, Taasisi wezeshi kutokuwa karibu na wawekezaji, ukosefu wa mitaji ya uhakika na utoaji wa adhabu zisizo za lazima.

Ameongeza kuwa uelewa mdogo wa wawekezaji katika kujiunga na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ni moja ya  changamoto na kuwataka  wawekezaji kwa hiari yao waone umuhimu wa kujiandikisha katika kituo hicho ili kutumia fursa zinazopatikana.

“Wawekezaji tunawakaribisha TIC ili mjue fursa ziliopo nchini zaidi na kuona namna mnavyoweza kunufaika na kituo hiki,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Ameongoza kuwa, ipo haja ya kila Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ili kutoa fursa zaidi kwa watu kuwekeza na kuhakikisha miundombinu muhimu inakuwepo.

“Natoa rai kwa kila Halmashauri kuhakikisha kila kijiji kinatenga walau heka 20 za maeneo ya uwekezaji na kuwasilisha taarifa zao TIC” alisema Waziri.

Aidha, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji kuzingatia sheria na taratibu za uwekezaji nchini ili waweze kunufaika na mitaji yao waliyowekeza.

“Endeleeni kuwekeza pasipo kuvunja sheria na kanuni zilizopo ikiwa ni kulipa kodi au kulipa vibali mbalimbali mfanye hivyo tena kwa wakati ili isitokee mmewekeza kwa mitaji mikubwa halafu ikawa kwa hasara,”alisisitiza Waziri Kairuki

Aliwahakikishia wawekezaji kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua mchango wao na imedhamiria kuhakikisha inaboresha miundombinu muhimu ikiwemo uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika, barabara bora, upatikanaji wa maji safi, kuboresha mifumo ya mawasilino na upatikanaji wa huduma bora za mamlaka zinazosimamia masuala yanayohusu uwekezaji nchini.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger