Friday 31 January 2020

Uchumi wa Tanzania Wazidi Kukua na Kuimarika

...
Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Hali ya uchumi wa Tanzania imezidi kuimarika na kukua  kwa asilimia 6.9 ikiwa ni  takwimu za hadi mwezi Septemba 2019, huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 7.0% na 7.1% .

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) Januari 20 mwaka huu, inaonesha  kuwa uchumi wa dunia utakua kidogo kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 3.3 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2019/20.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana jijini Dodoma, kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa, huu ni ukuaji mkubwa katika nchi za Afrika Mashariki nyuma ya Rwanda pekee na bado Tanzania ni miongoni mwa nchi za juu kwenye ukanda wa  Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika kwa ujumla.

Dkt. Abbasi alisema kuwa sekta inayoongoza kwa ukuaji wa uchumi ni ujenzi ambayo inachangia asilimia 16, uchimbaji madini na mawe asilimia 13.7, habari na mawasiliano 10.7, maji asilimia 9.1, na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo asilimia 9.1.

Aidha, Dkt. Abbasi alisema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika ongezeko la ukusanyaji wa mapato kwa mwezi kutoka shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3.

“Leo ninayo furaha kulitangazia rasmi taifa kuwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato na Idara nyingine za Serikali, wastani wa mapato ya kodi kwa mwezi kati ya Julai hadi Disemba, mwaka 2019, umepanda na sasa ni shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi. Hii kwa sasa ndio rekodi mpya, na ndio habari mpya ya mjini”, alisisitiza Dkt. Abbasi.

Ukusanyaji wa mapato ni moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Tano. Huku ikitazamia kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kifedha na kupunguza kwa kadri inavyowezekana utegemezi kutoka kwa Wadau wa Maendeleo na kuhakikisha kwamba mipango ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini inatekelezwa bila kukwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

 Aidha, azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, haiwezi kufikiwa endapo Serikali haitokuwa na uwezo wa kifedha wa kugharamia shughuli mbali mbali za maendeleo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger