Wednesday 22 January 2020

Njombe:Mahakama yakamilisha kusikiliza ushahidi wa kesi ya mwanafunzi kuvunjwa uti wa mgongo

...
Na Amiri kilagalila-Njombe
Kesi namba 141-2019 inayomkabili mwalimu Focus Mbilinyi anayetuhumiwa kumvunja uti wa mgongo aliyekuwa  mwanafunzi wa shule ya msingi Madeke wilayani Njombe Hosea Manga baada ya kumpa adhabu ya viboko 10 kwa madai ya kukosa hesabu 10 imeendelea kusikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe kwa kukamilisha mahojiano na mashahidi wawili wa mwisho kutoka upande wa utetezi ambao ni wanafunzi wenza wa majeruhi huyo.

Akitoa utetezi mbele ya mahakama,Catheline Hongoli aliyekuwa kiongozi wa darasa la  Hosea Manga anasema machi 21 ,2017 mwalimu wa hesabu aliingia darasani na kuagiza wanafunzi ambao hawajafanya hesabu alizotoa kupita mbele ,ambapo miongoni mwa wanafunzi waliopita alikuwepo Hosea Manga ambaye aliadhibiwa viboko vitatu makarioni kwa kosa hilo.

Baada ya adhabu hiyo mwalimu alitoka darasani na Hosea Manga akaelekea chooni na kurejea akiwa darasani akiwa mzima na kisha baada ya muda mfupi akadondoka na kushindwa kusimama hali ambayo iliwasukuma wanafunzi kumwita mwalimu mkuu ambaye alimtoa na kumlaza nje ya darasa kijana Hosea Manga.

Shahidi wa pili na wa mwisho kwa upande wa uetetezi  Sephania Kyelula ambaye pia ni mwanafunzi mwenza wa kijana Hosea anasema kabla ya kupatiwa adhabu ya viboko vitatu Hosea Manga alikuwa na uwezo wa kutembea huku akidai kuwa na maumivu ya mguu lakini mapema baada ya kuadhibiwa alitoka na kwenda chooni na kisha kurejea darasani na muda mfupi akadondoka na kushindwa kuinuka.

Kesi hiyo inayoendeshwa na hakimu mkazi Ivran Msaki na kusimamiwa na mawakili watatu wa upande wa utetezi ambao ni Liliani Gama,Octavian Mbugwani na Innocent Kibadu imeahirishwa mpaka februali 4 itakaposikilizwa kesi ya majumuisho na kutajwa tarehe ya hukumu.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger