Friday 24 January 2020

Makusanyo Kiduchu Halmashauri Za Mkoa Wa Rukwa Yamchefua Naibu Waziri Mabula

...
Na Munir Shemweta, WANMM RUKWA
Makusanyo ya kodi ya pango la ardhi katika halmashauri za mkoa wa Rukwa yamemvuruga Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula baada ya kuelezwa kuwa hadi kufikia Desemba 2019 jumla ya shilingi milioni 148.2 zilikusanywa na halmashauri zote nne sawa na asilimia 7.9 .

Akiwa  katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Rukwa jana ambapo alikutana na watumishi wa sekta ya ardhi, Dkt Mabula alishangazwa na namna maafisa ardhi wa halmashauri hizo wasivyofuatilia makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kiasi cha kuzifanya halmashauri hizo kukusanya kiasi kidogo cha fedha.

Alisema, haiwezekani ndani ya miezi sita halmashauri nne za mkoa wa Rukwa zikusanye asilimia 7.9 ya kodi ya pango la ardhi jambo alilolieleza kuwa linatia mashaka kama halmashauri hizo zitaweza kufikisha hata asilimia hamsini ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kwa mujibu wa Taarifa ya mkoa wa Rukwa iliyosomwa na Mrasimu Ramani wa mkoa wa Rukwa Kelvin Maungi, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri za mkoa huo  zilikadiriwa kukusanya jumla ya sh 1,880,000,000.00 ambapo Manispaa ya Sumbawanga ilikusanya kiasi cha sh. 94,253,273.00, Halmashauri ya wilaya ya Nkasi sh. 16,494,189.00, Kalambo sh 1,793,550.00 na Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga sh 35,680,575.00 na hadi hadi Desemba 2019 jumla ya shilingi 148,221,587.00 zilikusanywa kwa halmashauri zote sawa na asilimia 7.9.

‘’Wakurugenzi wako busy na masuala mengine, mkoa mzima una silimia 7.9 ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi! ni aibu na hamuwezi kufikia asilimia 50 ya makusanyo naagiza wote mkafanye uhakiki wa wadaiwa wa kodi ya ardhi na muwapelekee ilani ili watakaokaidi wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, Naibu Waziri Mabula aliagiza kufikia Machi 2020 lazima kuwe na mabadiliko ya utendaji kazi kwenye sekta ya ardhi kwa halmashauri za mkoa wa Rukwa, vinginevyo atafikiria kama wakuu wa idara wanatosha kuendelea na nafasi zao na kusisitiza kama ni Mkuu wa Idara au Afisa Ardhi Mteule ataondolewa.

Dkt Mabula alisema mikoa yote aliyoitembelea kwenye ziara zake za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi imefikisha asilimia thelathini ya makusanyo ya kodi ya ardhi lakini mkoa wa Rukwa umemsononesha sana na kumuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda Thadei Kabonge atoe maelezo kuhusiana na utendaji kazi wa Wakuu wa idara kama wanafaa kushika nafasi zao.

Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula alibainisha kuwa kulingana na taarifa zilizokuwa kwenye mfumo wa kielektronik Manispaa ya Sumbawanga ilitakuwa kukusanya Bilioni 6.7, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga milioni 20, Kalambo milioni 1.6 na Nkasi milioni 16 hiyo inatokana na halmashauri hizo kuwa na malimbikizo ya wadaiwa kodi ya pango la ardhi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger