TANZANIA na Burundi wamesaini makubaliano ya kuwarejesha Wakimbizi 2000 kwa kila wiki nchini mwao kuanzia Oktoba Mosi, 2019.
Wakimbizi hao waliopo katika Kambi ya Nduta na Mtendeli wanatarajiwa kusafirishwa kuelekea katika nchi yao ya asili kutokana na amani iliyopo katika nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchini Burundi, Pascal Barandagiye tayari wamesaini makubaliano hayo ambayo watahakikisha wakimbizi wote waliopo katika kambi hizo wanartejeshwa nchini mwao bila kukwamishwa na mtu au shirika lolote.
Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Kigoma jana, Waziri Lugola alisema makubaliano hayo yataanza rasmi Oktoba mosi na wakimbizi hao watakuwa wanarejeshwa nchini mwao na kupata mapokezi makubwa na Serikali ya Burundi.
“Tunataarifa wapo baadhi ya watu, mashirika ya kimataifa wanawarubani wakimbizi wakiowatangazia kuwa Burundi haina amani, jambo ambalo si la kweli, nchi hiyo ina amani na wakimbizi wanapaswa kurejea nchini mwao,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, atawachukulia hatua kwa watakaokwamisha zoezi hilo la kuwasafirisha wakimbizi hao, kwa kuwa Serikali ya Wakimbizi inataka watu wao na Tanzania imeamua kuwapa watu wao ili waende wakaijenge nchi.
“Natoa kauli hii sio kuwatisha au kutishia nyau, bali nasema, Serikali ya Magufuli haiwezi kuchezewa na mtu yeyote, hivyo tutawakamata wanaowarubani, wanaowashawishi wakimbizi wasiende nchini mwao,” alisema Lugola.
Wiki iliyopita, katika mkutano wa hadhara katika Kambi ya Nduta, baadhi ya Wakimbizi walisema wanawekewa vikwazo na kucheleweshwa na baadhi ya watendaji wa mashirika ya wakimbizi kambini humo wakati wanapoomba kujiandikisha kurejeshwa kwao.
Mkimbizi wa kambi hiyo, Nzoisa Bhainoje, alisema yupo tayari kurejea nchini Burundi lakini amefanya juhudi za kwenda eneo la kujiandikisha kambini hapo lakini hakufanikiwa kutokana na kusumbuliwa akiambiwa kuwa idadi wanaotakiwa kuondoka imekamilika.
“Nakumbuka nilifika eneo la kuondoka siku ya Jumanne lakini ilishindikana kujiandikisha kutokana na kukwamishwa, wengi tunataka kuondoka lakini tunashindwa kuondoka kwasababu tunakwamishwa,” alisema Bhainoje.
Bhainoje aliongeza kuwa, wanaomba watendaji hao wawaruhusu kwa wale wanaotaka kurejea nchini mwao kwa hiari, lakini kwa wale ambao hawataki kuondoka wanaweza kubaki kwa mipango yao.
Baada ya wakimbizi hao kutoa kero zao kwa Waziri Lugola na Waziri Barandagiye, ndipo Lugola aliagiza kufanyika uchunguzi katika kambi hiyo kuwakamata wale wote ambao wanakwamisha wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari.
“Naagiza uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo kwa yeyote atakayehusika anakwamisha zoezi hili la kuwarejesha wakimbizi hawa ambao wapo tayari kuondoka nchini kwao kutokana na amani iliyopo, awe Afisa kutoka Wizarani, awe afisa wa shirika lolote, awe yupo hapa kambini, lazima tutamkamata na kumpeleka mahakamani,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, muda umefika kwa wakimbizi wa Burundi kurudi nchini mwao, kwasababu zile sababu ambazo zilikuwa zinazuia zoezi la kuwarudisha kwao wakimbizi hao kwa sasa havipo tena kwasababu nchi hiyo ina amani.
Alisema Serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli imejiridhisha sababu kubwa iliyowaleta wakimbizi hao wa Burundi nchini ya kutowepo kwa amani haipo tena na kwamba kwa sasa Burundi ipo salama kiulinzi na kiusalama pia kisiasa hivyo wakimbizi hao wanapaswa kurudi nchi mwao wote bila kuwepo kikwazo chochote.
"Wanaosema Burundi haina amani wanaipaka matope nchi hiyo kwani jambo hilo halina ukweli wowote na Tanzania imefanya uchunguzi wa kutosha na kujiridhisha kuwa amani ya kudumu ipo nchini humo, Oktoba Mosi tutaanza kutekeleza mkataba wa pande tatu wa kurudishwa kwa wakimbizi 2000 kila wiki wa Burundi kwenda nchini mwao," alisema Lugola.
Naye Waziri Barandagiye, kwa upande wake alisema Burundi iko tayari kutekelezwa kwa makubaliano ya pande tatu ya kuhakikisha wakimbizi wote wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi mbalimbali ya wakimbizi mkoani nchini wanarudi Burundi lakini wanashangazwa na namna Shirika la Kuhudumia Wakimbizi linavyoendesha zoezi hilo kwa kasi ndogo.
Waziri Lugola na Barandagiye walitembelea Kambi ya Nduta, Wiliyani Kibondo na Mtendeli iliyopo Wilayani Kakonko mkoani humo, kwa lengo la kuhamasisha wakimbizi katika kambi hizo kurejea nchini kwao kwa hiari.
0 comments:
Post a Comment