Saturday 17 August 2019

Soko La DSE Laendelea Kushika Nafasi Ya Tatu Barani Afrika Kwa Ubora

...
Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Soko la Hisa la Dar es Salaam- DSE limetakiwa kuendelea kujiimarisha kwa kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwekeza zaidi katika soko hilo lengo likiwa kukuza kipato chao na uchumi wa nchi.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara katika Soko hilo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Dkt. Kazungu alisema kuwa, idadi ya watu takribani laki tano ambao wamewekeza katika Soko hilo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watanzania wote ambao ni zaidi ya milioni 50, hivyo ni vema DSE ikatumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha wananchi kushiriki katika Soko hilo ili kukuza kipato chao kutokana na faida zake.

Alisema ushiriki wa watu wengi katika Soko hilo hususani walio katika sekta ya uvuvi, mifugo na kilimo, kutaongeza chachu ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati uliojikita katika viwanda.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Moremi Marwa, amesema kuwa Soko la DSE lipo kwa ajili ya kuwezesha wawekezaji kuwekeza katika maeneneo mbalimbali kulingana na bidhaa zilizopo sokoni.

Alisema ili kuleta bidhaa zaidi katika Soko la Mitaji, DSE imekuwa ikifanya juhudi kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuziwezesha Serikali za Mitaa na Halmashauri za Miji na Majiji kuweza kupata fedha kupitia mifumo ya Masoko ya Mitaji ili kuweza kuwekeza katika miradi ya Maendeleo ya Uchumi na Kijamii.

Alieleza kuwa mifumo ya masoko ya Mitaji katika Halmashauri inataleta wigo mwingine wa upatikaji wa fedha kwa ajili ya kujenga miradi ya miundombinu na viwanda katika miji na majiji nchini.

Bw. Marwa alibainisha kuwa DSE huwapa wajasiriamali, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na Serikali kutumia soko kwa ajili ya masuala ya upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati katika kusaidia wafanyabiashara kuboresha biashara zao pia kwa Serikali Kuu kuendesha miradi mbalimbali ya Serikali hasa iliyo katika Bajeti.

“Soko la DSE limekua kutoka Sh. trilioni 16 hadi trilioni 20 katika kipindi cha miaka minne,  hati fungani Sh. trilioni 3.5 hadi trilioni 9.5. na kwa wawekezaji kutoka  220,000 na sasa 550,000; ukwasi na miamala sokoni imeongezeka kutoka wastani wa  takribani Shilingi bilioni 50 kwa mwaka hadi zaidi Shilingi bilioni 500  kwa mwaka na katika miamala na ukwasi wa hati fungani kutoka wastani wa Shilingi bilioni 300 hadi kufikia wastani wa takribani Shilingi bilioni 900 kwa mwaka”, alieleza Bw. Marwa

Bw. Marwa alisema kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri katika vigezo hivyo ambavyo hutumika katika kupima maendeleo ya Soko, pia DSE imeongeza tija na ufanisi kwa kuwa kampuni inayojiendesha kwa faida na kulipa faida hiyo kama gawio kwa wanahisa wake, ikiwemo Serikali.

Alisema kuwa DSE ilipata uanachama wa kidumu katika Chombo cha Kimataifa kinachosimamia masoko ya Hisa (World Federation of Exchanges) mwanzoni mwa mwaka huu, ikiwa ni soko la saba kufikia hatua hiyo barani Afrika.

Afisa huyo Mtendaji Mkuu wa DSE alisema Soko hilo limewekwa kwenye uangalizi “Watch-List” na Shirika la Kimataifa la Kupima viwango na ubora vya Uchumi na Masoko ya Mitaji “Country and Market Classification” kwa nia ya kuifanya DSE kuwa “Frontier Market Status” ifikapo Septemba Mwaka huu.

Hatua hiyo inatoa fursa ya kulitangaza zaidi soko kwa wawekezaji wa nje lakini pia kupata mitaji kutoka kwa wawekezaji wanaotoka nje wanaokuja kuwekeza katika kampuni na biashara nchini na kwenye miradi mbalimbali.



Soko la DSE limekuwa la tatu katika masoko 30 yaliyopo barani Afrika kufikia hatua hiyo, masoko mengine ni Soko la Hisa ni Johannesburg la Afrika Kusini ambalo lina miaka zaidi ya 100, na pia Soko la Hisa la Nairobi (Nairobi Securities Exchange) ambalo lina miaka takribani 70 tangu uanzishwaji wake, lakini DSE likiwa na miaka 20 tu na  linafanya vizuri katika medani za kimataifa.

Alisema kuwa DSE ina bidhaa kuu tatu zilizopo Sokoni ambazo mwananchi yeyote anaweza kuwekeza, bidhaa hizo ni Hisa, ambapo kuna Kampuni 28 zilizoorodheshwa Sokoni zenye ukubwa wa thamani ya takribani Shilingi bilioni 19.2. Bidhaa nyingine ni Hati Fungani za Serikali zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 9.5 na pia Hati fungani za makampuni binafsi zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 250.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger