Wednesday 14 August 2019

Jamii Yatakiwa Kuwatambua, Kuwatumia Wasaidizi Wa Kisheria Kupata Msaada Wa Kisheria

...
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Msajili wa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria Tanzania, Bi. Felistas Joseph kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ametoa wito kwa jamii kuwatambua na kuwatumia wasaidizi wa kisheria pindi wanapohitaji msaada katika masuala ya kawaida ya kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa, utelekezaji wa familia na masuala mengine wanayokutana nayo siku kwa siku, ambao amesema wanatoa huduma hizo bila malipo yoyote.

Bi Felistas ameyasema hayo jana katika kikao cha Uundaji wa Kamati ya Uratibu wa Huduma za Msaada wa kisheria Mkoani Simiyu   kilichofanyika  Mjini Bariadi.

Amesema kada hii inatambuliwa kwa mujibu wa sheria ya msaada wa kisheria na wamefundishwa mafunzo ya awali ya sheria katika masuala ambayo wananchi wanakutana nayo siku kwa siku hivyo ni vema jamii na wadau wengine wakawatambua na kuwapokea kwa kuwa ni watu waliojitoa kuisaidia jamii bila malipo yoyote.

“Nia yetu ni kwamba jamii iweze kuwafahamu na kuwapokea wasaidizi wa kisheria, hawa ni watu wanaojitolea kwa dhati kufanya hii kazi bila kudai malipo, wanachohitaji ni ushirikiano na wadau wengine wa Serikali pamoja na wananchi; kada hii inatambuliwa rasmi chini ya sheria ya msaada wa kisheria na wameshapewa vigezo na mipaka ya kufanyia kazi” alisema.

Ameongeza kuwa  Serikali imeandaa mtaala wa kufundisha wasaidizi wa huduma za kisheria na hadi sasa takribani wasaidizi wa kisheria 4500 wamefundishwa katika kipindi cha miaka mitatu nyuma ambao wamejiunga katika vikundi na kujisajili kama mashirika ambapo hadi sasa kuna jumla ya mashirika 200.
 
Awali akifungua kikao cha Uundaji wa Kamati ya Uratibu ya Huduma za Msaada wa kisheria Mkoani Simiyu, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  amesema endapo wasaidizi wa kisheria watutumiwa vizuri kero nyingi za wananchi zitatatuliwa na kufikia mwisho, huku kutoa wito kwa Wakuu wa wilaya, wabunge, madiwani na viongozi wengine kuwashirikisha wasaidizi wa kisheria katika mikutano ya hadhara ambapo wananchi huwasilisha kero zao.

Aidha, Mtaka amesema ili kuongeza uewelewa wa masuala ya msaada wa kisheria mkoani Simiyu ni vema Wizara ya Katiba na Sheria ikaona haja ya kuendela kutoa elimu kwa jamii, ambapo amewaalika kutoa elimu hiyo katika kambi za kitaaluma mkoani hapa ambazo zinatarajia kuanza mwezi Septemba, 2019 kwa kidato cha nne..

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Jumanne Sagini amesema viongozi wa Mkoa watahakikisha kamati za uratibu wa huduma za kisheria ngazi ya wilaya zinaundwa na wasaidizi wa kisheria wanatumiwa ipasavyo.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Mahamoud Kalokola amesema viongozi wa madhehebu ya dini wataendelea kutoa elimu kupitia makusanyiko ya ibada kwa waumini wao ili wananchi hususani wale ambao hawana na uwezo wa kifedha wa kuwalipa mawakili wajue kuwa wasaidizi wa kisheria wapo katika jamii na wanaweza kuwasaida kutatua changamoto zao.

Kamati ya Uratibu wa Shughuli za Huduma za Msaada wa Kisheria mkoa wa Simiyu imeundwa  na kuzinduliwa chini ya Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti, Msajili msaidizi(Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa), mtaalamu wa ardhi, jeshi la polisi (dawati la jinsia) Magereza, TAKUKURU, Mahakama, Mwanasheria, Afisa wa dawati la malalamiko, viongozi wa dini na Afisa ustawi wa jamii na Afisa habari ngazi.

Wajumbe wengine ni mwakilishi wa vyombo vya habari, wawakilishi wa wadau wa maendeleo, wawakilishi wa taasisi za watoa huduma za msaada wa kisheria,Mwenyekiti wa baraza la ardhi na mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambapo kwa muundo huu huu kamati za wilaya zitaundwa ziweze kutekeleza jukumu la uratibu wa shughuli za huduma za kisheria wilayani

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger