Sunday 18 August 2019

Idadi Kubwa Ya Hati Za Ardhi Ofisi Ya Msajili Kanda Ya Magharibi Yamshtua Naibu Waziri Mabula

...
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Idadi kubwa ya Hati za Ardhi takriban12,000 katika Ofisi ya Msajili wa Hati imemshtua Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi.

Mwishoni mwa wiki Dkt Mabula akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi sambamba na kukagua masijala ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Tabora alitembelea Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi kujionea utendaji kazi wa kanda inayojumuisha mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma.

Akiwa Ofisi ya Msajili wa Hati, Dkt Mabula alielezwa na Msajili wa Hati wa Kanda ya Magharibi Julian Ngonyani kuwa ofisi yake ina takriban hati 12,000 ambazo ziko tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwa waombaji lakini wahusika hawajajitokeza kuchukua kwa sababu ambazo hazijulikani.

Naibu Waziri Dkt Mabula alishangazwa na idadi kubwa ya Hati hizo na kubainisha kuwa Hati zilizopo Ofisi ya Msajili wa Hati kama zingechukuliwa basi wahusika wangekuwa na nyaraka zinazoonesha umiliki halali wa maeneo yao sambamba na hati hizo kuwasaidia katika shughuli za maendeleo kama vile kukopa pesa katika mabenki mbalimbali.

Alisema, Halmashauri katika mikoa ya Kanda hiyo ya Magharibi zinapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha waombaji wanapata hati ambapo alizitaka kuandaa utaratibu maalum utakaowezesha Hati kupelekwa kwenye halmashauri husika na waombaji kuzichukua.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, utaratibu huo utawawezesha wananchi kuchukua hati zao kwa urahisi bila ya usumbufu ambapo hivi sasa waombaji hulazimika kuzifuata Ofisi ya Kamishna wa Kanda jambo alilolieleza kuwa ni usumbufu kwani baadhi ya waombaji hulazimika  kutembea umbali mrefu hasa kwa wale wanaokaa maeneo yaliyo mbali na Ofisi ya Kanda.

‘’Halmashauri inaweza ikandaa utaratibu wa kupelekewa Hati za Ardhi katika maeneo yao na Ofisi ya Kamishna wa Kanda na jukumu la halmashauri litakuwa kugharamia pesa ya kujikimu kwa watumishi wa Kanda watakaopeleka hati na kuzikabidhi kwa waombaji, hiyo itasaidia kuwapunguzia mzigo wananchi’’ alisema Dkt Mabula.

Katika Hatua Nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameikabidhi Hati ya Kiwanja No 47 Block A Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tabora kilichopo eneo la Kanyenye Manispaa ya Tabora mkoni Tabora baada ya kiwanja hicho kuwa na mgogoro wa muda mrefu Kati ya ofisi ya CCM na Shirika la Utangazaji (TBC).

Dkt Mabula alimkabidhi hati hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tabora Mohamed Katete ambapo makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Katibu wa CCM mkoa wa Tabora Solomon Kasaba, Katibu UWT mkoa Rehema Mohamed, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharbi Idrissa Kayera na Msajili wa Hati wa Kanda Julian Ngonyani.

Katika Makabidhiano hayo, Dkt Mabula alisema Chama cha Mapinduzi kina maeneo mengi inayomiliki lakini siyo yote yenye hati na kubainisha kuwa kukabidhiwa hati hiyo iwe chachu kwa chama kuhakikisha maeneo yake yote yanakuwa na hati kuepuka migogoro.

Ametoa wito kwa CCM kuhakikisha maeneo ya Kata yanayomilikiwa na chama hicho yasiyopimwa yanapimwa na kupatiwa hati na hata yale yasiyo pimwa basi yawe na mipaka na kubainisha kuwa kwa kufanya hivyo kutaondoa migogoro na kukifanya chama kuwa na miliki halali ya maeneo yake.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger