Monday, 24 June 2019

Wema amaliza siku saba za kukaa gerezani....Mahakama Yampa Onyo la Mwisho

...
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imemuonya msanii wa Filamu nchini humo, Wema Sepetu(30), kutokukiuka masharti ya dhamana, vinginevyo haitasita kufutia dhamana yake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatayu, Juni 24, 2019 na Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Maira Kasonde wakati akitoa uamuzi kuhusiana na mshtakiwa kukiuka masharti ya dhamana.

"Mahakama inatoa onyo  la mwisho kwa mshtakiwa, ikitokea mshtakiwa huyu amevuja sheria kwa kutokufika mahakamani bila taarifa, Mahakama hii haitasita kumfutia dhamana.”

“Hivyo Mahakama imekurudishia dhamana yako na utakuwa nje kwa dhamana,"  amesema Hakimu Kasonde wakati akisoma uamuzi wake dhidi ya mshtakiwa huyo.

Wema ambaye alishawahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandaoni  wa Istagramu kinyume cha sheria.

Uamuzi wa kumpeleke Wema mahabusu ulifikiwa baada ya mshtakiwa huyo aliyekuwa anadaiwa kuruka dhamana kufikishwa mbele ya mahakama.

Akiiwakilisha Jamhuri Wakili wa Serikali, Glory Mwenda alidai mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani baada ya kuruka dhamana na mahakama kutoa hati ya kumkamata Juni 11 mwaka huu.

Hakimu Maira alisema mshtakiwa hakufika mahakamani Mei 14 mwaka huu bila taarifa na Juni 11 pia hakufika hivyo alimtaka kujieleza kwanini hakuhudhuria mahakamani na kwanini asifutiwe dhamana.

Akijieleza Wema alidai Mei 14 alisafiri kikazi kuelekea Morogoro akamjulisha Wakili wake, Ruben Simwanza na Juni 11 mwaka huu alifika mahakamani lakini aliumwa.

“Nilishindwa kupanda mahakamani, ninapofika kwenye siku zangu huwa napata maumivu makali, nilienda kuchoma sindano ya maumivu, nikapumzika kisha nikarudi nyumbani.

“Nilienda kuchoma sindano Hospitali ya Mbuyuni karibu na makaburi ya Kinondoni, nilifanyiwa upasuaji wa kizazi India hivyo maumivu yanatokea kila mwezi, naomba msamaha Mheshimiwa,”aliomba Wema.

Akijibu Wakili wa Serikali, Glory Mwenda alidai ni kweli mshtakiwa hakufika mahakamani kwa siku hizo lakini siku zote za kesi amekuwa akitoa taarifa hivyo aliiomba mahakama impe onyo kwa kutohudhuria sababu imeleta usumbufu.
 
Glory alidai siku nyingine asipofika wadhamini wake wafike kumwakilisha.

Wakili wake, Ruben aliomba Mahakama imsamehe mteja wake kwa usumbufu uliojitokeza na kuahidi kwamba hautajirudia.

“Tunaomba busara ya mahakama mshtakiwa abaki na dhamana yake,”alidai Ruben.

Hakimu Kasonde baada ya kusikiliza hoja za pande zote alisema atazizingatia pamoja na kiapo cha Wema kilichowasilishwa mahakamani hapo.

Alisema hawezi kutoa uamuzi siku hiyo kwani alikuwa na kazi nyingine, akaahidi kutoa uamuzi leo kisha aliamuru mshtakiwa akae mahabusu hadi leo atakapotoa uamuzi wa ama aendelee kuwa nje kwa dhamana ama amfutie dhamana.

Hakimu Maira ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2019 itakapoanza kusikilizwa ushahidi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger