Friday, 7 June 2019

Rais Magufuli, Wafanyabiashara Wajadili Fursa na Changamoto za Biashara Nchini

...
Adelina JohnBosco, MAELEZO Dodoma
Rais John Pombe Magufuli amekutana na wawakilishi wa wafanyabiashara nchini leo Ikulu Jijini Dar es salaam ili kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na jinsi ya kuzitatua kwa ajili ya kukuza uchumi kupitia sekta binafsi nchini.

Licha ya jitihada zinazoendelea kuleta uboreshaji katika sekta ya biashara, Rais ametaja uwepo wa changamoto mbalimbali kwa pande wa Serikali na wafanyabiashara wenyewe ambazo zimekuwa ni kikwazo katika kufanya biashara nchini.

Rais Magufuli amebainisha vikwazo vinavyosababishwa na wafanyabiashara kuwa ni pamoja na ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na vitendo vya rushwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazozuia uboreshaji wa sekta ya biashara nchini.

Amesema kuna kampuni 17,446 zinakwepa kodi kwa njia ya mauzo hewa ya biashara za ndani na nje, manunuzi hewa kutoka makampuni hewa na kuagiza kampuni hizo kuchunguzwa zaidi na zikithibitika kukwepa kodi zitalazimika kulipa kodi hiyo katika kipindi cha siku 30 kuanzia sasa.

''Baadhi yenu sio waaminifu mnakwepa kodi, mnatoa rushwa na wengine mmekuwa mkifanya kazi za udalali hasa kwenye biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho'' ameeleza Rais Magufuli

Changamoto nyingine kutoka kwa wafanyabiashara ni kuhujumu uchumi kwa kutokuwa wawazi katika mahesabu yao kwa kuwasilisha vielelezo tofauti vya taarifa ya fedha zinazopelekwa benki na TRA.

Aidha, amewaonya wafanyabiashara wanaobadilisha matumizi ya viwanda yaliyokusudiwa awali wakati yakisajiliwa na kuanzisha biashara nyingine pasipo kufuata utaratibu.

Upande wa Serikali, Rais Magufuli amebainisha changamoto mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa biashara nchini kuwa ni pamoja na wingi wa taasisi za udhibiti kama vile TRA, OSHA, TBS, TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuuu, Tume ya Ushindani, EWURA, na SUMATRA ambazo husababisha mwingiliano kimajukumu na kutoza tozo mbalimbali zinazofanana hivyo kudhoofisha ukuaji wa biashara nchini.

Ametaja vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wachache  wa Serikali wasio waadilifu kuwa ni miongoni mwa changamoto inayorudisha nyuma jitihada za wafanyabiashara hasa maeneo ya vizuizi barabarani, bandarini, na TRA.

Katika kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa, Rais amebainisha mikakati ya Serikali iliyoweka ikiwa ni pamoja na kuandaa kitabu cha mwomgozo na kwamba mapendekezo mbalimbali yameanza kutekelezwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya biasha nchini.

''Sasa Brela inatumia utaratibu mpya wa kusajili biashara kwa njia ya mtandao, kufuta baadhi ya ada na tozo zilizokuwa zikitozwa na taasisi za OSHA na Zima moto kabla ya kuanzisha biashara,'' amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha amezitaka mamlaka husika katika Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wakati kama ilivyofanyika kwa wafanyabiashara wakubwa.

''Wafanyabiashara wadogo na wakati ndiyo kitovu cha kukuza uchumi katika nchi, hivyo nashauri waendelezwe kama ambavyo tumeshaanza kwa kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo nchini'', alisisitiza Rsi Magufuli.

Kwa upande mwingine, Rais amezionya taasisi za kifedha kutokana na kuwa na mitaji midogo huku zikiweka masharti magumu na kutoza riba kubwa ikiwemo kuendesha shughuli zake zaidi mijini kuliko vijijini.

''Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa ikikopa fedha nyingi kwenye taasisi za kimataifa ikiwemo benki ya dunia kwa ajili ya kutoa dhamana na kuwakopesha wajasiriamali wa hapa nchini, lakini sina hakika kama fedha hizo zinawafikia walengwa,'' amehoji Rais Magufuli.

Rais amewaonya mawakala wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) nje ya nchi wanaowasababishia hasara wafanyabiashara kwa kuidhinisha bidhaa ambazo zinagundulika kuwa hazina viwango zinapokaguliwa baada ya kuingizwa nchini.

Aidha ameziagiza mamlaka husika kuangalia uwezekeno wa kuunganisha baadhi ya mifuko inayosimamia sekta ya biashara ili kuiimarisha na kupunguza gharama za uendeshaji huku akizitaka mamlaka zinazosimamia sekta ya biashara ikiwemo wizara, idara, wakala wa Serikali kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi mara moja ifikapo mwezi Julai mwaka huu, kwa kuzingatia mapendekezo yote yaliyomo katika kitabu cha mwongozo (Blue Print).

Hata hivyo, rais ametoa pongezi kwa wafanyabiashara halali wanaofuata taratibu elekezi ikiwemo kulipa kodi kwa wakati.

Mkutano huu ni mwendelezo wa mikutano inayofanywa na Rais kwa kuyahusisha makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, wachimbaji wa madini, wazee na watendaji Serikalini lengo likiwa ni kujadiliana na kuweka mikakati itakayosaidia kukua kwa uchumi kwa maslahi ya Taifa.

-Mwisho-


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger