Mwandishi wa habari wa wa siku nyingi nchini Kenya Mohammed Juma Njuguna amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu katika hospitali ya Nairobi.
Mtangazaji huyo ambaye uzoefu wake wa kazi hiyo unakaribia miongo minne alikuwa akifanya kazi kama mzalishaji wa vipindi katika kituo cha habari cha Citizen , jukumu aliloanza kutekeleza tangu 2016, Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya.
Wakenya na eneo la Afrika ,mashariki kwa jumla watamkumbuka Juma kwa kutangaza kwa kiswahili fasaha hatua ambayo ilimfanya kupokea tuzo kutoka kwa rais Mwai Kibaki mnamo tarehe 10 mwezi Machi 2010 hususan alipokuwa akilifanyia kazi shirika la habari la taifa KBC na kituo cha redio Citizen.
Aliondoka KBC na kuelekea katika kampuni ya habari ya Royal Media Services mwaka 1999 baada ya kuhudumu muongo mmoja katika shirika hilo la kitaifa.
Marafiki na mashabiki pamoja na wafanyikazi wenzake waliingia katika akaunti za mitandao yao kuomboleza kifo cha gwiji huyo wa matangazo nchini Kenya.
''Alikuwa na mbinu yake ya kipekee ya kutangaza mpira. Roho yake ilale mahali pema peponi'', alisema aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Jacob Goast Mulee.
''Nimesikitishwa na kufariki kwa rafiki yangu Juma Njuguna . Nimemjua mwandishi huyu wa muda mrefu tangu siku zetu katika kituo cha habari cha VOK sasa KBC na BBC mjini London. Natuma rambirambi zangu kwa famili yake na mashabiki. Roho yake ilale pahali pema peponi #MohammedJumaNjuguna." - aliandika Mbunge wa kamukunji Yussuf Hassan katika akunti yake ya Twitter.
"Tulikutana mara nyingi. Rafiki. Mshauri. Mtangazaji mkongwe Mohammed Juma Njuguna amefariki. Roho yako ilale pema peponi rafiki." Mwandishi wa Michezo Carol Radull alituma ujumbe wa Twitter.
Mohamed Juma Njuguna alikua mcheshi na mtu mwaminifu. Rafiki na mtangazaji mkongwe ambapo mara nynegine angewasalimia marafiki zake katika matangazo yake ya mpira. Ninamuenzi mimi na mashabiki wa michezo. Natuma rambi rambi zangu kwa familia yake, aliandika mwanahabari wa Michezo wa gazeti la Daily Nation, David Kwalimwa katika mtandao wake wa twitter.
0 comments:
Post a Comment